1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yaonya kuhusu kitisho cha kuaminika Kabul

Grace Kabogo
29 Agosti 2021

Marekani imeonya kuwa kuna kitisho cha kuaminika karibu na uwanja wa ndege wa Kabul na imewataka raia wake kuondoka kwenye eneo hilo mara moja.

https://p.dw.com/p/3zcyn
Afghanistan| ein US-Militärflugzeug startet am Flughafen in Kabul
Picha: Wali Sabawoon/AP/picture alliance

Taarifa hiyo imetolewa mapema Jumapili asubuhi, siku kadhaa baada ya kutokea shambulizi baya la kujitoa muhanga kwenye uwanja wa ndege wa Kabul na kuwaua takriban raia 169 na wanajeshi 13 wa Marekani. Umati mkubwa wa Waafghani unakwenda kwenye uwanja huo wa ndege kuukimbia utawala wa Taliban.

Taliban: Watuhumiwa kadhaa wakamatwa

Kundi la wanamgambo linalofungamana na lile linalojiita Dola la Kiislamu, IS-K limedai kuhusika na shambulizi hilo. Taliban imesema imewakamata washukiwa kadhaa waliohusika katika shambulizi hilo.

Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imewataka Wamarekani kuepuka kwenda kwenye uwanja wa ndege wa Kabul, pamoja na kutumia milango yote mikuu ya kuingilia katika uwanja huo.

Afghanistan, Kabul | US-Soldaten am Flughafen
Wanajeshi wa Marekani na Italia katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Hamid Karzai mjini KabulPicha: Staff Sgt. Victor Mancilla/USMC/UPI Photo/Newscom/picture alliance

Wizara hiyo imesema maeneo yanayopaswa kuepukwa ni pamoja na lango kuu la upande wa Kusini, wizara mpya ya mambo ya ndani na lango karibu na kituo cha mafuta cha Panjshir, kilichoko upande wa kaskazini maghabiri mwa uwanja huo wa ndege.
Tahadhari kadhaa kuhusu kitisho cha kutokea shambulizi la kigaidi, imekwamisha juhudi za kuwaondoa watu zinazofanywa na majeshi ya Marekani, ambayo yamelazimika kushirikiana kwa karibu kiusalama na Taliban ili kuzuia kutokea tena kwa shambulizi jingine kama la siku ya Alhamisi, kwenye moja ya lango kuu la kuingilia kwenye uwanja wa ndege wa Kabul.

Afisa wa masuala ya usalama wa mataifa ya Magharibi katika uwanja wa ndege wa Kabul, amesema kuna zaidi ya raia 1,000 waliobakia katika uwanja huo wakisubiri kuondolewa kwa usafiri wa ndege, wakati Marekani ikiwa kwenye awamu za mwisho za kuwaondoa watu. Kwa mujibu wa afisa huyo, umati wa watu uko kwenye milango mikubwa ya kuingilia ndani ya uwanja huo.

Biden aonya kuhusu shambulizi jingine

Mapema Jumamosi, Rais wa Marekani Joe Biden alionya kwamba makamanda wa kijeshi wamesema kuna uwezakano wa kutokea shambulizi jingine katika muda wa saa 24 hadi 36 zijazo, wakisema hali hiyo ni hatari sana.

Uingereza imesema majeshi yake ya mwisho yameondoka Kabul. Uingereza, Ufaransa na Uhispania zimetangaza kumaliza shughuli ya kuwaondoa watu mjini Kabul. Uingereza na Ufaransa zimesema zitatoa wito wa kuwepo kwa eneo salama mjini Kabul wakati wa mkutano wa dharura wa Umoja wa Mataifa utakaofanyika siku ya Jumatatu.

Soma zaidi: Juhudi za kimataifa kuwahamisha watu Aghanistan zashika kasi

Nazo Ujerumani, Uingereza na Uholanzi zimekubaliana kwamba shughuli ya kuwaondoa watu bado inabakia kuwa kipaumbele. Ofisi ya Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel imesema kiongozi huyo alijadiliana na mawaziri wakuu wa Uholanzi na Uingereza kuhusu hali ya Afghanistan. Viongozi hao watatu wamezungumzia pia juu ya uwezekano wa kuwepo mchakato wa kisiasa na kidiplomasia.

Wakati huo huo, vikosi vya kundi la Taliban vimeufunga uwanja wa ndege wa Kabul kwa raia wengi wa Afghanistan wanaotarajia kuondolewa wakati ambapo Marekani na washirika wake wakimalizia operesheni ya kuwaondoa watu kwa kutumia ndege na kukamilisha uwepo wa majeshi hayo kwa muda wa miongo miwili nchini humo.

Aidha, Taliban ambao ni watawala wapya wa Afghanistan pamoja na vikosi vya Marekani vinavyoondoka wanatarajia kuwepo kwa makabidhiano mazuri na ya haraka ya uwanja wa ndege wa Kabul.

Mapema Jumapili, afisa wa Taliban ambaye hakutaka kutajwa jina aliliambia shirika la habari la Reuters kuwa wanasubiri ishara kutoka kwa Wamarekani ili kuchukua udhibiti kamili wa uwanja huo wa ndege. Amesema Taliban ina timu ya wataalamu wa kiufundi na wahandisi wenye ujuzi ambao wako tayari kuchukua udhibiti wa uwanja wa ndege wa Kabul.

Afghanistan PK der Taliban
Msemaji wa Taliban, Zabihullah MujahidPicha: Rahmat Gul/dpa/AP/picture alliance

Ama kwa upande mwingine kundi la Taliban limelaani vikali shambulizi la Marekani la ndege isiyokuwa na rubani lililotokea siku ya Jumamosi katika jimbo la mashariki la Nangarhar linalopakana na Pakistan.

Marekani yadai kuwaua wawili

Wizara ya Ulinzi wa Marekani imedai kuwa shambulizi hilo limewaua maafisa wawili wa ngazi ya juu wa IS-K wanaodaiwa kupanga shambulizi la kwenye uwanja wa ndege wa Kabul.

Msemaji wa Taliban Zabihullah Mujahid amesema wanajeshi wa Marekani walipaswa kuwaarifu kabla ya kufanya shambulizi hilo la anga. Amesema ni dhahiri shambulizi hilo limetokea katika eneo la Afghanistan, ambapo wanawake wawili na mtoto mmoja walijeruhiwa.

Huku hayo yakijiri, Mujahid amesema kundi la Taliban pia linajiandaa kutangaza baraza lake jipya la mawaziri katika siku chache zijazo.

(AP, AFP, Rueters)