Maandamano dhidi ya ″Innocense of Muslims″ yaendelea | Matukio ya Kisiasa | DW | 21.09.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Maandamano dhidi ya "Innocense of Muslims" yaendelea

Maelfu ya raia nchini Pakistan wanatarajiwa kuingia mitaani baada ya swala ya Ijumaa kuandamana, kupinga filamu inayoukashifu Uislamu, na vikaragosi vya Mtume Muhammad vilivyochapishwa na jarida moja nchini Ufaransa.

Waumini wa dini ya Kikristu nchini Pakistan wakiandamana kupinga filamu ya Innocense of Muslims inayoukashifu Uislamu.

Waumini wa dini ya Kikristu nchini Pakistan wakiandamana kupinga filamu ya Innocense of Muslims inayoukashifu Uislamu.

Balozi za mataifa ya magharibi katika nchi za kiislamu ziliwekwa katika tahadhari kubwa kabla ya swala ya Ijumaa, ambayo mara nyingi hufuatiwa na maandamano. Serikali ya Pakistan iliitangaza siku ya Ijumaa kuwa ni ya mapumziko, ikiitaja kuwa ni siku ya mapenzi kwa mtume, na iliwataka watu kuandamana kwa amani ili kuonyesha upinzani wao kwa filamu hiyo iliyotengenezwa kwa mtindo wa chini sana na kupewa jina la "Innocensce of Muslims". Vyama vyote vikubwa vya siasa nchini humo na makundi ya dini vilitangaza kufanya maandamano, kama yalivyotangaza makampuni ya biashara na usafirishaji.

Mawakili wa Pakistan wakiichoma bendera ya Marekani wakati wanajaribu kuingia ubalozi wa nchi hiyo mjini Islamabad siku ya Alhamis.

Mawakili wa Pakistan wakiichoma bendera ya Marekani wakati wanajaribu kuingia ubalozi wa nchi hiyo mjini Islamabad siku ya Alhamis.

Maduka, masoko na vituo vya mafuta vilitarajiwa kufungwa na shughuli za usafiri zitasimama, lakini mamlaka zimesema zinatumaini hakutakuwa na marudio ya fujo zilizoshuhudiwa siku ya Alhamisi mjini Islamabad. Katika ishara ya kile kinachotarajiwa Ijumaa, makundi nchini Nigeria, Iran na Afghanistan yalikuwa yakiimba nyimbo za "Kifo kwa Ufaransa, kifo kwa Marekani, kifo kwa Israel."

Serikali ya Marekani yajitenga na filamu hiyo

Filamu hiyo imesababisha maandamano katika mataifa yasiyopungua 20 tangu vipande vyake viwekwe kwenye mtandao wa Youtube, na zaidi ya watu 30 wameuawa katika vurugu zinazohusiana nayo. Wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani imewaonya raia wake dhidi ya kusafiri kwenda Pakistan, na utawala mjini Washington umelipia matangazo katika vituo vya Televisheni nchini Pakistan katika jaribio la kujitenga na filamu hiyo.

"Tangu kuanzishwa kwetu, Marekani imekuwa nchi inayoheshimu dini zote. Tunapinga juhudi zozote zinazolenga kushusha hadhi ya dini za watu wengine," anasemarais Barack Obama katika sehemu ya tangazo hilo.

Pia, waziri wa mambo ya kigeni, Hillary Clinton anaokena akisistiza kwamba serikali ya Marekani haikuhusika kwa namna yoyote ile na video hii na kwamba serikali hiyo inapinga kwa nguvu zote, yaliyomo kwenye filamu hiyo pamoja na ujumbe wake.

Je,wapakistan wataulewa ujumbe huo?

Ingawa ujumbe huo wa rais Obama na waziri Clinton siyo mpya, wizara ya mambo ya kigeni inasema haukuwafikia vizuri Wapakistani na ndiyo maana Marekani imeamua kutumia kiasi cha dola elfu 70 kuulipia. Ubalozi wa Marekani mjini Islamabad pia umetuma maafisa wake mitaani wakifanyiwa mahojiano na vyombo vya habari kujaribu kubadilisha mtizamo wa raia wa Pakistan dhidi ya Marekani kuhusiana na filamu hiyo.

Lakini Mhariri wa jarida la Foreign Policy la Marekani, anasema ujumbe huo hautokuwa na athari kwa raia hao ikizingatiwa kuwa wamekuwa na historia ya kuichukia Marekani. Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni Victoria Nuland, alisema waliamua kulipia ujumbe huo kwa kuwa serikali ya Pakistan iliwashauri wafanyehivyo.

Wanawake nchini Iran wakiandamana mbele ya ubalozi wa Ufaransa kupinga uchapishaji wa vikaragosi vya Mtume Muhammad na jarida la Charlie Hebdo la nchini Ufaransa.

Wanawake nchini Iran wakiandamana mbele ya ubalozi wa Ufaransa kupinga uchapishaji wa vikaragosi vya Mtume Muhammad na jarida la Charlie Hebdo la nchini Ufaransa.

Kwa upande wake, serikali ya Sudan imetaka mtandao waYoutube ufungiwe nchini humo ili kuzuia watu kuitizama filamu hiyo. Wakati huo Ujerumani imesitisha mkutano wa kujadili namna ya kuongeza uwekezaji nchini Sudan, uliyokuwa ufanyike mwezi ujao, kufuatia vurugu zilizopelekea kuchomwa kwa ubalozi wa Ujerumani mjini Khartoum. Na nchini Tunisia, ambako machafuko ya wiki iliyopita yalisababisha uharibifu mkubwa kwenye ubalozi wa Marekani, serikali imetangaza kuyapiga marufu maandamano.

Ufaransa nayo katika mtihani

Ufaransa nayo imejikuta katika wakati mgumu kufuatia kuchapishwa kwa michoro ya katuni zinazomuonyesha mtume Muhammad na jarida la Charlie Hebdo, zikiwemo mbili zinazomuonyesha akiwa uchi. Serikali ya Ufaransa ilipinga maandamano yaliyopangwa siku ya Jumamosi mbele ya msikiti mkuu wa Paris na imetangaza kufunga balozi na shule zake katika mataifa 20 leo.

Viongozi wa jumuiya ya kiislamu nchini Ufaransa, ambayo ndiyo kubwa zaidi barani Ulaya wamesema miito ya kuwepo na utulivu itasomwa misikitini nchini kote, lakini pia wamelaani kitendo cha jarida hilo kuchapisha michoro hiyo. Mhariri wa jarida hilo, Stephane Charbonnier, aliwadhihaki waliochukizwa na vikaragosi hivyo kwa kuwaita 'vichekesho', huku akiikosoa serikali kwa alichokiita kuwaendekeza na kuungana nao kulikosoa jarida hilo.

Mwandishi:Iddi Ismail Ssessanga/AFPE
Mhariri: Josephat Nyiro Charo

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com