1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yaendelea kuishambulia Ukraine

19 Julai 2022

Huku Urusi ikiendelea na mashambulizi ya mara kwa mara kuelekea nchini Ukraine, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy amewafuta kazi watumishi 28 wa shirika la ujasusi la nchi hiyo, SBU.

https://p.dw.com/p/4ELUH
Ukraine | Wolodymyr Selenskyj in Dnipro
Picha: Ukrainian Presidential Press Office/AP/dpa/picture alliance

Siku moja baada ya kumfungisha virago mkuu wa masuala ya ujasusi, Ivan Bakanov kwa madai kwamba walihifadhi watu hasimu na wasaliti.

Katika hotuba ya kila jioni kwa taifa lake, Zelenskiy amesema kuwa watumishi waliofukuzwa wanatoka katika ngazi mbali mbali za shirika hilo, na kusema sababu za wao kuondolewa ni kutokuwa na ufanisi wa kutosha kazini.

"Na habari moja muhimu zaidi kuhusu Huduma ya Usalama ya Ukraine. Ukaguzi wa wafanyakazi unafanyika. Suala la kufukuzwa kazi kwa maafisa 28 linazingatiwa kwa viwango tofauti na mwelekeo tofauti. Lakini misingi ni sawa... utendaji wa kazi usioridhisha." amesema Zelensky.

Hata hivyo maafisa wa Marekani jana Jumatatu walisema Washington itaendelea kuipatia taarifa za kijasusi Ukraine ambazo Kyiv hutumia kujibu mashambulizi ya Moscow.

Mashambulizi zaidi

Ukraine-Krieg | zerstörte russische Panzer
Picha: IRINA RYBAKOVA/UKRAINIAN GROUND FORCES/REUTERS

Huku haya yakijiri mamlaka ya Ukraine imeripoti kuwa vikosi vya Urusi leo viliendelea kuishambulia kwa mabomu na makombora huku mashambulizi makali zaidi yakilenga maeneo ya Sumy kaskazini, Mykolaiv na Odesa kusini.

Ukraine imesema vikosi vya Urusi vimezidisha mashambulizi ya masafa marefu na kulenga maeneo mengine mbali na uwanja wa vita na kusabisha mauwaji ya idadi kubwa ya raia, kauli ambayo Moscow inakanusha kwa kusema imekuwa ikilenga maeneo ya kijeshi.

Nini hatma ya bomba la gesi?

Deutschland | Gas Pipeline Nord Stream 1
Kampuni ya bomba la gesiPicha: Hannibal Hanschke/REUTERS

Aidha wiki hii inaweza kuwa muhimu kwa nchi za Ulaya kuhusu athari ya vita hivyo na vikwazo kwa usambazaji wa gesi wakati Urusi ikitarajia kufungua tena bomba lake kuu la gesi asilia la Ujerumani, Nord Stream 1, baada ya kufungwa kwa matengenezo, lakini mataifa ya Ulaya yana wasiwasi Moscow inaweza kuendelea kulifunga.

Kulingana na barua iliyoonekana na shirika la habari la Reuters, Kampuni ya Gazprom ya Urusi, ambayo inaendesha bomba hilo, imesema haiwezi kuwahakikishia wateja wake wa Ulaya usambazaji wa gesi kwa sababu ya  kile ilichokitaja kama hali "zisizo za kawaida", na kuzua mjadala kwamba Urusi inatumia bomba hilo kulipiza kisasi baada ya kuwekewa vikazo vya kiuchumi na nchi za Magharibi.

Hapo jana Urusi ilisema waziri wake wa Ulinzi Sergei Shoigu ameamuru vikosi vya jeshi kuzingatia kuharibu roketi na silaha za Ukraine zinazotolewa na Magharibi.

Wakati huo huo mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya walikubaliana kutoa euro milioni 500 nyingine fedha za manunuzi ya kununua silaha, na kuongeza msaada wa umoja huo kuelekea Ukraine hadi euro bilioni 2.5 tangu tangu Moscow ilipovamia Februari 24.

 

Vyanzo/Reuters/AP