1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makubaliano ya nyuklia ya Iran kufikiwa karibuni?

Lilian Mtono
24 Agosti 2022

Marekani imesema jana kwamba Iran imekubali kulegeza masharti muhimu yaliyokuwa yakizuia kufufuliwa kwa makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015. Kinachosubiriwa sasa ni kile kitakachosemwa na rais Joe Biden.

https://p.dw.com/p/4FwYC
USA Präsident Biden Klima und Gesundheit
Picha: Susan Walsh/AP Photo/picture alliance

Marekani inatarajiwa kuijibu Iran siku chache zijazo kupitia wasuluhishi ambao ni Umoja wa Ulaya, baada ya mwaka mmoja na nusu wa diplomasia isiyo ya moja kwa moja ambayo hata hivyo wiki iliyopita ilionekana kama inafikia ukingoni.

Maafisa wa Marekani wamesema Iran imekubali kuondoa masharti ya kuwazuia wakaguzi wa Umoja wa Mataifa kukagua baadhi ya vinu vya nyuklia na sharti jingine ambalo waliitaka Washington kukiondoa Kikosi chake cha walinzi wa mapinduzi cha Jeshi la Iran kwenye orodha mbaya ya ugaidi.

Kulingana na maafisa hao, Marekani huenda ikatoa majibu ya maoni ya Iran kuhusu rasimu ya mapendekezo yaliyofikishwa kwao na Umoja wa Ulaya hii leo Jumatano na baada ya hapo kunatarajiwa kuwepo na mabadilishano mengine ya maelezo ya kiufundi. Hatua hizi mpya zinaonyesha dhahiri kwamba makubaliano hayo yanaweza kufikiwa hivi karibu.

Soma Zaidi: Ines Pohl: Hatari ya mamlaka na nguvu za rais Donald Trump

Atomanlage im Iran
Mtambo mmojawapo wa nyuklia wa Iran uliopo maili 200 kutoka kusini mwa Tehran.Picha: Getty Images

Hata hivyo, msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Marekani Ned Price amesema bado kuna vizingiti vinavyotakiwa kushughulikiwa ili kuepusha juhudi za kuurejesha mkataba huo kurejeshwa nyuma.

"Tunatiwa moyo na ukweli kwamba Iran inaonekana kuondoa baadhi ya matakwa yake, kama vile kuondoa Shirika la Kigaidi la Kigeni, la IRGC au Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Mmesikia kutoka kwetu kwa siku kadhaa zilizopita kwamba bado kuna maswala kadhaa ambayo lazima yatatuliwe," alisema Price.

Huko Washington, serikali ya Biden bado inakabiliwa na upinzani mkubwa wa kisiasa kuhusiana na kuurejesha mkataba huo kutoka kwa pande zote mbili, Democratic na Republican bungeni, wakati wabunge hao wakisisitiza kwamba bado hawajashawishika kwamba makubaliano hayo ni kwa maslahi ya usalama wa taifa la Marekani.

Madai ya hivi karibuni ya raia wa Iran kupanga kumuua mshauri wa zamani wa usalama wa taifa, John Bolton na shambulio dhidi ya mwandishi wa habari Salman Rushdie kwa pamoja vinatajwa kama viashiria kwamba Iran haiwezi kuaminiwa.

Wakati huo huo, mshirika mkuu wa Marekani katika ukanda wa Mashariki ya Kati, Israel inaonekana kushtushwa na harakati hizi baada ya waziri mkuu mbadala wa Israel Naftali Bennett jana Jumanne kuitolea mwito serikali ya Biden kuachana na mpango huo na Iran.

Amesema ingawa Israel haikuwa sehemu ya makubaliano hayo yaliyosainiwa na mataifa matano makubwa ya Marekani, Uingereza, Urusi, Ufaransa, China pamoja na Ujerumani, lakini ndio muathirika wa moja kwa moja na kwa maana hiyo lina haki ya kuangalia namna ya kujilinda.

Mashirika: APE/AFPE