Kumalizika mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya | Matukio ya Kisiasa | DW | 30.10.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Kumalizika mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya

Mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya umemalizika

default

Rais Vaclav Klaus wa Jamhuri ya Cheki, katika mkutano na waandishi wa habari mjini Prague

Mkataba wa Lisbon wa kuufanyia marekebisho Umoja wa Ulaya umepita kiunzi chake cha mwisho. Wakuu wa serekali na nchi wanachama wa Umoja huo jana waliyakubalia matakwa ya rais wa Jamhuri ya Cheki, Vaclav Klaus, kwa maslahi ya nchi hiyo. Kwa hivyo, yaonesha kikwazo ambacho kiliwekwa na Bwana Klaus kabla ya kufanyiwa marekebisho hayo sasa kimemalizika.

Rais Vaclav Klaus aliyeleta mushkili huo hapo mwanzo, sasa ameridhika huko Prague. Amepata kile alichokitaka. Umoja wa Ulaya umeamuwa kuweko ibara ndani ya Mkataba wa Lisbon ambayo itaipa upendeleo maalum Jamhuri ya Cheki, ibara ambayo, kiundani na kisheria, haina umuhimu. Hata hivyo, inamridhisha rais huyo wa Cheki ambaye aliutilia guu mkataba huo. Sasa ni juu yake yeye kutimiza sehemu yake wa mapatano, ili mkataba huo upewe idhini ya mwisho. Sakata hili la upinzani dhidi ya Mkataba wa Umoja wa Ulaya lazima likome.

Somo ambalo wakuu wengine wa serekali na nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya wamelipata, kutokana na sakata hili lililoendeshwa huko Cheki, halifurahishi. Inaonesha mtu anashinda ndani ya Umoja wa Ulaya ikiwa anaonesha kichwa ngumu. Anahitaji tu mtu kuwaweka watu wengine roho juu kwa muda mrefu wa kutosha, na baadae anapata kile anachotaka. Vaclav Klaus alijitangaza kama waziri na waziri mkuu, lakini baadae rais huyo aliyechaguliwa chupu chupu alijikuta yuko katika kona. Umoja wa Ulaya umehakikisha ile ibara kwa ajili ya Bwana Klaus, ambayo tangu hapo imo ndani ya Mkataba wa Umoja wa Ulaya, kwamba mkataba huo utashughulikia masuala ya sheria za siku za baadae na sio ya zamani. Kile kinachotajwa kuwa ni hofu ya kwamba watu wenye asili ya Kijerumani waliofukuzwa Cheki wataweza kudai ardhi zao ni jambo ambalo halijakuweko.

Ni kutokana na juhudi ndipo viongozi wa serekali na nchi za Umoja wa Ulaya wamweza kuzizuwia nchi nyingine, kama vile Slovakia na Hungary, kushikilia kuweko kanuni maalum kama hizo kwa ajili yao. Kumridhia Vaclav Klaus kile alichokitaka kunaweza kukawa ni mfano wa hatari katika siku za mbele, pale mikataba mingine ya kimsingi itakapobidi ifanyiwe mashauriano. Kila nchi huenda ikadai ipatiwe bahashishi ya ziyada, ikitoa mfano wa nini alichopewa Vaclav Klaus. Haitowezekana kuufanya Umoja wa Ulaya kuwa na nguvu katika mashauriano, kuongoza mambo na pia kufikia malengo yake pale mtu daima itambidi atilie maanani matakwa maalum ya kila nchi mwanachama.

Kwa hivyo, sasa Mkataba wa Lisbon wa Umoja wa Ulaya utaweza kuanza kufanya kazi hapo Januari Mosi mwakani, pindi mahakama ya katiba ya Jamhuri ya Cheki wiki ijayo haitotoa hukumu itakayosema vingine. Kwamba kesi ilioko mbele ya mahakama hiyo ilichochewa na mwenyewe Rais Klaus, hivyo inachukuliwa sasa hoja zilizotolewa ili kuuwekea kiunzi mkataba huo haziko, kwa vile yeye mwenye Vaclav Klaus ameshapata kile alichotaka.

Mkataba wa Lisbon unataka kuweko nyadhifa mbili za juu katika Umoja wa Ulaya, ambazo bado haiajawezekana kuwapata watu wa kuzijaza.Katika mfumo mgumu wa kuamuwa juu ya jambo hilo baina ya madola makubwa na madogo, madola ya kaskazini, kusini, na yale ya mashariki, yanayofuata siasa za Ki-Conservative na yale yanayofuata siasa za Social Democratic, mataifa yote hayo yamegongana katika kupata mtetezi mmoja. Raia wa Kijerumani hajatajwa tena kwa ajili ya nyadhifa hizo, na kwa nchi kubwa kabisa katika Umoja wa Ulaya jambo hilo sio la sifa. Kwa ajili ya uamuzi wa nani akamate nyadhifa hizo itabidi sasa uitishwe mkutano maalum wa kilele. Hiyo pia inaashiria namna gani ilivvyo vigumu hivi sasa kwa umoja huo wenye nchi wanachama 27 kufikia suluhisho la busara katika wakati uliowekwa. Umoja huo unahitaji kufikia maamuzi mengi kwa msingi wa wingi, na jambo hilo linatarajiwa karibuni litafikiwa kutokana na Mkataba wa Lisbon.

Mwandishi: Bernd Riegert /ZR/Othman Miraji

Mhariri:M.Abdul-Rahman

 • Tarehe 30.10.2009
 • Mwandishi Miraji Othman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/KJan
 • Tarehe 30.10.2009
 • Mwandishi Miraji Othman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/KJan
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com