Maoni ya wahariri juu ya Rais Hollande na sakata la udukuzi | Magazetini | DW | 19.11.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Maoni ya wahariri juu ya Rais Hollande na sakata la udukuzi

Wahariri wanazungumzia juu ya ziara ya Rais Hollande katika Mashariki ya Kati, sakata la udukuzi na madai ya kukiukwa haki za binadamu nchini Qatar.

Rais Francois Hollande wa Ufaransa na Rais wa Mamlaka ya ndani ya Palestina Mahmoud Abbas.

Rais Francois Hollande wa Ufarasna na Rais wa Mamlaka ya ndani ya Palestina Mahmud Abbas 18.11.2013

Mhariri wa gazeti la "Die Welt" anasema kuwa Rais Francois Hollande anastahili pongezi kwa kufanya ziara katika Mashariki ya Kati japo umaarufu wake unazidi kuteremka katika kura za maoni nchini mwake.


Mhariri wa "Die Welt" anatilia maanani katika maoni yake kwamba ni Ufaransa, iliyosimama na kupinga kufikiwa kwa makubaliano ya pupa na Iran kwenye mazungumzo juu ya mpango wa nyuklia wa nchi hiyo ya uajemi.Msimamo huo wa Ufaransa ni miongoni mwa maadili ya kimagharibi ambayo kwa sasa mtu hayaoni.

Sakata la udukuzi

Gazeti la " Bild" linazungumzia juu ya kukwaruzika kwa uhusiano baina ya Ujerumani na Marekani kutokana na sakata la udukuzi wa simu ya Kansela wa Ujerumani Angela Merkel. Hata hivyo Mhariri wa gazeti hilo anasema Kansela Merkel hayupo tayari kuyapalia makaa. Sababu ni kwamba Kansela huyo sasa yumo katika juhudi za kutanabahisha juu ya uhusiano baina ya Rais Vladmir Putin na nchi za jirani. Putin anajaribu kuzifunga nira nchi hizo,Ukraine,Georgia na Moldavia.Putin anajaribu kuzibana nchi hizo na kujaribu kuziamulia ni kwa kiasi gani zinaruhusiwa kuusogelea Umoja wa Ulaya. Ni msimamo wa Kansela Angela Merkel kwamba nchi hizo zina haki ya kujiamulia mambo yao.Na siyo wajibu wa Rais Putin.

Mhariri wa gazeti la "Die Rheinpfalz" anasema ni haki ya Ujerumani kulalamika juu ya upelelezi uliofanywa na Marekani.Mhariri huyo anatilia maanani kwamba msimamo huo ulisisitizwa tena jana na Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani Hans - Peter Friedrich wakati wa mjadala bungeni.

Kombe la Dunia, Qatar

Gazeti la "Weser Kurier" linataka kubatilishwa kwa uamuzi wa kuichagua Qatar kuwa mwenyeji wa mashindano ya kugombea kombe la dunia la kandanda mnamo mwaka wa 2022. Mhariri wa gazeti hilo anasema nchi kama Qatar inayokiuka haki za binadamu haistahili kuwa mwenyeji wa mashindano hayo. Tokea mwanzo kabisa uamuzi wa kuyapeleka mashindano ya kombe la dunia katika nchi hiyo ya jangwani ulikuwa wa makosa. Uamuzi huo unapaswa kusahihishwa mara moja. Bado pana muda wa kuyafanya masahihisho hayo.

Mwandishi: Mtullya Abdu./Deustche Zeitungen.

Mhariri: Josephat Charo