1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kabul: Vikosi vya Marekani vyawekwa kwenye tahadhari kubwa

Zainab Aziz Mhariri: Sudi Mnette
28 Agosti 2021

Ubalozi wa Marekani nchini Afghanistan mapema Jumamosi umetoa tahadhari mpya ya usalama kwa raia wake kutokufika katika uwanja wa ndege wa Kabul. Muda wa mwisho wa kuwahamisha watu ni Agoszi 31.

https://p.dw.com/p/3zc2R
Afghanistan | Evakuierung Flughafen Kabul
Picha: Staff Sgt. Victor Mancilla/U.S. Marine Corps/AP Photo/picture alliance

Raia wote wa Marekani walitakiwa waondoke kwenye lango la Abbey kwenye uwanja huo wa ndege, na pia upande wa Mashariki na Kaskazini mwa uwanja wa Hamid Karzai mjini Kabul. Wizara ya Mambo ya Ndani ya Marekani pia ilisisitiza ushauri wake kwa raia wake wa kuepuka kuufikia uwanja huo wa ndege.

Taliban wamepeleka vikosi vya ziada karibu na uwanja huo wa ndege wa Kabul kuzuia umati mkubwa wa watu wanaokusanyika katika eneo hilo tangu wiki mbili zilizopita kwa lengo la kutaka kundoka Afghanistan.

Taliban waweka vizuizi kwenye maeneo ya uwanja wa ndege mjini Kabul
Taliban waweka vizuizi kwenye maeneo ya uwanja wa ndege mjini KabulPicha: REUTERS

Hatua hiyo imechukuliwa siku mbili baada ya kutokea shambulio kubwa la kujitoa muhanga mjini Kabul wakati ambapo Marekani inaendelea na shughuli za kuwaondoa raia wake na wale wa Afghqnistan kutoka nchini humo kabla ya tarehe ya mwisho ambayo ni Agosti 31.

Mataifa mengi ya Magharibi tayari yamekamilisha zoezi la kuwahamisha watu kutoka Afghanistan kabla ya tarehe hiyo ya mwisho ambayo ni siku ya Jumanne siku inayotarajiwa kuwa Marekani itakuwa imeviondoa vikosi vyake vyote kutoka nchini humo.

Shambulio la kujitoa mhanga lilifanywa mnamo siku ya Alhamisi na mpiganaji wa kundi la kigaidi linalojiita Dola la Kiisilamu IS. Miongoni mwa watu waliouawa ni Waafghanistan 169 na wanajeshi 13 wa Marekani. Pana wasiwasi mkubwa kwamba kundi hilo ambalo lina itikadi kali zaidi kuliko la Taliban huenda likafanya mashambulizi mengine.

Rais wa Marekani Joe Biden
Rais wa Marekani Joe BidenPicha: Jonathan Ernst/REUTERS

Jeshi la Marekani limemuua mtu anayedaiwa kupanga shambulizi hilo la kwenye uwanja wa ndege wa Kabul kwa kutumia ndege isiyokuwa na rubani baada ya Rais wa Marekani Joe Biden kuahidi kwamba nchi yake ingelipiza kisasi.

Zaidi ya watu 110,000 wameshahamishwa kupitia uwanja wa ndege wa Kabul tanguTaliban ilipochukua udhibiti wa nchi ya Afghanistan, kulingana na Marekani, ikiwa ni pamoja na karibu watu 6,800 waliohamishwa katika muda wa saa 24 zilizopita. Maelfu zaidi wanajitahidi kuipata nafasi ya kuondoka lakini huenda wasifanikiwe kufikia hiyo Jumanne.

Raia wa Afghanistan
Raia wa AfghanistanPicha: Hoshang Hashimi/AFP

Wakati huo huo shirika la chakula la Umoja wa Mataifa limetoa tahadhari kuwa ukame unazidi kutishia maisha ya watu zaidi ya milioni 7. Shirika hilo la Chakula na Kilimo FAO limesema Waafghanistan pia wanateseka kutokana na janga la maambukizi ya virusi vya corona na wengi  wao hawana makazi kutokana na mapigano ya hivi karibuni.

Mapema mwezi huu, Shirika hilo la Mpango wa Chakula Ulimwenguni la Umoja wa Mataifa lilikadiria kuwa takriban mtu mmoja kati ya watu watatu nchini Afghanistan yenye watu wapatao milioni 14 anahitaji msaada wa chakula haraka.

Vyanzo:/DPA/AP