1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maonesha ya picha za Afrika Solingen

11 Novemba 2008

"Abbilder Afrika" ni maonesho ya picha juu ya Afrika ya mchoraji Bernd Schottdorf.

https://p.dw.com/p/Frmy

Ufukara,vita,misaada ya maendeleo- ndio maneno waandishi wa habari nchini Ujerumani, mara nyingi hupenda kuyatumia wanaporipoti juu ya Afrika. Lakini,kwa jicho la Bernd Schottdorf,mpiga-picha na mchoraji ,bara la Afrika lina pia sura nyengine na ni ulimwengu wa kipekee tofauti kabisa na dhana na fikra za wengi Ujerumani. Mchoraji na mpigapicha huyu, amefungua maonesho maalumu kwa jina la "ABBILDER AFRIKA" -sura ya Afrika katika jumba la makumbusho ya sanaa la Baden,mjini Solingen,kiasi ya mwendo wa nusu saa kutoka mjini Cologne.

Manesho haya juu ya picha za Afrika, azma yake ni kumsafirisha anaeyatembelea barani Afrika -bara la kutatanisha zaidi na lenye sura nyingi kuliko wazungu wengi wanavyofikiria.

Kuna zaidi ya picha 50 ukutani.Rangi mbali mbali kila unapotupa macho kwenye ukumbi wa maonesho.Kila unapoangalia kuna picha za wanaume,wanawake,watoto ambao wanamchekea mtembezi maoneshoni n a wakati mwengine wanamkodolea macho wazi.

mpiga picha na mchoraji mwenyewe akiwa ukumbini Bernd Schottdorf anasimulia:

"Hii ni Kilindoni,na hii ni Mlamo na hapa ni Tanzania -picha hii ikionesha watoto 4 wadogo wakiwa ndani ya marekebu ni kilindoni na hii yenye ngamia na kifaru bila shaka ni Eritrea."

Kwa mtu ambae zaidi ya mara 100 ametembelea nchi mbali mbali za Afrika ,Bernd Schottdorf anakumbuka mengi ajabu.Kwa kweli, Bernd Schottdorf,alizaliwa 1940 mjini Berlin na kazi yake ilikua daktari katika maabara na mwanabiashara.Uchoraji na sanaa ni sehemu ya maisha yake .Bara la Afrika lilikuwa na linaendelea kuwa na maana maalumu kwake.

"Shauku ambayo nilikuwa nayo mwanzo, ilitokana na kuingiwa kidogo na huzuni kuona jinsi gani Ujerumani baada ya kumalizika vita vya pili vya dunia,mapinduzi ya kilimo yalingoa kila kitu ambacho nilijionea utotoni mwangu.Hapo tena nilisafiri mara kwa mara barani Afrika na kujionea mengi tena moja kwa moja kule ambako mtu hafiki anapokwenda kama mtalii."

Na kile ambacho Bernd Schottdorf amejionea ama alikipiga picha au alichora tena kwa aina pekee mtayarishaji wa maonesho Jurgen Kaumkotter anasimulia:

"Wanaotembelea maonesho haya, watasangaa ,kwavile, yanaonesha Afrika nyengine kabisa kuliko walioizowea kuineshwa katika vyombo vya habari.Yaonesha aina mbali mbali za sura ya Afrika na yaonesha pia bila uwezo mkubwa waweza kufanya mengi. Yaonesha furaha maishani, utamaduni na jinsi vipimo vyengine vya kimaisha vilivyo na thamani nyengine kuliko tunavyodhania .Na hii ndiyo inayopendeza mno maoneshoni ."

Katika ghorofa mbili picha za Bernd Schottdorf zimeenea ukutani mjini Solingen,zikioneshwa pamoja na sanaa za kiafrika .Picha na michoro zinaonesha hasa binadamu mfano wakati wa sherehe za ulimwengua za voodoo za

Januari mwaka huu huko Benin.

Jicho jengine analopata anaetembelea maonesho haya, ni kusoma na kuangalia kitabu cha muandsihi aliezaliwa Kongo-Brazzaville,Wilfried NSonde kwa jina la "Moyo wa watoto wa chui".Riwaya yake imetoka hivi punde katika maduka ya vitabu nchini Ujerumani na kimejulishwa katika maonesho haya ya Solingen "Abbilder Afrika".

Kitabu cha Nsonde, ni hadithi ya kijana mweusi kutoka kitongoji cha mji wa Paris alieshtakiwa kwa uhalifu ambao kamwe hakuufanya.Muandishi wa kitabu hiki ametumia picha nyingi za kuvutia za Afrika sawa na zile unazoweza kujionea katika ukumnbi wa maonesho haya mjini Solingen.