1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel kukutana na Putin

Sekione Kitojo
18 Agosti 2018

Rais wa Urusi Vladimir Putin atakutana na kansela wa Ujerumani Angela Merkel leo Jumamosi(18.08.2018)kwa mazungumzo juu ya  mizozo nchini Ukraine na Syria, pamoja na mradi wa bomba la gesi ambao unashutumiwa na Marekani.

https://p.dw.com/p/33LbT
Russland Sotschi - Wladimir Putin und Angela Merkel
Picha: Reuters/S. Karpukhin

Putin amewasili  nchini  Ujerumani  baada  ya  kutembelea  shamba la mizabibu  nchini  Austria  kuhudhuria  harusi  ya  waziri  wa  mambo  ya  kigeni Karin Kneissl ambaye  anaoana  na  mfanyabiashara  Wolfgang Meilinger.

Merkel  ameonya  jana  Ijumaa  dhidi  ya  matarajio  makubwa  kutoka  katika majadiliano  yake  na  Putin katika  makao  makuu  ya  serikali  ya  Meseberg, lakini  amesema  nchi  hizo  mbili zinahitaji kuendelea , "kuwa  na  majadiliano kila  mara" kuhusiana  na  orodha  ndefe ya  matatizo zinazokabiliana  nayo.

Deutschland Bundeskanzlerin Angela Merkel
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel Picha: picture-alliance/AP Images/J. Meyer

"Ni mkutano  wa  kazi ambao  hakuna  matokeo  maalum yanayotarajiwa," amewaambia  waandishi  habari. Viongozi  hao  wawili  walikutana  mara  ya mwisho mjini  Sochi mwezi  Mei  na  walishindwa  kuondoa  tofauti  zao.

Lakini Juergen Hardt, msemaji wa  sera za  mambo  ya  kigeni  katika  kundi la  vyama  vya  kihafidhina  vinavyoongozwa  na  kansela  Merkel , na  Achim Post , mjumbe  mwandamizi  wa  chama  cha  Social Democrats SPD, chama  mshirika  katika  serikali  ya  Ujerumani , walikuwa  na  matumaini.

Hatua zinazochukuliwa

"Tunaweza  kwa  tahadhari kuwa  na  matumaini," Hardt  aliliambia  gazeti  la Stuttgarter Zeitung katika  mahojiano  yaliyochapishwa  leo  Jumamosi. "rais wa  Urusi amejiingiza  mwenyewe  katika  hali  ya  kufikia  mwisho  nchini Syria  na  mashariki  mwa  Ukraine, na  anahitaji  washrika  wa  kimataifa. Kwa hilo anahitaji  kuchukua  hatua.

Deutschland Merkel und Putin in Dresden - Begrüßung
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel (kulia) na rais wa Urusi Vladimir Putin(kushoto)Picha: picture-alliance/dpa/M. Hiekel

Afisa  mwandamizi  wa  serikali  ameliambia  gazeti : "Kumekuwa  na  hatua zinazochukuliwa," lakini  hakutoa  maelezo  zaidi.

Post  amesema   katika  taarifa  kwamba  anatarajia  Merkel  na  Putin kuangalia  suluhisho  linalowezekana  lililo katika  misingi ya  maslahi  ya pamoja. "Katika  dunia  ambayo  inaongezeka  hali  ya  sintofahamu, tunapaswa  kuzungumza  hususan  na  washirika  ambao  ni  wenye  matatizo kama  Urusi," amesema.

DW Karikatur Sergey Elkin - Putin vor dem Treffen mit Angela Merkel
Mchoro wa kibonzo , katika mkutano kati ya Putin na MerkelPicha: DW/S. Elkin

Urusi  na  mataifa  ya  magharibi  zinabaki kutofautiana  kuhusiana  na  hatua ya  Urusi  kulinyakua  jimbo  la  Crimea  kutoka  Ukraine  mwaka  2014 na kuzuka  mzozo  kati  ya   watu wanaotaka  kujitenga  wanaoungwa  mkono  na Urusi  katika  eneo  la  mashariki  mwa  nchi  hiyo  wakipambana  na   jeshi  la Ukraine. Kuhusu  Syria , Ujerumani  inamtaka  Putin kukamilisha  makubaliano ya  kudumu  ya  kusitisha  mapigano  nchini  humo  kwa  makubaliano  na Marekani. Merkel  jana  Ijumaa  alisema  mkutano  wa  pande  nne  kuhusu Syria unaoihusisha  Ujerumani , Urusi, Uturuki  na  Ufaransa  unawezekana kufanyika.

Mwandishi: Sekione  Kitojo / rtre

Mhariri: Jacob Safari Bomani