1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kutanuwa malengo ya Urusi ni propaganda mpya - Baerbock

Mohammed Khelef
21 Julai 2022

Waziri wa Mambo wa Kigeni wa Ujerumani amesema madai ya Urusi kuchukuwa maeneo zaidi ya Ukraine mbali ya Donbas hayana uhalali wowote, huku akionya juu ya "ghiliba za mataifa mengine."

https://p.dw.com/p/4ESHq
Annalena Baerbock im DW-Interview
Picha: DW

Annalena Baerbock ametumia mazungumzo hayo marefu na DW mjini Hannover siku ya Jumatano (20 Julai) kuweka rikodi sawa juu ya msimamo wa Ujerumani panapohusika uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine.

Waziri huyo wa mambo ya kigeni aliyakataa madai ya Urusi kwamba hatua ya mataifa ya Magharibi kutuma silaha za kivita kwa Kiev inachochea pakubwa uamuzi wake wa kutanuwa malengo yake ya kijeshi nchini Ukraine.

"Imekuwa hivyo hivyo kwenye miezi iliyopita: tunaiunga mkono Ukraine sio tu kwa mshikamano, bali pia kwa kuonesha kila siku kwamba huu ni uvunjaji mkubwa wa sheria za kimataifa unaofanywa na Urusi, na pia kwa msaada wa kijeshi ili waweze kuilinda nchi yao, mipaka yao. Urusi inatumia hoja tafauti kila wakati. Mara hii ni kwa sababu ya msaada ya kijeshi, wanasema. Lakini wamekuwa wakiishambulia Kiev na maeneo mengine ya Ukraine hata kabla ya msaada huo. Kwa hivyo ni propaganda mpya tu ya Urusi." Alisema Baerbock.

Mapema siku ya Jumatano, Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Urusi Sergei Lavrov alisema malengo ya kijeshi ya Moscow sasa yamekwenda mbali zaidi ya Donbas.

Badala ya kujikita kwenye mikoa ya kaskazini yaDonestk na Luhansk, ambako waasi wanaoungwa mkono na Urusi wamekuwa wakiendesha uasi tangu mwaka 2014, Lavrov alisema Moscow imeelekeza pia macho yake kwenye mikoa ya kusini ya Kherson na Zapozizhzhia. Waziri huyo wa mambo ya nje wa Urusi alionya kuwa malengo ya nchi yake yatazidi kutanuka ikiwa mataifa ya Magharibi yanaendelea kutuma silaha za masafa marefu kwa Ukraine.

Hakuna mashindano ya silaha

Hata hivyo, kwenye mazungumzo yake na DW, Baerbock alisema licha ya Ujerumani kukosolewa kwa kutokuwa kwenye nafasi tatu za juu miongoni mwa mataifa yanayotuma silaha kwa wingi nchini Ukraine, Berlin haijaiwacha mkono Ukraine, akihoji kwamba hilo halimaanishi kuwa wanaingia kwenye mashindano ya silaha na mtu yeyote.

"Takwimu ni tafauti kama unahisabu pesa ama unahisabu uzito wa silaha zenyewe. Lakini haya si mashindano ya silaha juu ya nani yuko juu ya nani. Huu ni msaada kutoka jumuiya ya kimataifa kwa ujumla wake, kutoka wanachama wa NATO, kuiunga mkono Ukraine. Ndio maana tunachanganya msaada wetu na wengine, kwa sababu kwenye baadhi ya maghala hatuna kila kitu." Alisema waziri huyo wa mambo ya kigeni wa Ujerumani.

Kwenye mahojiano hayo, Baerbock ametowa wito kwa bara la Ulaya kutojiwachia likaghilibiwa na vitisho vya Urusi kutokana na utegemezi wao wa nishati na bidhaa za vyakula kwa taifa hilo ambalo alisema linatumia nishati kama kura ya kujipatia ushawishi lisiostahiki.

DW-Interview mit Bundesaußenministerin Baerbock
Picha: Zura Karaulashvili/DW