Kombe la klabu bingwa barani Afrika | Michezo | DW | 09.04.2007
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Michezo

Kombe la klabu bingwa barani Afrika

Katika kinyan'ganyiro cha Kombe la klabu bingwa barani Afrika ,Young Africans ya Tanzania imekiona kilichomtoa kanga manyoya. B.Munich yailaza Hannover 2:1 na Schalke iko bado kileleni mwa Bundesliga.

Schweinsteiger-jogoo la Bayern Munich

Schweinsteiger-jogoo la Bayern Munich

TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo imeitandika mjini Kinshasa FAR Rabat ya Morocco bao 1:0 wakati M amelodi Sundowns ya Afrika Kusini ilimudu suluhu nyumbani mjini Pretoria na mabingwa Al Ahly ya Misri ya mabao 2:2.Nsarawa United ya Nigeria iliikomea Al Hilal ya Sudan mabao 3:0.

Mjini Tunis, Young Africans ya Tanzania ilizabwa mabao 3:0 na sasa yanga inahitaji mabao 4 nyumbani Dar-es-salaam kuzuwia kuambiwa buriyani katika kombe la klabu bingwa barani Afrika.

Duru ya pili itachezwa April 20-22.

Ama katika changamoto za Kombe la shirikisho la dimba la AfrikaATRACO ya Rwanda ilimudu suluhu ya mabao 2:2 na Gafsa ya Tunisia mjini Kigali wakati Benefica Luanda ya Angola ilitamba tena mara hii kwa mabao 3:0 dhidi ya Astres Douala.

Union Douala ya Kamerun ilitoka suluhu bao 1:1 nyumbani na Kwara Utd. Ya Nigeria.Ismailia ya Misri, mabingwa wa zamani wa Kombe hili waliwika kwa mabao 2: kwa 1 la Buffalos ya Zambia.

Timu 8 zilizoshinda katika duru hii zitakumbana na timu zilizopigwa kumbo katika duru ya 3 ya kombe la klabu bingwa barani Afrika kwa mapambano ya duru 2 mwezi ujao .Washindi hugawanywa makundi 2 .Washindi wa kwanza katika kila kundi, wanacheza finali.Mabingwa wa zamani wa kombe hili lililochukua nafasi ya kombe la washindi ni pamoja na Hearts of Oak ya Ghana,FAR Rabat ya Morocco na Etoile du Sahel ya Tunisia.

Katika kinyan’ganyiro cha Bundesliga-ligi ya Ujerumani-timu 4 ziliopo kileleni-Schalke,Bremen,Stuttgart na Bayern Munich –zote zilitoroka na ushindi mwishoni mwa wiki huku mechi 6 tu zikisalia kabla msimu kumalizika.

Mechi 28 zikiwa zimeshachezwa, Schlake 04 imeshakusanya pointi 56 ikifuatwa na Bremen pointi 54.Stuttgart ina pointi 52 na mabingwa Bayern Munich wananyatia nafasi ya 4 wakiwa na pointi 50.

Jumamosi Schalke iliizaba Borussia Mönchengladbach mabao 2:0.Mshambulizi Kevin Kuranyi alimtupia pasi maridadi Gerald Asamoah wa asili ya Ghana nae hakukawia kulifumania lango la Borussia.Assamoah alisema,

“Mambo hayakuwa rahisi kwangu.Nilijaribu kucheza kwa nguvu sana kama niwezavyo n a kwa bahati nzuri niliweza kufunga bao.”

Stuttgart ilitamba mbele ya Hamburg ilipoizaba mabao 4:2.Bremen ikaikomea Nuremberg bao 1:0.Bayern munich mabingwa walitoka nyuma baada ya kukandikwa bao 1 na mwishoe waliondoka na ushindi wa mabao 2:1 na Hannover.Munich ikiania tiketi ya kucheza msimu ujao wa champions League-kombe la klabu bingwa barani Ulaya- ikihitaji ushindi kufa-kupona.Akithibitisha hayo kocha wao Ottmar Hitzfeld alisema:

“Baada ya mpambano mgumu sana wa champions League, tumenyakua leo pointi 3 ,Shabaha imebakia ile ile –kunyakua nafasi ya kucheza msimu ujao katika champions League na kwahivyo ushindi tu leo ndio ungeweza kutusaidia kutimza shabaha hiyo.”

Ama katika Premier League-ligi ya Uingereza ,Manchester United viongozi wa Ligi wamezabwa mabao 2:1 na Portsmouth na mwanya wao wa uongozi kilelelni sasa umepuingwa hadi nusu baada ya mahasimu wao Chelsea kuitandika Tottenham Hotspur bao 1:0.

Huko Itali,AS Roma iliopo nafasi ya pili ya ngazi ya Ligi maandalio yao ya mpambano wao wa kesho na Manchester united kwa duru ya pili yameenda uzuri baada ya kuikandika Catania 2:0.

La Liga huko Spain imegeuka mbio za farasi 3 baada ya Real Madrid iliopo nafasi ya tatu, kuinyemelea Sevilla iliopo nafasi ya pili hadi pointi 1 na pointi FC Barcelona hadi pointi 2.Barcelona ililazwa kwa bao 1:0 na Real Zaragoza hapo jumamosi.