Mazungumzo ya kuundwa serikali ya muungano Magazetini | Magazetini | DW | 08.01.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Mazungumzo ya kuundwa serikali ya muungano Magazetini

Mazungumzo ya kuundwa serikali ya muungano mjini Berlin, jinsi warepublican walivyosimama kidete nyuma ya rais wa Marekani Donald Trump na juhudi za kupunguza mivutano kati ya Uturuki na Ujerumani magazetini

Tunaanzia Berlin ambako jana yameanza rasmi mazungumzo ya kutathmini kama vyama ndugu vya klihafidhina CDU na CSU pamoja pia na SPD wanaweza kuunda serikali imara ya muungano, miezi zaidi ya mitatu baada ya uchaguzi mkuu. Duru hii ya sasa ya mazungumzo imepangwa kuendelea kwa siku tano. Gazeti la "Saarbrücker Zeitung" linaandika: "Kazi kwake sasa kansela Angela Merkel. Kwasababu yeye ndie atakaekula hasara kubwa zaidi ikiwa mazungumzo kati ya CDU, CSU na SPD hayatafanikiwa hadi mwishoni mwa wiki hii kuleta tija na kufungua njia ya kuundwa serikali ya muungano. Hali hiyo itamaanisha mwisho wa mhula wake kama kansela. Merkel amepindukia kilele cha madaraka yake. Na hilo analitambua. Na ndio maana atafanya kila la kufanya ili serikali ya muungano wa vyama vikuu iundwe. Hata kama baadae, na kama ilivyodhihirika katika mazungumzo ya kuunda serikali ya muungano wa Jamaica, kati ya CDU, CDU, waliberali wa FDP na walinzi wa mazingira die Grüne, watu watajiuliza, alama ya vyama ndugu vya kihafidhina iko wapi?"

Mtindo wa utawala wa Merkel umedhoofika

Na chama cha Social Democrat nacho pia kina majukumu yake linaandika kwa upande wake gazeti la "Weser-Kurier: Majukumu ya kitaifa mabegani mwa SPD hayahusiki pekee na kutawala, bali pia kuhakikisha utulivu na kuongoza upande wa upinzani. Majukumu ya kitaifa ya Angela Merkel yanahusika na kuunda serikali imara hata kama hatima yake binafsi ya kisiasa ina mipaka. Mtindo wake wa kutawala, au bora tuseme wa kuongoza umedhoofika, kama ulivyokuwa umedhoofika mfumo wa utawala wa Helmut Kohl baada ya miaka 16 madarakani. Ni ishara ya udhaifu, au pengine ya woga inayojitokeza anapotaka kwa kila hali kuiokoa serikali ya muungano wa vyama vikuu."

Trump anatawala peke yake au vipi au anaongozwa ?

Haipiti siku moja bila ya kusikia chochote kutoka Marekani, tangu nchi hiyo ilipojipatia rais mpya takriban mwaka mmoja uliopita. Hata hivyo imani ya wahafidhina kwa rais wao haikutetereka, linaandika gazeti la "Leipziger Volkszeitung" na kuendelea : "Kama ilivyo hivi sasa, msikamano wa wahafidhina wa Marekani ulidhihirika kuwa imara tu wakati wa utawala wa Ronald Reagan. Idadi kubwa ya wapiga kura wanaonyesha wanaridhika sana na yanayoendelea. Sehemu nyengine ya wananchi ambao idadi yao inazidi kuongezeka wanajiuliza lakini, anaeitawala nchi yao ni nani hasa? Eti ni mwenye kichaa Trump, au kundi kundi la watu fulani walioko nyuma yake wanaofurahikia vituko vyake na kujivunia uangalifu? Majibu yote mawili hayamfanyi mtu kuondowa taharuki."

Ujerumani na Uturuki kupunguza mivutano

 Mada yetu ya mwisho magazetini imehusika na mkutano wa jumapmosi iliyopita kati ya waziri wa mambo ya nchi za nje wa Uturuki Mevlüt Cavosoglu  na mwenzake wa Ujerumani Sigmar Gabriel mjini Goslar nchini Uturuki. Gazeti la "Emder Zeitung linaandika: "Unapowaona wanasiasa hao wawili  mjini Goslar utafikiri kila kitu ni barabara. Sivyo lakini kabisa.  Na hali itaendelea kuwa hivyo kwa wakati wote ule ambapo nchini Uturuki watu wanaendelea kushikiliwa bila ya sababu; Mfano wa ripota wa gazeti la Ujerumani die Welt Deniz Yücel, anaeshikiliwa karibu mwaka mmoja sasa nchini Uturuki. Watu wasifikirie kamba kwa kukubali kuhudhuria mkutano huo nchini Uturuki, Ujerumani inaonyesha kuuelewa yanayotokea Uturuki, mwanachama wa jumuia ya kujihami ya NATO, tangu njama iliyoshindwa ya mapinduzi mwaka 2016.

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir / Inlandspresse

Mharir. Mohammed Abdul-Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com