Kundi mpinzani wa Iran lashambuliwa Iraq. | Matukio ya Kisiasa | DW | 29.07.2009
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Kundi mpinzani wa Iran lashambuliwa Iraq.

Kundi kubwa zaidi la upinzani nchini Iran lililo uhamishoni limelaani uvamizi ulioendeshwa na serikali ya Iraq katika kambi moja wanamoishi wafuasi wake.

default

Polisi waendesha uvamizi katika kambi mjini Ashraf nchini Iraq.

Msemaji wa kundi hilo la National Council of Resistance of Iran linalojumuisha kundi lililojihami la People`s Mujahedeen of Iran waliulaani uvamizi huo.

"Kila mtu anafahamu kuwa uongozi wa kiongozi wa kidini nchini Iran, Ayatollah Ali Khamenei alihusika na hili. Anajaribu kusalia madarakani na hafichi hofu aliyo nayo na kundi la People`s Mujahedeen," alisema Afchine Alavi.

Wairan wanaoishi uhamishoni nchini Irak wanamshutumu kiongozi wa kidini nchini Iran Ayatollah Ali Khamenei kwa kumshinikiza waziri mkuu wa Iraq Nuri al Maliki kuvishambulia vituo vyao katika mji wa Ashraf nchini Iraq.

Kiongozi wa kundi la National Council of Resistance of Iran Maryam Rajavi wakati huo huo amemuomba rais wa Marekani Barack Obama na serikali yake kuingilia kati na kuzuia maafa ya kibinadamu nchini Iraq.

"Uvamizi huu ni kinyume na makubaliano na hakikisho la serikali ya Marekani na ile ya Iraq kuhusu kuwalinda wakazi wa mji wa Ashraf," amesema Rajavi. Polisi wa Iraq waliivamia kambi hiyo hapo jana katika oparesheni iliyosababisha zaidi ya watu 250 kujeruhiwa.

Watu wapatao 6 wameripotiwa kuuawa na wengine zaidi ya 50 kukamatwa. Hata hivyo utawala wa Iraq umekanusha kutokea kwa vifo wakati wa uvamizi huo lakini ukathibitisha kuwa watu 50 walikamatwa.

Polisi waliofanya uvamizi mapema leo wameondoka katika kambi hiyo ya Ashraf kufuatia mazungumzo kati ya mkuu wa polisi katika mkoa wa Diyala na kundi la Peoples Mujahedeen, na mahala pao pakachukuliwa na wanajeshi wa Iraq.

Mkuu huyo wa polisi amesema kuwa idadi ya wale waliojeruhiwa wakati wa uvamizi huo imefikia watu 300 wakiwemo wanawake 25. Pia maafisa 110 wa usalama walijeruhiwa wakati wa uvamizi huo.

Ripoti zaidi zinasema kuwa wakaazi wa kambi hiyo wamesusia chakula wakitaka wanajeshi wa Iraq waondolewe katika eneo hilo na badala yake wanajeshi wa Marekani wachukue mahala pao.

Ashraf ni makaazi ya karibu wafuasi 3,500 wa kundi la Mujahedeen na familia zao. Kambi hiyo ilibuniwa mnamo miaka ya 80 wakati rais wa zamani wa Iraq Saddam Hussein alikuwa vitani na Iran na kuwa kama kituo cha kuendesha oparesheni dhidi ya Iran.

Baada ya Marekani kuendesha uvamizi nchini Iraq mwaka 2003 kumng´oa madarakani rais marehemu Saddam Hussein, wanajeshi wa Marekani waliwapokonya silaha wapinzani hao wa Iran ambao wanatambulika na Marekani kama kundi la kigaidi.

Wakati huo huo, Iran imeupongeza uvamizi katika kambi hiyo ambayo inawataja wakaazi wake kuwa waasi. Iran inasema kuwa kabla ya kuondolewa madarakani rais wa zamani wa Iraq marehemu Saddam Hussen kundi la Peoples Mujahedeen of Iran mara kwa mara liliivamia Iran na kusasabisha kutokea kwa mapigano kati yao na jeshi la Iran.

Marekani imesema inafuatilia kwa karibu uvamizi wa kambi ya Ashraf. Msemaji wa wizara ya mambo ya ndani nchini Marekani, Ian Kelly, amesema kuwa ni wajibu wa serikali ya Iraq kushughulikia usalama wa kambi hiyo.

Mwandishi :Jason Nyakundi/AFPE

Mhariri :Josephat Charo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com