Marekani yaimarisha ukaguzi wa safari za anga kwa baadhi ya nchi. | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 04.01.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Timu Yetu

Marekani yaimarisha ukaguzi wa safari za anga kwa baadhi ya nchi.

Marekani imetangaza utaratibu mpya ambapo abiria wanaotumia usafiri wa anga kutoka baadhi ya nchi watakabiliwa na ukaguzi wa mwili nzima, kabla ya kupanda ndege chini ya taratibu mpya zinazolenga kuimarisha ukaguzi.

default

Mmoja wa maafisa wa Uwanja wa Ndege nchini Marekani akiwakagua abiria. Marekani imeimarisha zaidi ukaguzi kwa abiria hususan katika nchi 14 zinadaiwa kuwasaidia magaidi.

Utaratibu huo ambao umeanza kutumika leo Jumatatu, unafuatia jaribio la kulipua ndege ya Marekani iliyokuwa ikijiandaa kutua katika uwanja wa ndege wa Detroit, ikitokea Amsterdam, wakati wa sikukuu ya Krismas, jaribio ambalo lilifanywa na raia wa Nigeria Umar Farouk Abdulmuttalab, ambaye Marekani inaamini kuwa amepewa mafunzo na Al Qaeda nchini Yemen.

Umar Farouk Abdulmutallab

Raia wa Nigeria Umar Farouk Abdulmutallab aliyetaka kuilipua ndege ya Marekani katika uwanja wa ndege wa Detroit na kusababisha mtafaruku ulioko sasa wa kuimarishwa kwa ukaguzi.

Kwa mujibu wa Afisa mmoja katika serikali ya Rais Barack Obama, ambaye hakutaka kutajwa jina lake, abiria wanaosafiri kutoka ama kupitia katika nchi ambazo zimeorodheshwa kama mataifa yanayofadhili au kusaidia ugaidi, ambayo yametajwa kuwa ni Cuba, Iran, Sudan na Syria, watakaguliwa kupitia utaratibu huo.

Nchi nyingine ambazo zimekumbwa na utaratibu huo mpya wa ukaguzi ni pamoja na Afghanistan, Algeria, Iraq, Lebanon, Libya, Nigeria, Pakistan, Saud Arabia, Somalia na Yemen.

Aidha afisa huyo wa Marekani amesema wasafiri hao watakaguliwa mwili mzima, kukagua mizigo na kuchunguza vifaa vya milipuko.

Idara inayohusika na usalama wa Usafiri wa anga nchini humo imetangaza kuziimarisha taratibu za uchunguzi na kuongeza kwamba wasafiri watachunguzwa mwili mzima.

Lakini hata hivyo tangazo hilo la Marekani la hatua mpya za usalama limekuja wakati chama cha upinzani nchini humo cha Republican kikiendelea kuikosoa serikali na wakosoaji wengine kwamba wanadiplomasia wa nchi hiyo na maafisa usalama walishindwa kuzuia tukio hilo la Desemba 25, licha ya kuwa na ushahidi kuhusiana na kijana huyo wa Kinigeria.

Marekani na Uingereza zafunga balozi zake Yemen: Wakati Yemen ikitajwa pia katika orodha ya nchi zilizokumbwa na utaratibu huo mpya na nchi ambayo inaripotiwa kuwa ndiko alikopata mafunzo raia wa Nigeria aliyefanya jaribio la kulipua ndege wakati wa Krismas, ambayo yalitolewa na Mtandao wa Al Qaeda, Marekani na Uingereza zimefunga balozi zake katika mji mkuu wa nchi hiyo Sana'a, kutokana na sababu za usalama wa kushambuliwa na wapiganaji wa Al Qaeda baada ya kushindwa kwa kwa jaribio hilo la kulipua ndege ya Marekani.

Marekani yasema Al Qaeda wapanga kufanya mashambulio Sanaa: Msaidizi wa Rais Barack Obama katika masuala ya kukabiliana na ugaidi John Brennan Marekani ina vielelezo kwamba Al Qaeda wamepanga kufanya mashambulizi katika mji huo wa Sana'a.

John Brennan Bildergalerie Kabinett

Msaidizi wa Rais Obama katika masuala ya kukabiliana na ugaidi, John Brennan asema kuna ushahidi kwamba Al Qaeda wamepanga kuishambulia Sanaa.

Naye Waziri Mkuu wa Uingereza Gordon Brown amesema Uingereza na Marekani zinaimarisha juhudi zake za kukabiliana na ugaidi nchini Yemen, nchi ambayo imekuwa kituo cha magaidi wenye msimamo mkali.

Kwa upande wake, Yemen imeimarisha ulinzi katika pwani yake kuwazuia wapiganaji wa kiislamu kujipenyeza na kuingia nchini humo kutokea Somalia.

Awali wapiganaji wa Somalia walisema wako tayari kutuma nguvu zaidi kuwasaidia Al Qaeda nchini humo.

Mwandishi: Halima Nyanza(Reuters)

Mhariri:mwadzaya,thelma

 • Tarehe 04.01.2010
 • Mwandishi Halima Nyanza
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/LJU6
 • Tarehe 04.01.2010
 • Mwandishi Halima Nyanza
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/LJU6
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com