Mkutano wa kilele wa Jumuiya ya Madola-Commonwealth. | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 11.12.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Timu Yetu

Mkutano wa kilele wa Jumuiya ya Madola-Commonwealth.

Mkutano wa viongozi wakuu wa taifa na serikali wa jumuiya ya madola-Commonwealth unafunguliwa leo katika mji mkuu wa Uganda-Kampala, mada kuu zikiwa Pakistan na Zimbabwe.

default

Malkia Elizabeth II

Mkutano huo utakaofunguliwa na Malkia wa Uingereza Elizabeth wa pili, unatarajiwa miongoni mwa mengine kufikia uamuzi wa kuikubali Rwanda kuwa mwanachama mpya au la.

Ombi la Rwanda ambayo ni mzungumzaji Kifaransa la kutaka kujiunga na Jumuiya ya madola inayoyakusanya hasa mataifa yaliokua zamani makoloni ya Uingereza , linaungwa mkono na serikali ya Uingereza yenyewe na hayo yamethibitishwa na afisa mmoja wa ngazi ya juu aliyesema kwamba kwa mtazamo wao Rwanda ni mshirika mwenye nguvu barani Afrika.

Mbali na Rwanda tayari Msumbiji ambayo ni koloni la zamani la Ureno ni mwanachama wa jumuiya hiyo na pia Kamerun kunakozungumzwa lugha zote mbili Kiingereza na Kifaransa kama lugha rasmi. Moja kubwa katika masharti ya kujiunga ni kukitambua Kiingereza kuwa lugha nyongeza rasmi, kuheshimu haki za binaadamu na msingi ya demokrasia, lakini utaratibu wa kufikia kukubaliwa uwanachama unaweza kuchukua miaka kadhaa.

Rais Paul Kagame wa Rwanda alikuweko Kampala Jumanne kabla ya mkutano huo wa viongozi na kuambia mkutano wa kibiashara kwamba uchumi wa nchi yake hauwezi kuendelea ikiwa itajiweka tu katika ushirikiano wa kikanda au wa bara hilo pekee.

Mbali na uwanachama wa Rwanda, masuala mengine makuu yanayotarajiwa kuugubika mkutano huo wa kilele ni Zimbabwe na Pakistan .

Katika suala la Zimbabwe ambako mgogoro wa kisiasa kati ya serikali ya rais Mugabe na chama kikuu cha upinzani Movement for Democratic change-MDC bado unaendeklea huku pande hizo zikiwa katika mazungumzo ya kusaka suiluhisho yanayoongozwa na Afrika kusini, kiongtozi wa MDC Morgan Tsvangirai aliwasili Kampala kujaribu kuwarai viongozi wa nchi wanachama kumshinikiza Rais Mugabe ili suluhisho la haraka lipatikane na Zimbabwe irudi kuwa sehemu ya jamii ya kimataifa.

Tsvangirai akasisitiza kwamba mgogoro wa Zimbabwe unahitaji mshikamano wa jamii ya kimataifa.

Kwa upande mwengine wadadisi wanasema kuwa utakua pia ni nafasi kwaRais Yoweri Museveni kuiweka nchi yake katika aramani na kuvutia wawekezaji na kukuza utalii.

Lakini kitakachomulikwa pia kandoni mwa hali hiyo, ni suala zima la demokrasia na haki za binaadamu katika taifa hilo la Afrika mashariki.

Tayari chama kikuu cha upinzani Forum for Democaratic Change –FDC, kimesema hiyo ni nafasi ya kuuzindua ulimwengu kuhusu kukandamizwa kwa uhuru wa raia nchini Uganda.

Hoja hiyo pamoja na hayo inapingwa na msemaji wa Museveni Tamale Mirundi aliyesema kuheshimiwa haki za binaadamu nchini Uganda kunaonekana wazi na mfano mmoja wapo ni kuwa hata wapinzani wameruhusiwa kuandamana wakati wa mkutano huo.

Hata hivyo itakumbukwa kwamba mnamo mwezi Aprili mwaka huu, askari wa usalama waliivamia mahakama kuu na kuwakamata watuhumiwa wa mashitaka ya uhaini ambao tayari mahakama iliamuru waachiwe kwa dhamana, huku askari hao wakiwapiga mawakili, likiwa tukio la pili la aina hiyo kuwahi kutokea katika kipindi cha miaka miwili.

Museveni aliyekua akizingatiwa kama kizazi cha uongozi mpya barani Afrika mnamo miaka ya nyuma, aliwavunja moyo wengi nchini mwake na nchi za nje, alipoongoza kampeni ya kubadilishwa katiba 2005 ili kumruhusu kuendelea kuwa rais bila ya kipingamiza cha muhula maalum.

Mkutano huo wa kilele wa Jumuiya ya madola utamalizika siku ya Jumapili.

 • Tarehe 11.12.2007
 • Mwandishi Mohammed AbdulRahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CQkV
 • Tarehe 11.12.2007
 • Mwandishi Mohammed AbdulRahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CQkV

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com