Mawaziri washindwa kuafikiana kuhusu uhamiaji | Matukio ya Kisiasa | DW | 19.07.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Mawaziri washindwa kuafikiana kuhusu uhamiaji

Mkutano wa mawaziri wa Umoja wa Ulaya huko Helsinki Finland, Alhamis, ulishuhudia Ujerumani na Ufaransa kushindwa kupata mwafaka wa mpango wa muda na mataifa mengine ya Umoja wa Ulaya wa kuwagawanya wahamiaji.

Mkutano huu umefanyika huku kukiwa na juhudi za kuyasaidia mataifa kama Italia kukabiliana na wanaowasili kutafuta hifadhi.

Pendekezo la Ujerumani na Ufaransa linataka kubuniwe muungano wa nchi ambazo kwa hiari zitakuwa tayari kuwaruhusu wahamiaji kila wanapoteremka kutoka kwenye meli za uokoaji hadi mwezi mwezi wa Oktoba.

Baadhi ya mataifa wanachama walifikiri kwamba mkutano huo ungeyashawishi mataifa kama Italia kuunga mkono pendekezo hilo. Lakini Waziri wa mambo ya ndani wa Italia Matteo Salvini ametoa taarifa akielezea upinzani wa Italia na nchi zengine kwa pendekezo hilo.

Salvini hatotia saini makubaliano yanayosema Italia ndio kituo cha kuwasili wahamiaji

Hoja kuu kwa Salvini ni kwamba hatua hizo zinazochukuliwa zinashuhudia Italia kuwa kituo cha kikuu cha kuwasili kwa wahamiaji.

Finnland, Helsinki: Matteo Salvini (picture-alliance/S. Cavicchi)

Waziri wa mambo ya ndani wa Italia Matteo Salvini

"Italia haiwezi kuwa kituo cha kuwasili kwa wahamiaji kama ilivyoelezewa kwa kuwa hiyo ina maana kwamba wahamiaji wote watawasili Italia au Malta. Siwezi kabisa kutia saini makubaliano yanayosema kuwa kila mmoja ni sharti awasili nchini mwangu kwasababu hatuwezi kuwategemea katika suala la kuwasambaza katika nchi zengine," alisema Salvini.

Serikali ya Italia inayojali fikra za wananchi wake imekataa kukubalia meli za wahamiaji waliookolewa kutia nanga katika bandari yake iwapo wahamiaji hao watakuwa wanachukuliwa na nchi chache tu za Umoja wa Ulaya.

Mkuu wa Kamisheni ya uhamiaji ya Umoja wa Ulaya Dimitris Avramopoulos amewataka mawaziri waungane badala ya kuwa na fikra za kibinafsi ambazo zitaleta matatizo makubwa baadae. Amewaambia kwamba watahukumiwa na kauli ya raia wa nchi za Umoja wa Ulaya iwapo watashindwa kuafikiana kuhusiana na jinsi ya kukabiliana na wahamiaji wapya wanaowasili.

Waziri wa Ufaransa asema juhudi zaidi zinahitajika kupatikana kwa suluhu

Licha ya yote hayo Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani Horst Seehofer amesifu hatua zilizopigwa katika mazungumzo hayo ambayo hayakuwa rasmi huko Helsinki.

Horst Seehofer Porträt Interview (DW/B. Riegert)

Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani Horst Seehofer

Lakini waziri mwenzake wa Finland Maria Ohisalo mazungumzo hayo yalikuwa ni mwanzo tu na kwamba juhudi zaidi zinahitajika.

Waziri wa mambo ya ndani wa Ufaransa Christophe Castaner amesema kuanzia mwanzo baadhi ya mawaziri walikataa kuwachukua wahamiaji, huku wengine wakitaka mshikamano zaidi katika suala hilo na wengi wakaelezea wasiwasi wao kwamba wakiwachukua wahamiaji itakuwa ni kama kuwapa motisha watu wengi zaidi kujaribu safari hiyo ya hatari ya kuvuka Mediterenia na kuingia Ulaya.

Castaner amesema mazungumzo yanatarajiwa kuendelea baada ya mkutano kati ya mawaziri wa mambo ya nje na mambo ya ndani wa Umoja wa Ulaya mjini Paris, Jumatatu.

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com