Kura ya maoni kuhusu uhuru wa Sudan Kusini huenda isifanyike | Matukio ya Kisiasa | DW | 13.08.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Kura ya maoni kuhusu uhuru wa Sudan Kusini huenda isifanyike

Tume inayoandaa kura ya maoni kuhusu uhuru wa Sudan Kusini inakabiliwa na mkwamo hivyo kuhatarisha uwezekano wa kufanyika kura hiyo ya maoni iliyopangwa kufanyika Januari 9 mwaka ujao 2011

default

Kiongozi wa SPLM, Salva Kiir Mayardit (kushoto) akizungumza na rais wa Sudan, Omar al-Bashir

Chama tawala huko Sudan Kusini kimesema leo kwamba kura ya maoni kuwauliza wananchi wa eneo hilo kama wanataka uhuru kutoka kwa Sudan, haitafanyika hadi mkwamo ndani ya tume inayoiandaa kura hiyo utakapopatiwa ufumbuzi katika wiki chache zijazo. Pagan Amum, katibu mkuu wa kundi la zamani la waasi la Sudan People´s Liberation Movement, SPLM, amesema chama tawala cha National Congress, NCP, hakijafaulu kuwavutia raia wa Sudan Kusini kuhusiana na suala la umoja wa taifa la Sudan, tangu kusainiwa mkataba wa amani mnamo mwaka 2005, uliovimaliza vita virefu vya wenyewe kwa wenyewe barani Afrika.

"Tume inaonekana imekwama katika mchakato wa kumchagua katibu mkuu. Kwa sasa imekwama na haiwezi kuendelea na shughuli zake," amesema Amum. Katibu mkuu ndiye atakayeiongoza tume hiyo na kusimamia bajeti yake. Amum pia amesema kama suluhisho halitapatikana katika wiki mbili zijazo kuhusiana na masuala yanayowakabili sasa, basi kura ya maoni itapigwa kabali na kuzikwa katika kaburi la sahau. Ameelezea wasiwasi wake kwamba wanachama wa tume hiyo wanafanya makusudi kuvuruga mchakato mzima kuelekea kura hiyo ya maoni.

Chama tawala nchini udan, cha NCP na chama cha SPLM vimekuwa vikigombana kuhusu utekelezaji wa kila sehemu ya mkataba wa amani. Wachambuzi wanasema chama cha NCP kinasita kuutelekeza mkataba huo huku SPLM kikiwa hakina uwezo wa kuutekeleza, hivyo kuukwamisha mkataba huo na kuzusha kitisho kipya cha Sudan kurejea kwenye mzozo.

Kura ya maoni kuhusu uhuru wa Sudan Kusini inatakiwa kufanyika sambamba na kura nyengine itakayoamua mustakabali wa eneo lenye utajiri mkubwa wa mafuta la Abbey, ikiwa lijiunge na kusini au kaskazini. Chama cha NCP na SPLM vimeshindwa kuunda tume itakayosimamia kura kuhusu eneo la Abbey ambalo mipaka yake bado haijawekwa.

SPLM inakilaumu chama tawala kwa sera ya kuwasaidia watu wa kuhamahama wa jamii ya Kiarabu ya Missiriya, kuishi katika eneo la mpakani la Sudan Kaskazini, hivyo kuwahamisha wakaazi wa eneo hilo wa kabila la Ngok Dinka kwa matumaini ya kubadili wizani wa kura katika kura ya maoni kuhusu uhuru wa Sudan Kusini. Katibu mkuu wa SPLM, Pagan Amum, amesema hali hiyo inatishia kuzuka kwa mauaji ya safisha-safisha na kuongeza kuwa chama chake kimeutaka Umoja wa Mataifa uingilie kati kuutanzua mzozo huo. Chama tawala nchini Sudan, NCP kimekanusha madai hayo.

Mwandishi: Josephat Charo (RTRE)

Mhariri: Abdul-Rahman

 • Tarehe 13.08.2010
 • Mwandishi Josephat Nyiro Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/OmVX
 • Tarehe 13.08.2010
 • Mwandishi Josephat Nyiro Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/OmVX
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com