1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Libya yataka mkataba na Ulaya

Mohamed Dahman7 Machi 2008

Libya yataka pia ushirikiano wa kiuchumi na Marekani

https://p.dw.com/p/DK3S
Kiongozi wa Libya Kanali Muammar Gaddafi.Picha: picture-alliance/dpa

Libya yakusudia kusaini mkataba wa ushirikiano na Umoja wa Ulaya mwaka 2008 na kuanzisha uhusiano madhubuti wa kiuchumi na hasimu wake wa zamani Marekani.

Dhamira hiyo ya Libya imebainishwa na waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo iliotengwa hapo zamani.

Abdel -Rahman Shalgam ameongeza kusema kwenye matamshi yake kwa bunge kwamba atasafiri kuelekea Uingereza wiki ijayo kusaini mkataba wa kubadilishana wafungwa na Waziri Mkuu wa nchi hiyo Gordon Brown.

Kufuatia mazungumzo ya miezi kadhaa kati ya Uingereza na Libya juu ya mkataba wa ushirikiano kuhusu masuala ya kisheria ikiwa ni pamoja na uhamishaji wa wafungwa kumezusha ishara zilizokanushwa na serikali ya Uingereza kwamba nchi hiyo inapanga kumrudisha nyumbani Abdel -Basset al -Megrahi aliepatikana na hatia ya kuripua ndege juu ya anga ya Lockerbie.

Megrahi jasusi wa zamani wa Libya anatumikia kifungo cha maisha huko Scotland kutokana na kuripua ndege hapo mwaka 1988 juu ya anga ya mji wa Lockerbie ambapo kwayo watu 270 waliuwawa.

Shalgam amesema ziara ya kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi huko Ureno,Ufaransa na Uhispania mwaka jana zimepelekea kuwepo kwa jaribio jipya la kuimarisha uhusiano na Ulaya ambayo inachukuwa takriban mafuta yote yanayosafirishwa nje na nchi hiyo mwanachama wa Shirika la Nchi zinazozalisha mafuta kwa wingi duniani OPEC.

Katika hotuba yake kwa bunge wiki hii waziri huyo wa mambo ya nje wa Libya amesema wameanza mazungumzo kabambe ya ushirikiano na Umoja wa Ulaya.

Halmashauri ya Umoja wa Ulaya mwezi uliopita ilipendekeza kuanzisha mazungumzo kuhusu ushirikiano wa karibu wa kisiasa na kiuchumi na Linbya mwaka huu kama sehemu ya kuimarisha uhusiano na msambazaji huyo wa nishati.

Uhusiano wa Umoja wa Ulaya na Libya ulikuwa umekwama kwa miaka mingi kutokana na madai kwamba serikali ya Libya ilikuwa ikiunga mkono ugaidi. Makao makuu ya Umoja wa Ulaya mjini Brussels ilitangaza hapo mwezi wa Julai kwamba itaimarisha uhusiano wake na Libya baada ya nchi hiyo kuwaachilia huru waaguzi wa Kibulgaria waliokuwa wakituhumiwa kuwambukiza virusi vya HIV watoto wa Libya.

Katika makubaliano yaliofikiwa ya kuwaachilia huru wauguzi hao Umoja wa Ulaya umeipa matumaini Libya ya kupatiwa nafasi zaidi za masoko kwa biadhaa zake za uvuvi na kilimo na ushirikiano katika suala la uhamiaji na utalii.

Shalgam amesema kuna matatizo ya kisheria na Marekani na kwamba Libya inapinga sera ya Marekani kwa Iraq,Palestina na Syria lakini wamepiga hatua kutoka sera ya malumbano na kuelekea ile ya mazungumzo na kwamba ili kufanikisha maendeleo ya nchi hiyo baada ya vikwazo vya miaka 20 uhusiano wa kiuchumi na kitamaduni na Marekani hauna budi kuwa madhubuti.

Hapo mwezi wa Mei mwaka 2006 utawala wa Rais Bush ulisema utarudisha uhusiano wake rasmi na Libya kama tuzo kwa Libya kwa kuachana na mpango wake wa kutengeneza silaha za maangamizi.

Lakini masuala ya kisheria yaliokosa uvumbuzi ikiwa ni pamoja na kesi zinazohusu Lockerbie na uripuaji wa bomu kwenye disko la Ujerumani hapo mwaka 1986 yanaendelea kuwa vikwazo.Wananchi wa Marekani walikufa katika matukio yote mawili na sheria mpya ya Marekani imetanuliwa kuwawezesha wahanga wa ugaidi wa Marekani kudai fidia.

Waraka wa maelewano ulisainiwa hapo mwezi wa Mei mwaka 2007 wakati wa ziara nchini Libya ya aliekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza wakati huo Tony Blair kufanya mazungumzo ya kuwa na mkataba kuhusu ushirikiano wa kisheria katika kipindi kisichozidi mwaka mmoja katika masuala kama vile sheria ya biashara na kurudisha na kuhamisha wafungwa.