1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano yanapamba moto Gaza na kuenea pia Ukingo wa Magharibi

Oummilkheir13 Juni 2007

Hamas wawapa muda Fatah waweke silaha chini kabla ya saa moja usiku hii leo

https://p.dw.com/p/CB3d
Picha: AP

Kitisho cha kuzuka vita vya wenyewe kwa wenyewe kinazidi kukua baada ya tawi la kijeshi la Hamas kuwapa muda watumishi wa idara ya usalama wanaomuunga mkono rais Mahmoud Abbas waweke chini silaha huko Gaza kabla ya magharibi ya leo.Mapigano yameripotiwa pia Ukingo wa magharibi.

Ujerumani , mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa ulaya imeyatolea mwito makundi yote yanayohusika na ugonvi wa Palastina wajiepushe na balaa la kuzuka vita vya wenyewe kwa wenyewe.Umoja wa Ulaya umelaani mashambulio ya wanamgambo dhidi ya vikosi vya usalama na kuelezea uungaji mkono wake kwa rais Mahmoud Abbas.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinemeier amezungumza kwa simu na kiongozi wa utawala wa ndani wa Palastina na kuelezea uungaji mkono wa nchi yake na Umoja wa Ulaya kwa juhudi zinazosimamiwa na Misri na mataifa mengine ya kiarabu katika kuutuliza mzozo huo.Msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje ya Ujerumani mjini Berlin Martin Jäger amesema waziri Steinemeier anapanga pia kuzungumza kwa simu pamoja na washirika wa Umoja wa ulaya nchini Misri na Saud Arabia baadae hii leo.

Wawakilishi wa pande nne zinazosimamia utaratibu wa amani ya mashariki ya kati,ambazo ni Marekani,Urusi,Umoja wa mataifa na Umoja wa ulaya wanatazamiwa kukutana wiki ijayo mjini Washington kukandaa mkutano wa dharura utakaoitishwa June 26 na 27 ijayo mjini Cairo.Duru za kuaminika zinasema huenda kiongozi wa utawala wa ndani Mahmoud Abbas na waziri mkuu Ismael Hanniyeh wakashiriki katika mkutano huo wa Cairo.

Katika maeneo ya utawala wa ndani kwenyewe,tawi la kijeshi la Hamas,limewataka watumishi wa idara ya usalama wanaomuunga mkono rais Mahmoud Abbas waweke chini silaha kabla ya saa moja za usiku hii leo.Hamas wanadai wameiteka sehemu kubwa ya kaskazini mwa Gaza.

Mapigano kati ya Hamas na Fatah yanaendelea na kuenea pia katika Ukingo wa magharibi.

Wanaharakati wa Hamas na wale wa Fatah wamepigana Naplouse baada ya mashahidi wa al Aqsa kukizingira kituo cha kunasia matangazo ya televisheni cha Hamas.Watumishi sabaa wa kituo hicho wametekwa nyara.

Hii ni mara ya kwanza kwa mapigano kuripotiwa Ukingo wa magharibi .Mapigano yaliyoripuka Gaza tangu June sabaa iliyopita huko Gaza yameshagharimu maisha ya zaidi ya watu 67.Pekee hii leo wapalastina 17 wameuwawa.

Fatah wamesema watajitoa katika serikali ya umoja wa taifa ikiwa mapigano hayatasita.

Askari polisi 40 wa Palastina wanaomuunga mkono rais Mahmoud Abbas wamekimbilia Misri hii leo wakiyapa kisogo mapigano yanayoendelea Gaza.

Na shirika la umoja wa mataifa la misaada kwa wapalastina limesitisha shughuli zake kwa muda hii leo baada ya watumishi wake wawili kuuliwa.

Israel inasema hali katika maeneo ya utawala wa ndani ndio itakayoamua hatima ya utaratibu wa amani ya mashariki ya kati. Wakati huo huo mwanasiasa aliyebobea,na mshindi wa amani ya Nobel Shimon Peres, amechaguliwa hii leo kua rais wa Israel.