1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kombe la Klabu Bingwa Afrika

13 Septemba 2010

TP Mazembe njiani kuutetea ubingwa ?

https://p.dw.com/p/PB9l
Muukraine Wladimir Klitschko atamba FrankfurtPicha: AP

-Katika Bundesliga,Mainz 05, ilitoka nyuma na kuitundua Kaiserslauten kileleni kwa ushindi wa mabao 2-1.

Hoffenheim, inaongoza Bundesliga baada ya kuipiga kumbo Schalke 04 Ijumaa.

-TP Mazembe, imeingia nusu-finali ya Kombe la klabu bingwa ikijiwinda sasa kutetea taji lake.

-Marekni, imetawazwa mabingwa wa dunia baada ya jana kuwatimua waturuki kwa mabao 81 kwa 64.

Mainz 05: imeparamia nafasi ya pili ya ngazi ya Bundesliga jana baada ya kutoka nyuma na kuizima Kaiserslauten ilioanza Ligi hii kwa vishindo kwa mabao 2:1.Srjan Lakic,alilifumnia lango la Kaiserslauten na kutia bao lake la 4 msimu huu kuipa Kaiserslauten uongozi.

Lakini, kati kati ya kipindi cha pili,Kaiserslauten ilifanya uzembe na Niko Bungert, akasawazisha dakika ya 71 ya mchezo.Andre Schurrle, akaipatia Mainz mwishoe, bao la ushindi.

FC Cologne, pia jana ilitamba nyumbani tangu kupita kipindi kirefu pale mkwaju maridadi wa Lukas Podolski, ulipogonga mwamba wa lango la St.Pauli na kurejea uwanjani.Taner Yalcin, akausindikiza mpira wavuni kwa kichwa.Cologne, ikaondoka na pointi 3 za kwanza msimu huu baada ya kulazwa mapambano 2 yaliopita.

Mabingwa Bayern Munich, walimudu sare tu ya 0:0 nyumbani dhidi ya mahasimu wao wakubwa Werder Bremen.Hivyo, Munich, ilishindwa kutoa zawadi ya miaka 65 ya kuzaliwa kwa stadi wao mkubwa Franz Beckenbauer.

Philipp Lahm,mlinzi wao alieleza hivi jinsi mchezo ulivyokwenda:

" Kutoka sare 0:0 jakuridhishi.Na katika mapambano 3 ukiondokea na pointi 3 sivyo kabisa tulivyotarajia.Makosa mengi yamefanyika ambayo hayangefaa kufanyika."

Alisema Philip Lahm.

Tayari Ijumaa usiku Hoffenheim , ilifunza darasa la dimba Schalke 04,makamo-bingwa wa Ujerumani.Hilo likawa pigo la 3 kwa Schalke tangu kuanza msimu huu .Baadae kocha wao Felix Magath,alieitawaza mwaka juzi Wolfsburg mabingwa wa Bundeliga alisema:

"Yafaa kupongeza kwamba, tuliweza kuwapa changamoto kali kwa viongozi hao wa Ligi na hta kuonesha mchezo mzuri." Alijitapa hivyo Magath ingawa pointi 3 ameziacha Hoffenheim.

Katika kinyan'ganyiro cha Kombe la klabu bingwa barani Afrika,mabingwa TP mazembe ya Jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo na mabingwa mara 6 wa kombe hilo Al-Ahly ya misri wameingia nusu-finali ya kombe hilo wakati katika kombe la Shirikisho-CAF-Confederations Cup,Zanaco ya zambia imejitosa katika duru ijayo baada ya kuilaza CS Sfaxien ya tunisia bao 1:0.

TP Mazembe ilizima vishindo vya Dynamo ya Zimbabwe mjini Lumbubashi na mwishoe iliondoka na ushindi wa mabao 2:1 .Al Ahly, mabingwa mara 6 wa kombe hilo waliondoka na ushindi sawa na huo wa 2-1 dhidi ya makamo-bingwa wa mwaka jana Heartland ya Nigeria,mjini Cairo.

Kwahivyo, TP Mazembe na Al Ahly, wanajiunga na JS Kabylie ya Algeria inayohanikiza hivi sasa pamoja na Esperance ya Tunisia, mwezi ujao .Mshindi wa taji hili ataondoka na kitita kinono cha dala milioni 1.5.

Yeyote atakaetorka na taji kufuatia finali ya duru 2 nyumbani na ugenini, ndie atakaewakilisha Afrika katika Kombe la dunia la klabu bingwa. mjini Lumbubashi, Mazembe ilishindwa kutumia nguvu zake kimchezo kugeuza mabao dhidi ya adui ambao walipungukiwa na wachezaji wao 7 bora.Kabylie ilitoroka na ushindi wa bao 1:0 ukiwa 4 pale mnigeria,Azuka alipolifumania lango la Ismailia ya Misri huko Tizi-Ouzou,Algeria.

Ama katika changamoto za kombe la Shirikisho la dimba la Afrika-Confederation Cup,Zanaco ya zambia mwishoe imefaulu kuingia duru ya pili ya makundi kwa kuwatia munda viongozi CS Sfaxien ya tunisia bao 1:0 nyumbani Lusaka,Zambia.

Mchezaji wao wa kiungo Winston Kalengo aliipatia Zanaco bao hilo la ushindi.Hatahivyo, Sfaxien inaongoza kwa tofauti ya mabao katika kundi hili B.

Ama katika kundi A,FUS Rabat ya Morocco iliondoka na ushindi wa bao 1:0 dhidi ya Harras al-Hodoud ya Misri.Lakini, ASFAN ya Niger haikuwa na bahati kama wenzao kwani walikiona cha mtema kuni mbele ya Al-Ittihad ya libya mjini Tripoli.

Al Hilal ya Sudan, ikiania taji lake la kwanza la kombe la Afrika , baada ya mara 2 kuibuka makamo-bingwa, ndio wanaoongoza kwa kunyakua pointi zote hadi sasa.Baada ya duru 3,Al Hilal, inaendelea kutamba kwa kuitoa Djoliba kwa mabao 2.1.

Mashindano ya mpira wa kikapu ya ubingwa wa dunia (Basketball-world championship" yalimalizika jana kwa ushindi wa Marekani dhidi ya Uturuki.

Marekani ilikusanya mabao 81 kwa 64 ya Uturuki.Nafasi ya 3 ilikuja Lithuania ilioitoa Serbia kwa mabao 99 kwa 88.

Na katika ringi ya mabondia,mbabe wa wezani wa juu ulimwenguni mwenye kuhodhi mataji 3 muukraine mwenye kambi yake Ujerumani Wladmir Klitscko alimdengua mnigeria Samuel Peter mnamo duru ya 10 ya changamoto yao ya duru 12.

Mwandishi:Ramadhan Ali/ rtr,afp,dpa

Mpitiaji:Mohammed Abdul-Rahman