Mkutano wa Kilele baina ya Russia na Umoja wa Ulaya | Matukio ya Kisiasa | DW | 27.06.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Mkutano wa Kilele baina ya Russia na Umoja wa Ulaya

Rais Dmitry Medvedev wa Russia anakutana na wakuu wa Umoja wa Ulaya

Rais Dmitry Medvedev wa Russia

Rais Dmitry Medvedev wa Russia

Rais Dmitry Medvedev wa Russia ameanza kufanya mazungumzo na viongozi wa nchi za Umoja wa Ulaya hii leo ambayo yanatarajiwa yataanzisha tena mashauriano juu ya mkataba wa ushirika baada ya uhusiano kati ya pande hizo mbili kuwa baridi. Wachunguzi wanasema mazungumzo hayo yatapima kama kuna utashi wa kisiasa wa kuyakiuka matatizo kadhaa katika masuala ya nishati na usalama kabla ya mashaurriano juu ya mkataba huo kuanza hapo July 4 mjini Brussles.

Wanadiplomasia walioko Brussels wanatarajia kwamba Rais Medvedev ataonekana kuwa mshirika aliye mlaini zaidi kulinganisha na mtangulizi wake, Vladimir Putin, ambaye msimamo wake mkakamavu ulizidisha kuwa mbaya uhusiano wa nchi yake na nchi za Umoja wa Ulaya ambazo zamani zilikuwa chini ya ushawishi wa Urussi. Poland na Lithuania zilipinga majaribio ya mwanzo ya kupatikana makubaliano kutokana na ugomvi wao wa kibiashara na Russia na pia namna Russia inavojiingiza katika mizozo ya nchini Georgia na Moldavia. Lakini Rais Medvedev haoneshi kutaka kuyachafua mambo zaidi. Hata hivyo, taarifa za washauri wake wakuu zimelaumu majaribio ya nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya kuingiza siasa nyingi katika uhusiano baina ya pande mbili. Pande zote mbili zinatafutiana mkatba huo uwe wa aina gani. Mratibu wa siasa za kigeni za Umoja wa Ulaya, Javier Solana, amesema moja kati ya masuala muhimu ya uhusiano wa pande mbili hizo ni yale yanayoambatana na nishati, kwani pande hizo mbili zinategemeana katika suala hilo. Umoja wa Ulaya unahisi suala la nishati lichomoze wazi wazi katika mkataba huo mpya.

Kufanyika mkutano huu wa kilele katika mji wa Khanty-Mansiysk ulio na utajiri wa mafuta huko Siberia ni alama, kwani eneo hilo linatoa asilimia 40 ya mafuta yanayosafirishwa nje na Russia, na nchi za Umoja wa Ulaya ndio wateja wakubwa. Umoja wa Ulaya unataka mazungumzo hayo yaingize malalamiko ya Georgia kwamba Russia inawasaidia waasi katika mkoa wa Abkhazia. Rais Medvedev alikutana jana na kiongozi wa mkoa huo unaopigania kujitenga na akasisitiza juu ya kuambatana na mkataba wa sasa wa kuweko majeshi ya kulinda amani ya Umoja wa Mataifa katika sehemu hiyo. Mkataba huo unaruhusu wanajeshi wa Russia kupiga doria katika mkoa huo ulio na utawala wake wa ndani. Umoja wa Ulaya unashikilia kuweko mkataba mpya wa amani juu ya mkoa huo na ambao utapunguza mchango wa Russia wa kuweka amani, lakini pendekezo hilo lilikataliwa na Russia.

Katika mkutano huu Umoja wa Ulaya utataka uhakikishiwe zaidi usalama wa kuuziwa mafuta na gesi ya ardhini kutoka Russia. Pia ikumbukwe kwamba zaidi ya asilimia 50 ya uwekezaji wa moja kwa moja huko Russia unatokea nchi za Umoja wa Ulaya. Mkakati wa siku zijazo wa Umoja wa Kujihami wa NATO unaitia wasiwasi Russia. Licha ya hayo, Russia haipendi kufanywa kama mtoto wa shule anayefunzwa na nchi za Magharibi juu ya maedeleo inayofanya kuhusu demokrasia. Na hasa wakati huu ambapo Russia inajiamini zaidi kutokana na utajiri wake wa mafuta na gesi ya ardhini.

Umoja wa Ulaya katika mazungumzo haya unawakilishwa na Janez Jansa, waziri mkuu wa Slovenia, nchi ambayo sasa inashikilia urais wa Umoja wa Ulaya, rais wa komisheni ya Umoja huo, Jose Manuel Barroso, na mkuu wa siasa za kigeni, Javier Solana.

 • Tarehe 27.06.2008
 • Mwandishi Othman, Miraji
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/ERv4
 • Tarehe 27.06.2008
 • Mwandishi Othman, Miraji
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/ERv4
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com