1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mawaziri wa fedha wa nchi saba tajiri wakutana Japan.

Zainab Aziz
11 Mei 2023

Mawaziri wa fedha wa kundi la G-7 wanakutana katika mji wa bandari wa Niigata nchini Japan. Watajadili njia za kukabiliana na changamoto za kiuchumi duniani pamoja na vita vya nchini Ukraine.

https://p.dw.com/p/4RCgw
Deutschland Münster | Flaggen G7
Picha: Wolfgang Rattay/AFP/Getty Images

Mawaziri hao wa fedha wa kundi la mataifa saba tajiri wanakutana katika mji wa bandari wa Niigata kabla ya mkutano huo wa G-7 kufanyika mjini Hiroshima. Viongozi hao kwenye mkutano wao watajadili njia za kukabiliana na changamoto za kiuchumi duniani pamoja na vita vya nchini Ukraine.

Waziri wa Fedha wa Marekani Janet Yellen.
Waziri wa Fedha wa Marekani Janet Yellen.Picha: Jose Luis Magana/AP Photo/picture alliance

Mkutano huo unafanyika wakati ambapo taifa kubwa la Marekani linakabiliwa na mzozo kuhusu kikomo cha kuongeza deni la nchi hiyo na wakati huo huo kuna uwezekano wa Marekani kushindwa kulipa deli lake jambo ambalo linaweza kusababisha mtafaruku katika uchumi wa dunia nzima.

Gavana wa benki kuu ya Japan, Kazuo Ueda, amesema ikiwa Marekani itashindwa kulipa deni lake, hatua hiyo itasababisha tatizo kubwa, lakini amesema anaamini serikali ya Marekani itafanya kila iwezalo kuepuka hali kama hiyo kutokea.

Soma:Mkutano wa viongozi wa G7 na Umuhimu wake duniani

Waziri wa fedha wa Marekani Janet Yellen amesema moja ya vipaumbele vyake katika mkutano huo wa Niigata, ni kusisitiza juu ya umuhimu wa kutatua mkwamo wa deni la Taifa katika nchi ya Marekani ambayo ni taifa lenye uchumi mkubwa zaidi duniani. Amesema kukosa kulipa deni hilo ni jambo lisilofikirika. Waziri huyo wa fedha wa Marekani Janet Yellen amelitaka bunge kuongeza kikomo cha deni la taifa la dola trilioni 31.4 ili kuepusha hali ya kushindwa kulipa deni ambayo ikitokea itasababisha kuzorota kwa uchumi wa dunia.

Waziri wa Fedha wa Ujerumani Christian Lindner.
Waziri wa Fedha wa Ujerumani Christian Lindner.Picha: Kay Nietfeld/dpa/picture alliance

Uchumi wa nchi nyingine wanachama wa kundi la G-7 pia unakabiliwa kuongezeka kwa bei za bidhaa na hivyo kuzilazimu benki kuu za nchi hizo kuongeza viwango vya riba vilivyokuwa vimepungua kabla ya kuzuka janga la corona.

Mawaziri wa fedha wa G-7 walikutana mwezi uliopita, mjini Washington, Marekani wakati wa mkutano wa kila mwaka wa Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa, IMF. Walisisitiza kujitolea kwao kusaidia uchumi wa nchi zilizoathirika kutokana na vita vya Ukraine, kuzisaidia katika kukabiliana na mzigo wa madeni, kuimarisha mifumo ya afya kimataifa na kusaidia kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Mataifa saba Tajiri yanaounda kundi la G-7 ni pamoja na  Canada, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Japan, Uingereza na Marekani. Waalikwa kwenye mkunao huo wa Japan ni pamoja na Umoja wa Ulaya, IMF, Benki ya Dunia, mawaziri wa fedha wa Brazil, Comoro, India, Indonesia, Korea Kusini na Singapore.

Vyanzo:AP/RTRE