Mahakama ya uhalifu wa kivita kuwakamata vigogo wa Sudan | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 11.07.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Timu Yetu

Mahakama ya uhalifu wa kivita kuwakamata vigogo wa Sudan

Rais Bashir aweza kukamatwa kuhusu Darfur

Rais wa kijeshi wa Sudan Omar Hassan al-Bashir.

Rais wa kijeshi wa Sudan Omar Hassan al-Bashir.

Viongozi fulani wa ngazi ya juu nchini Sudan huenda wakahitajika kukamatwa na mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ICC ya mjini The Hague, Uholanzi wakati mwendesha mashtaka mwandamizi atakapokuwa anafungua kesi mpya za makosa ya jinai kuhusu Darfur.

Miongoni mwa viongozi hao wa ngazi za juu wa serikali ya Khartoum ametajwa rais Omar El Bashir .

Kulingana na taarifa iliyotolewa na upande wa mashtaka wa mahakama hiyo, mwendesha mashtaka mkuu Luis Moreno-Ocampo atawasilisha ushahidi alionao kwa majaji ili kutaka kutolewa waraka wa kukamatwa kwa watu binafsi.

Hata hivyo taarifa haikutoa maelezo zaidi.

Ushahidi unaozungumzwa hapa ni kuhusu makosa yaliyofanyika katika eneo la Sudan la Darfur kwa kipindi cha miaka mitano.

Sudan inasema kuwa hatua kama hiyo inaweza ikavuruga mchakato wa kuleta amani Darfur, na maafisa wa kutoa misaada wanahofu kuwa hatua hiyo itapingwa vikali.

Pia uchunguzi kuhusu Darfur unaweza ukaiaibisha China,wakati huu ambapo zimesalia wiki chache kufunguliwa kwa michezo wa Olimpiki mjini Beijing.

China ni mshirika wa karibu wa Sudan.

Gazeti la Marekani la Washington Post,likiwanukuu maafisa pamoja na wanadiplomasia wa Umoja wa mataifa, limeripoti kuwa mwendesha mashataka mkuu wa mahakama ya uhalifu wa kivita ataomba waranta wa kumkamata kiongozi wa Sudan, Omar Hassan al-Bashir,ili kumfungulia mashtaka dhidi ya mauaji ya halaiki na makosa dhidi ya binadamu.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,Ban Ki-moon amekataa kusema nani atatajwa katika ripoti ya mwendesha mashataka mkuu au athari zinazoweza kukipata kikosi cha muungano wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika kinacholinda amani Darfur,hasa wakati huu ambapo kimepoteza wanajeshi wake saba baada ya kushambuliwa jumanne na wanamgambo ambao hawajatambuliwa baado.

Bw.Ban Ki-moon aliuambia mkutano wa waandishi habari kuwa amani haiwezi kuimarishwa bila ya kutenda haki, na kuongeza kuwa itambidi atathmini hali zote wakati mahakama ya ICC itakapotoa tangazo.

Nae mwendesha mashtaka mkuu kwa upande wake alisema mwezi uliopita kuwa, karibu vyombo vyote vya dola vilihusika kwa njia moja au nyingine, katika kampeini ya kuwashambulia raia katika eneo la Darfur na kuahidi kutoa ushaidi huo mwezi huu.

Tayari ICC imesha toa waraka wa kukamtwa kwa washukiwa wawili Sudan,waziri mmoja Ahmed Harun pamoja na mkuu wa wanamgambo Ali Khushayb.

Utawala wa Khartoum umekataa kuwakabidhi watu hao ikisema kuwa mahakama zake zinauwezo kushughulikia makosa ya uhalifu wa kivita.

Balozi wa kudumu wa Sudan katika Umoja wa Mataifa,Abdel-Mahmood Abdalhaleem amemuiita mwendesha mashtaka mkuu kama mtu asiewajibika, na kuliambia shirika la habari la Reuters kuwa hawatingishiki na vitisho vyake.

Balozi huyo ameongeza kuwa ikiwa atamhusisha rais Bashir iitamlazimu mwendesha mashtaka huyo pia, awahusishe raia millioni 40 wa Sudan kwani nao wanapinga vikali kile alichokiita-vitisho.

China imeishauri Sudan kushirikiana na Umoja wa mataifa katika juhudi za kuutanzua mgogoro wa Darfur.Hata hivyo China imelaumiwa sana na mataifa ya magharibi kwa kutofanya chochote kwani inaiuzia Sudan silaha na pia kununua mafuta yake.

Watalaamu wa kimataifa wanasema takriban watu laki mbili wameuawa Darfur na wengine millioni mbili unusu kuachwa bila makazi tangu uasi utokee mwaka wa 2003.

Khartoum inasema kuwa idadi kamili ya waliokuwa ni elf 10.

Mahakama ya ICC iliundwa mwaka wa 2002 mjini The Hague ili kuchunguza makosa ya jinai nchini Uganda,Jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo, na Jamhuri ya Afrika ya Kati lakini hadi sasa ina wazuilia watu wanne tu na wote kutoka Kongo ya Kinshasa.

 • Tarehe 11.07.2008
 • Mwandishi Kalyango Siraj
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/EaQs
 • Tarehe 11.07.2008
 • Mwandishi Kalyango Siraj
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/EaQs
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com