Miaka 25 tangu kutokea mauaji katika kambi za wakimbizi za Sabra na Shatila nchini Lebanon | Matukio ya Kisiasa | DW | 18.09.2007
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Miaka 25 tangu kutokea mauaji katika kambi za wakimbizi za Sabra na Shatila nchini Lebanon

Mapambano ya Wapalastina kutaka kuwa na taifa lao yameigharimu nchi jirani ya Lebanon. Miaka 25 iliopita, Lebanon ilipata hasara kubwa kutokana na vita baina ya Israel na wapiganaji wa Kipalastina waliokuweko Libanon, na hata kusababisha kuhamishwa hao wapiganaji kutoka nchi hiyo, na pia kutokea yale mauaji ya kikatili ya wakimbizi wa Kipalastina katika kambi za Sabra na Shatila mjini Beirut.

Maiti za wakimbizi wa Kipalastina katika kambi za Sabra na Shatila karibu na Beirut, Lebanon

Maiti za wakimbizi wa Kipalastina katika kambi za Sabra na Shatila karibu na Beirut, Lebanon

Hadi mwaka 1993, pale mkataba wa Oslo juu ya amani ya Mashariki ya Kati ulipotiwa saini, Chama cha PLO cha rais wa Wapalastina, Yasser Arafat, kilikuwa chama cha ukombozi. Katika maeneo ya Wapalastina yaliotekwa na Israel, chama hicho kilikuwa hakijafanikiwa sana katika mapambano dhidi ya Israel. Kwa hivyo, kilijaribu, kutokea Jordan, kuendesha mapambano dhidi ya dola ya Kiyahudi. Hapo tena kukatokea mwaka 1970 kile kilichoitwa Septemba Nyeusi, ambapo chama hicho kilifukuzwa kutoka Jordan kwa tuhuma kwamba kilikuwa na mpango wa kuupinduwa ufalme wa Jordan, na pia kujaribu kutaka kuwa dola ndani ya dola. Hapo tena Chama cha PLO kikahamia Libanon ambako huko kiliendesha mapambano zaidi ya kisilaha dhidi ya Israel. Aliyekuja kuwa waziri mkuu wa Israel, Ariel Sharon, alikuwa anangoja tu nafasi ya kujiingiza, na nafasi hiyo ilipatikana miaka 25 iliopita pale Chama cha PLO kilipofukuzwa kutoka Kusini mwa Libanon. Wa-Israeli hawajatosheka na hilo, walitaka hasa kukisagasaga kabisa chama cha PLO, hivyo kuondosha kabisa kitisho kilichokuwa kinaikabili nchi yao.

Kutoka juu kwenye paa la jengo al Shirika la Umeme la Beirut, mtu aliweza kuiona kwa uzuri bandari ya mji mkuu wa Beirut. Na jambo hilo lilikuwa muhimu katika mwezi wa Agosti mwaka 1982. Hapo wanajeshi na waandishi wa habari wa Ki-Israeli walijikusanya, na baadae akawasili waziri wa ulinzi, Ariel Sharon. Watu wote walitaka kushuhudia nini kitafanyika hapo Bandarini. Ikilindwa na wanajeshi wa Kifaransa, ambao walishuka Beirut hapo Agosti 21, milolongo ya malori yaliojaa wapiganaji wa PLO ilikuwa inapita na kuingia katika meli ya mwanzo kati ya meli nyingi zilizokodiwa kutoka kampuni ya Cyprus inayoitwa Solomonides. Watu wengine walikuwa wanangoja nje ya bandari. Wote walikuwa wanataka kusaidia kumalizika kwa moja wapo ya ukurasa mbaya kabisa katika historia ya Beirut.

Kwa wiki kadhaa, wanajeshi wa Israel waliizingira na kuishambulia kwa mabomu sehemu ya Magharibi ya mji wa Beirut ambako Chama cha cha Ukombozi wa Palastina, chini ya Yasser Arafat, kilijificha. Hapo palikuwa ni mahala pa mwisho walikokimbilia wapiganaji wa Kipalastina baada ya hapo kabla kufukuzwa kutoka Kusini mwa Libanon. Ariel Sharon alikuwa ameazimia kuiangamiza PLO kabisa huko Libanon, na njia ya kufanya hivyo ilikuwa kuivamia nchi jirani ya Lebanon. Israel ilianza kuyatuma majeshi nchini humo hapo Juni 6, na si muda mrefu baadae wanajeshi wa Israel walikuweko Beirut na kuizingira sehemu ya magharibi ya mji huo. Vilifuata vita vya wiki nzima ambavyo viliwatia katika shida kubwa raia wa mji wa Beirut. Punde baadae ikaja fikra kwamba suluhisho litawezekana tu kupatikana pindi Chama cha Ukombozi wa Palastina,PLO, kitaondoka Libanon.

Philip Habib, mshauri na mwakilishi wa Kimarekani juu ya Mashariki ya Kati, mtu aliyekuwa na uzoefu mkubwa wa masuala ya kidiplomasia, alitayarisha utaratubu wa wapiganaji wa PLO kuondoka kutoka Libanon. Kikosi cha mchanganyiko wa wanajeshi wa kutoka Ufaransa, Italy,Uengereza na Marekani kilihakisha jambo hilo linafanyika na baadae kikaikamata sehemu ya magharibi ya mji wa Beirut. Majeshi hayo yaliwasili Libanon Agosti 21 na tarehe 30 wapiganaji wa PLO wakaanza kuondoka. Na japokuwa Ariel Sharon miaka baadae, katika mahojiano, alisikitika kwamba wakati huo hajamuuwa Yasser Arafat, hata hivyo, waziri huyo wa ulinzi wa Israel alijihisi amefikia lengo lake:

+Katika vita hivi, Israel haijashindwa. Chama cha kigaidi cha PLO kimeangamizwa kabisa. Hakiko tena kama chama cha kigaidi cha PLO.+

Wapiganaji wa Yasser Arafat waliihama Beirut na kwenda Tunis, mji mkuu wa Tunisia, Yemen ya Kusini, Misri na katika nchi nyingine za Kiarabu. Sehemu yao, akiwemo pia mkuu wa PLO, Yasser Arafat, walichipuka tena baadae kaskazini mwa Libanon, wakitaka kuendeleza upya mapigano dhidi ya Israel. Kama vile Yasser Arafat alivosema pale alipoondoka Beirut:

.

+Nabeba dhamana juu ya mabega yangu kuendelea na safari hii ndefu. Mimi nimekuahidini kwamba safari hii itaendelezwa hadi pale tutakapoweza kuunda dola yetu huru, mji mkuu wake ukiwa Jerusalem.+

Arafat na Chama cha PLO bado viko mbali na lengo hilo. Lakini Lebanon haijawa tena katika utulivu. Vikosi vya lile jeshi la kimataifa viliondoshwa baada ya wapiganaji wa PLO kuhama, kwa matarajio kwamba hali ya kawaida itarejea. Matumainio hayo alikuwa nayo Rais wa Marekani, Ronald Reagan, hapo Septemba 30:

+Kuondoashwa wapiganaji wa PLO kutoka Beirut sasa kumemalizika, na sasa tunaweza kuwasaidia Wa-Lebanon kuijenga upya nchi yao iliovurugika kutokana na vita. Tunawajibika sisi na kwa ajili ya vizazi vijayo kutenda kwa haraka na kujenga juu ya matokeo haya. Libanon ilio na utulivu, tena isiogawika, ni shuruti ya matarajio yetu ya amani katika eneo hili. Watu wa Lebanon wanastahiki yalio bora kabisa kutoka kwetu na kutoka kwa jamii ya kimataifa ili kwamba maafa ya miaka michache iliopita yabadike kuwa ni kuchomoza kupya kwa juwa litajkaloleta matumainio.

Israel iliendeklea kuikalia sehemu ya magharibi ya Beirut, na siku chache baadae rais aliyechaguliwa, Bashir Gemayel, aliuliwa, na siku mbili baadae yakaanza mauaji wa Sabra na Shatila. Baada ya kuondoka wapiganaji wa PLO, kambi za wakimbizi wa Kipalastina zilibakia bila ya ulinzi wa watu wenye silaha, hivyo wanamgambo wa Kikristo waliingia katika kambi hizo mbili wakawauwa wanawake, watoto na vikongwe. Idadi ya watu waliouliwa haijulikani, lakini inasemekana baina ya mamia fulani hadi 3500. Kwa vyovyote, mauaji hayo yalisababisha malalamiko makali duniani kote, na huko Israel kuliendeshwa uchunguzi rasmi ambao uliwekea alama ya kuuliza juu ya uwezo wa Ariel Sharon kukamata wadhifa rasmi. Marekani pamoja na Italy na Ufaransa zilituma tena jeshi la kimataifa hadi Libanon na yakabakia huko hadi Februari 1984 yalipopata mapigo makubwa. Kuondoka wapiganaji wa PLO kulikuwa ni kisa, lakini suluhisho la tatizo halijapatikana si kwa Wapalastina au Israel, si kwa Libanon na wala wakaazi wa mji wa Beirut.

Insert: Music… Fayruz.ala Jisr il lawaziyaah

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com