1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani kuongeza wanajeshi 500 zaidi Ujerumani

Iddi Ssessanga
13 Aprili 2021

Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin ametangaza siku ya Jumanne, mpango wa kupanua uwepo wa jeshi la Marekani nchini Ujerumani kwa kuongeza wanajeshi 500, katika juhudi za kuimarisha uhusiano na nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/3rwrs
Berlin Besuch Verteidigungsminister USA Lloyd Austin  mit Annegret Kramp-Karrenbauer
Picha: KAY NIETFELD/REUTERS

Hatua hiyo inaashiria wazi kujitenga kwa utawala wa Joe Biden na msimamo wa uhasama zaidi kuelekea Ujerumani, uliochukuliwa na mtangulizi wake Donald Trump, aliekuwa amechukuwa hatua ya kupunguza uwepo wa wanajeshi wa Marekani nchini humo, ambao ni msingi wa usalama wa jumuiya kujihami NATO tangu mwanzo wa Vita Baridi.

Soma pia: Ujerumani haitishwi na Marekani kuondoa wanajeshi

Austin ametoa tangazo hilo siku ya Jumanne, baada ya mazungumzo na waziri wa ulinzi wa Ujerumani Annegret Kramp- Karrenbauer, katika ziara yake ya kwanza ya Ulaya tangu alipoteuliwa kuiongoza wizara ya ulinzi Pentagon mnamo mwezi Januari.

Waziri Kramp-Karrenbauer amekaribisha tangazo hilo alilolitaja kuwa ishara thabiti ya uhusiano imara kati ya Marekani na Ujerumani.

Berlin Besuch Verteidigungsminister USA Lloyd Austin  mit Annegret Kramp-Karrenbauer
Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin na mwenzake wa Ujerumani Annegret Kramp-Karrenbauer wakiweka shada la maua katika jengo la Bendlerblock katika wizara ya ulinzi ya Ujerumani mjini Berlin, Aprili 13, 2021.Picha: KAY NIETFELD/REUTERS

Mawaziri hao pia wamezungumzia uamuzi unaosubiriwa wa rais Joe Biden kuhusu juu ya ama kuwaondoa kikamilifu wanajeshi wa Marekani nchini Afghanistanikifikapo Mei Mosi, ambayo ndiyo tarehe ya mwisho utawala wa Trump ulikubaliana na kundi la wapiganaji wa Taliban.

Ujerumani ni sehemu muhimu wa muungano unaoongozwa na Marekani nchini Afghanistan.

Austin amesema kwenye mkutano wa pamoja na Kramp-Karrenbauer kwamba wanajeshi 500 wa ziada wa Marekani watawekwa kwa kudumu katika eneo la Ujerumani la Wiesbaden kuanzia majira ya mapukutiko mwaka huu.

"Wanajeshi hawa wataimarisha uzuwiaji na ulinzi barani Ulaya, na wataongezea uwezo wetu tulio nao kwa sasa wa kuzuwia mzozo na ikihitajika, kupigana na kushinda," alisema waziri Austin.

Nord Steam 2 Bauarbeiten
Mradi wa ujenzi wa bomba la gesi la Nord Stream 2 kutoka Urusi kwenda Ujerumani umekuwa chanzo cha mvutano kati ya Marekani na Ujerumani.Picha: Walter Graupner/Nord Stream 2

Adokeza kutotekeleza mpango wa Trump

Mwaka uliyopita, rais Donald Trump aliamuru kuondolewa kwa wanajeshi 12,000 kutoka Ujerumani kama hatua ya kuiadhibu nchi hiyo kwa kile alichokichukulia kuwa kukataa kwa Ujerumani kuongeza matumizi yake ya kijeshi. Austin alisitisha hatua hiyo mara ya kuingia ofisini.

Tangazo lake la leo ndiyo ishara ya kwanza ya wazi kwamba huenda asitekeleze aumuzi wa Trump, ambao ulihusisha pia kuhamishwa kwa makao makuu ya vikosi vya Marekani barani Ulaya kutoka Ujerumani kwenda Ubelgiji.

Waziri Austin pia amezungumzia Bomba la gesi la Nord Stream ambalo lilikuwa sehemu ya mzozo katika ya Ujerumani na Marekani, akisema licha ya upinzani wa wazi wa Marekani dhidi ya mradi huo wa Urusi na Ujerumani, Marekani haitaruhusu suala hilo kuathiri uhusiano wa muda mfefu na wa kimkakati kati yake na Ujerumani.

Chanzo: Mashirika