1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matayrisho ya kuapishwa Barack Obama kuwa Rais wa Marekani

Miraji Othman13 Januari 2009

Jumanne ijayo Barack Obama ataapishwa kuwa rais wa Marekani

https://p.dw.com/p/GX9K
Rais-mteule Barack Obama (kushoto) akimtembelea Rais George Bush katika Ikulu, mjini WashingtonPicha: AP


Jumanne ijayo, Januari 20, tukio la kihistoria litajiri katika mji mkuu wa Marekani, Washington. Barack Obama ataapishwa kuwa rais wa kwanza wa Kimarekani mwenye asili ya Kiafrika. Jambo hilo litashuhudiwa na mamilioni ya watu watakaotokea sehemu mbali mbali za dunia, na ndani kwenyewe Marekani ambapo inakisiwa mabasi ya kukodi alfu kumi yatafika katika mji huo. Kuapishwa kwa rais huyo wa 44 kutaanzisha enzi mpya, ambayo Barack Obama mwenyewe amahidi kwamba itakuwa ya mabadiliko kwa sura ya Marekani ndani nchini na nje pia. Wenyewe Wamarekani wanataraji Barack Obama atasafiri na nyota nzuri katika utawala wake, angalau kuyatanzuwa matatizo makubwa ambayo nchi yao inakabiliana nayo, licha ya vita huko Iraq na Afghanistan.

Juu ya umuhimu wa siku hiyo, msikilize Profesa Julius Nyangoro wa Chuo Kikuu cha Carolina ya Kaskazini huko Marekani...

Inakadiriwa karibu watu milioni mbili watamiminika katika viwanja vya Ikulu huko Washington katika siku hiyo ambayo watabiri wa hali ya hewa wameshasema kutakuweko baridi na pia mvuwa itanyesha. Pale John F. Kennedy alipoapishwa mwaka 1961, kulikuweko msongamano mkubwa katika barabara za mji wa Washington kwa vile ilianguka theluji nyingi. Lakini tuombe tu isiwe kama ilivotokea Machi mwaka 1841 pale William Harrison alipoapishwa, huku akiwa hajavaa koti, hali ya hewa ikiwa ni baridi kali, na akatoa hotuba kwa saa moja na dakika arbaini. Hiyo ilikuwa hotuba ndefu kabisa kuwahi kutolewa na rais aliyeapishwa. Siku chache baadae, William Harrison aliugua homa ya mapavu na kufa mwezi uliofuata.

Nini ambacho kitakuwemo katika hotuba ya Barck Obama, anakisia hivi Profesa Julius Nyangoro...

Kutokana na watu wengi watakaofika katika sherehe hizo, maafisa wa usalama sasa wanakuna vichwa, hasa kutafuta njia za kuhakikisha kwamba rais mteule atakuwa salama pamoja na familia yake. Inakisiwa idadi ya watu watakaofika itapindukia wale milioni 1.2 waliowasili mwaka 1965 wakati alipoapishwa Lyndon Johnson kuchukuwa nafasi ya John F. Kennedy.

Mara hii eneo la kilomita tisa za mraba kuzunguka Ikulu litawekwa chini ya ulinzi mkali, huku kukiwekwa vizuizi kwa matumizi hata ya anga juu ya jengo la Ikulu na njia za maji zinazoelekea eneo hilo.

Barack Obama na makamo wa rais Joe Biden watakula kiapo adhuhuri ya siku hiyo ya jumanne. Obama atakula kiapo huku akishikilia biblia ambayo iliwahi kuwa ya yule shujaa anayemhusudu, Rais Abraham Lincoln aliyeuliwa. Bibilia hiyo ya kihistoria itatumiwa kwa mara ya kwanza tangu alipotawazwa Abraham Lincoln mwaka 1861, rais wa 16 ambaye alikomesha utumwa nchini Marekani.

Katika viwanja vya Ikulu kutawekwa maskrini makubwa kumi na vikuza sauti mia moja kwa ajili ya watu watakaofika na watu hao wataangaliwa na maafisa wa polisi 8,000, wakiwa alfu moja zaidi kuliko wale waliotumiwa wakati wa kutawazwa George Bush mwaka 2005, na pia wanajeshi 11,500.

Baada ya Barack Obama kutawazwa kama rais,gwaride la kijeshi litapita katika barabara ya Pennsylvannia hadi Ikulu. Japokuwa timu ya Obama imesema sherehe hizo za kutawazwa ni kwa Wamarekani wote, kuwekwa usalama katika tokeo hilo kutagharimu dola milioni 75.

Tangu sasa mahoteli katika mji wa Washington na katika mikoa ya karibu ya Virginia na Maryland imejaa na kuna msongamano mabarabarani.

Idadi ya waandishi wa habari kutoka nchi mbali mbali waliojisajili kuripoti juu ya tokeo hilo mara imezidi marudufu, na bila ya shaka hawatavunjika moyo, watashuhudia ufasaha wake wa kuhutubia watu.

Hata hivyo, baada ya sherehe hizo Barack Obama atakabiliana na mrundo wa mambo ya kuyashughulikia.

Kama Barack Obama ataweza kuyatanzuwa matatizo hayo, tena Profesa Julius Nyangoro wa Chuo Kikuu cha Carolina ya Kaskazini...

George Bush, akiwa Ikulu kwa miaka minane, alikuwa na kitu kingine muhimu katika familia yake, naye ni mbwa wake aliyemuongoza kila pahala. Barack Obama hajachaguwa bado atakuwa na mbwa gani. Profesa Nyangoro anaelezea umuhimu wa mbwa katika jamii ya Kimarekani...

Katika mazungumzo yake na waandishi wa habari kabla ya kuihama Ikulu, Rais Bush alimtakia heri Rais-mteule Obama, na hajachelea kusema miaka minane ya urais wake haujawa wakati rahisi kwake, wala kwa nchi yake ya Marekani. Tumuombee dua Obama- kila la heri.