1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maroketi zaidi yaelekezwa Kabul

Lilian Mtono
30 Agosti 2021

Kundi la wanamgambo wa Taliban limesema shambulizi la ndege isiyo na rubani ya Marekani lililomlenga mtuhumiwa wa shambulizi la kujitoa muhanga mjini Kabul jana Jumapili limesababisha vifo na majeruhi ya raia.

https://p.dw.com/p/3zfx7
Afghanistan PK der Taliban
Picha: Rahmat Gul/dpa/AP/picture alliance

Kundi hilo la waamgambo la Taliban pia limeilaumu Marekani kwa kushindwa kuwaarifu mapema kabla ya kuanzisha shambulizi hilo. 

Msemaji wa kundi hilo la Taliban Zabihullah Mujahid amekiambia kituo cha televisheni cha serikali cha China, CGNT hii leo kwamba watu kumi wameuawa kwenye shambulizi hilo la ndege isiyo na rubani, na kulitaja shambulizi hilo la Marekani kwenye ardhi ya Afghanistan kuwa lisilokubalika kisheria.

Amesema kama kungekuwa na kitisho kikubwa, Marekani ilitakiwa kukiripoti kwao badala ya kuanzisha mashambulizi hayo.

Soma Zaidi:Marekani yaonya kuhusu kitisho cha kuaminika kwenye uwanja wa ndege wa Kabul 

Wizara ya Ulinzi ya Marekani, Pentagon imesema mshambuliaji huyo wa kujitoa muhanga alikuwa kwenye gari akijiandaa kushambulia uwanja wa ndege wa Kabul, wakati jeshi lake lilikuwa katika hatua za mwisho za kuondoka. Pentagon imesema alikuwa anajiandaa kushambulia kwa niaba ya kundi la wanamgambo la ISIS-K lenye mahusiano na Dola la Kiislamu na lenye uadui na Taliban na mataifa ya Magharibi.

Mapema leo, afisa mmoja wa Marekani amesema, mfumo wa ulinzi dhidi ya makombora wa Marekani umefanikiwa kuzuia karibu maroketi matano yaliyorushwa kuelekea uwanja wa ndege wa Kabul. Vyombo vya habari vya Afghanistan vimesema roketi ilifyatuliwa kutokea nyuma ya gari. Shirika la habari la Pajhwok limesema maroketi kadhaa yalielekezwa kwenye maeneo mbalimbali ya Kabul.

Hakukuwa na ripoti za majeruhi ama vifo kwa upande wa WaMarekani.

Soma Zaidi: Kabul: Vikosi vya Marekani vyawekwa kwenye tahadhari kubwa

Afghanistan Kabul | Zerstörtes Auto nach Rekatenangriff
Moja ya magari yaliyoharibiwa baada ya mashambulizi ya roketi kuelekea mji wa KabulPicha: Wakil Kohsar/AFP/Getty Images

Huku hayo yakiendelea, Umoja wa Ulaya umesema serikali zake zinatakiwa kuongeza shinikizo la mpango wa kikosi cha dharura cha Ulaya kujiandaa vyema kwa ajili ya mizozo ya siku za usoni kama huu wa sasa wa Afghanistan.

Ulaya yataka shinikizo zaidi kuhusu kikosi cha kukabiliana na dharura.

Mkuu wa sera ya kigeni wa Ulaya Josep Borrell amesema kwenye mahojiano hii leo na gazeti la Italia la 11 Corriere della Sera kwamba hatua ya ghafla ya Marekani ya kupeleka wanajeshi wakati usalama ukiwa tete nchini humo imeonyesha kunahitajika shinikizo zaidi za kuwa na sera ya pamoja ya ulinzi.

Katika hatua nyingine waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Heiko Maas amesema wataendelea kuwasaidia watu wanaotaka kuondoka Afghanistan na ambao tayari wamekimbia. Maas amesema wakati anaanza ziara ya siku nne katika nchi tano tofauti inayoanzia leo, Uturuki. Ziara hiyo inaangazia juhudi za kuwasaidia WaAfghanistan.

Uzbekistan nayo imekubali kuwafungulia mipaka watu walioko kwenye orodha iliyoandaliwa na Ujerumani inayoonyesha wanakabiliwa na kitisho cha Taliban, hii ikiwa ni kulingana na Maas.

Alisema "Tumejadiliana namna ya kuwasaidia wale wanaotuhusu, ambao ni kundi dogo tu kuwa wanaweza kuletwa Ujerumani wakati wanapokwenda Uzbekistan."

Lakini, Kinyume cha hayo, Uturuki imesema haiko tayari kupokea wimbi jipya la wakimbizi kutoka Afghanistan.

Tukirejea tena Ulaya, mawaziri wa mambo ya ndani wa umoja huo, wanatarajiwa kuelezea nia yao ya kuzuia wahamiaji zaidi  kutokea Afghanistan, hii ikiwa ni kulingana na rasimu ya taarifa iliyoonekana na shirika la Reuters. Mawaziri hao wanakutana kesho kwa kikao cha dharura mjini Brussels kujadiliana juu ya mzozo nchini humo.

Soma Zaidi: 

Mashirika: RTRE/DW