1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel: COVID-19 ni changamoto kubwa ya Ujerumani

Grace Kabogo
19 Machi 2020

Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel amesema nchi hiyo inakabiliwa na changamoto kubwa tangu Vita Kuu ya Pili ya Dunia katika mapambano dhidi ya virusi vya corona.

https://p.dw.com/p/3ZgJY
Deutschland Berlin | Coronavirus | Ansprache Angela Merkel, Bundeskanzlerin
Picha: picture-alliance/dpa/Bundesregierung/S. Kugler

Akilihutubia taifa kwa njia ya televisheni, Merkel amewataka wananchi kutambua jukumu lao katika kuzuia kuenea kwa maambukizi ya virusi hivyo.

Ujerumani ni moja ya nchi za Ulaya ambazo zimeathirika kwa kiasi kikubwa na mripuko wa COVID-19. Katika hotuba hiyo ya aina yake na isiyo ya kawaida aliyoitoa Jumatano jioni, Merkel aliwasihi wananchi kuendelea kufuata maagizo yaliyotolewa na serikali ya kubakia majumbani na ametoa wito kwa taifa kuungana pamoja.

Hotuba hiyo ameitoa siku moja baada ya Ujerumani kutangaza hatua mpya na madhubuti za kupunguza kuenea kwa virusi hivyo. Siku ya Jumatano Ujerumani ilirekodi ongezeko la zaidi ya visa 1,000 vya virusi vya corona ikilinganishwa na siku moja iliyopita. Kwa mujibu wa kituo cha utafiti cha John Hopkins, watu 12,300 wameambukizwa virusi hivyo nchini Ujerumani na wengine 28 wamekufa, huku zaidi ya watu 100 wakiwa wamepona.

Changamoto kubwa

Merkel amesema hali ni mbaya na inapaswa kuchukuliwa kwa umakini mkubwa. Amebainisha kuwa tangu kuungana kwa Ujerumani Mashariki na Magharibi, na tangu Vita Kuu ya Pili ya Dunia, Ujerumani haijawahi kukumbwa na changamoto kubwa kama ya mripuko wa virusi vya corona. Tofauti na nchi nyingine kama vile Italia, Ufaransa na Uhispania, Ujerumani haijaweka marufuku ya nchi nzima inayowazuia watu kuondoka majumbani isipokuwa kwa lengo la kwenda kazini, kupata matibabu au kununua chakula.

Coronavirus-COVID-19 Eindrücke aus einer leeren Stadt¦. Es ist traurig. Die Stadt Stuttgart an einem Mittwoch Vormittag
Moja ya maeneo ya mji wa Stuttgart likiwa halina watuPicha: imago images/Lichtgut/L. H. Piechowski

Hata hivyo, Ujerumani imeifunga mipaka yake kwa raia wasiotoka kwenye nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya, imezuia safari na imeamuru kusimamishwa kwa shughuli nyingi za umma, kufungwa shule pamoja na biashara. Merkel amewataka wananchi kutopuuza mripuko wa virusi hivyo na kwamba serikali inahitaji mchango wa kila mtu kusaidia katika kudhibiti COVID-19.

Mapema Jumatano, wataalamu wa afya wa Ujerumani walionya kuwa idadi jumla ya watu watakaoambukizwa virusi vya corona inaweza ikafikia milioni 10 katika miezi ijayo, iwapo wananchi hawatofuata hatua zilizowekwa katika kupunguza kuenea kwa virusi hivyo.

Pongezi kwa kazi inayofanywa

Aidha, Merkel amepongeza kazi inayofanywa na wataalamu wa afya na wafanyakazi katika maduka makubwa na amewahakikishia Wajerumani kwamba chakula kitaendelea kuuzwa kwenye maduka mbalimbali. Wiki iliyopita Ujerumani ilishuhudia watu wakinunua bidhaa kwa wingi kutokana na hofu.

Ama kwa upande mwingine, Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa zaidi ya watu milioni 24 duniani huenda wakakosa ajira kutokana na athari ya janga la COVID-19. Ripoti ya Shirika la Kazi Duniani, ILO, imeeleza kuwa ukosefu wa ajira ulimwenguni unaweza ukaongezeka hadi watu milioni 5.3 kwa kiwango cha chini na milioni 24.3 kwa kiwango cha juu.

Siku ya Jumatano Italia iliripoti karibu vifo 500 vya virusi vya corona, idadi kubwa kabisa ya vifo kwa siku moja ambayo haijawahi kushuhudiwa katika taifa lolote lile duniani tangu kuzuka kwa virusi hivyo nchini China Desemba mwaka uliopita.

Ureno imetangaza siku 15 za hali ya hatari kutokana na hatua zilizochukuliwa na nchi jirani za Uhispania na Ufaransa. Rais wa Ureno, Marcelo Rebelo de Sousa amesema hali hiyo ni demokrasia ya kujaribu kuzuia usumbufu unaoweza kujitokeza kwenye maisha ya watu.

Portugal Präsident Marcelo Rebelo de Sousa
Rais wa Ureno, Marcelo Rebelo de SousaPicha: Reuters/M. F. Lopes

Polisi nchini Ufaransa Jumatano imewatoza faini zaidi ya watu 40,000 kwa kukiuka amri iliyowekwa ya kubakia nyumbani, ikiwa ni siku ya kwanza tangu nchi hiyo kutangaza marufuku ya nchi nzima. Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ufaransa, Christophe Castaner amesema faini hiyo ni kuanzia Euro 35 hadi 135.

China imesema itaupatia Umoja wa Ulaya vifaa maalum milioni 2 vya kufunika uso, vifaa 200,000 maalum vya kujikinga na virusi vya corona aina ya N95 pamoja na vifaa 500,000 vya kupima virusi hivyo. Rais wa Marekani Donald Trump, leo anatarajiwa kusaini sheria ya ulinzi ya uzalishaji ambayo inairuhusu serikali kuongeza utengenezaji wa vifaa vya kufunika uso na vifaa maalum vya kupitisha hewa na kujikinga.

Wakati huo huo, China imesema kuwa haijarekodi kisa chochote kipya cha virusi vya corona kwenye jimbo la Hubei, ambako virusi hivyo vilianzia katika kipindi cha muda wa saa 24. Aidha hakuna mgonjwa yeyote aliyeripotiwa kuambukizwa COVID-19 katika nchi nzima ya China, hii ikiwa ni mara ya kwanza katika muda wa wiki nane zilizopita. 

Hata hivyo, Tume ya Taifa ya Afya imerekodi visa vipya 34 vya wagonjwa walioingia nchini humo kutoka nchi za nje. China imeanzisha hatua kadhaa za kuzuia mripuko wa pili wa COVID-19, ikiwemo kuwaweka kwa lazima katika karantini raia wa kigeni wanaowasili kwenye mji mkuu wa Beijing, pamoja na kubadilisha baadhi ya safari za ndege za ndani.
 

(DPA, AP, AFP, DW)