1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mawaziri wa mambo ya kigeni wajadili hali nchini Georgia.

13 Agosti 2008

Mawaziri wa mambo ya kigeni wa umoja wa Ulaya waunga mkono kulipeleka jeshi la kulinda amani Georgia.

https://p.dw.com/p/Ewia
Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na suala la Georgia .Picha: AP

Mawaziri wa mambo ya kigeni wa umoja wa Ulaya wameeleza kuunga kwao mkono leo kupelekwa kwa jeshi la kulinda amani la umoja huo ili kulinda makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa kwa upatanishi wa Ufaransa kati ya Urusi na Georgia katika jimbo linalotaka kujitenga la South Ossetia.

Umoja wa Ulaya uko tayari kushiriki, ikiwa ni pamoja na kutuma jeshi, kusaidia juhudi za umoja wa mataifa na nchi za OSCE, amesema waziri wa maendeleo wa Ireland Peter Power baada ya mkutano wa dharura wa umoja wa Ulaya mjini Brussels.

Power amesema maelezo juu ya kutumwa jeshi hilo la kulinda amani yatajadiliwa katika mkutano wa mawaziri wa mambo ya kigeni wa umoja wa Ulaya mwezi Septemba.

Mapema leo Jumatano, waziri wa mambo ya kigeni wa Ufaransa Bernard Kouchner, ambaye alifuatana na rais Nicolas Sarkozy katika ujumbe wake wa upatanishi katika makubaliano ya amani mjini Moscow jana Jumanne, amesema kuwa anaimani Urusi itakubali kuwepo majeshi ya Ulaya.

Makubaliano ya kupeleka jeshi la kulinda amani yalifikiwa katika mkutano wa mawaziri wa mataifa 27 wanachama wa umoja wa Ulaya wakati hali ya utulivu iliporejea nchini Georgia baada ya vita vya siku sita kati ya Georgia na Urusi , vita ambavyo vilileta wasi wasi mkubwa katika mataifa ya magharibi. Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier amesema kuwa ni muhimu kuliangalia kwa uangalifu suala hili.

Mbali na taarifa za watu walioshuhudia kinyume na hali halisi katika eneo hilo , waziri wa mambo ya kigeni wa Georgia Ekaterine Tkeshelashvili amesema alipowasili mjini Brussels kuwa Urusi bado inashambulia mji wa Gori nchini Georgia , nje ya jimbo la South Ossetia.

Ni lazima waangalizi wa amani wa umoja wa Ulaya wawepo.

Ulaya ni lazima ijihusishe na Ulaya ni lazima isitishe hali hii isiendelee, amewaambia waandishi wa habari.

Lakini waziri wa mambo ya kigeni wa Sweden Carl Bildt, ambaye ametembelea Georgia kama mjumbe wa baraza la Ulaya , ametia shaka iwapo Urusi itaruhusu walinzi wa amani wa Ulaya katika maeneo ambayo wamekuwa wakiyashikilia ama wameyakamata.

Marekani wakati huo huo imeomba mkutano wa mawaziri wa mambo ya kigeni wa NATO kuhusiana na hali katika jimbo la Georgia, ambao unaweza kufanyika huenda mapema wiki ijayo, amesema msemaji wa NATO.

Mzozo huo unaweka wazi mgawanyiko katika umoja wa Ulaya kuhusiana na jinsi ya kushughulika na Urusi ambayo imekuwa na mahusiano ya mivutano tangu kupanuliwa mipaka ya umoja wa Ulaya na kuziingiza nchi zilizokuwa katika kambi ya kikomunist mwaka 2004.