Kombe la Cecafa: Zanzibar 2-Sudan 2 | Michezo | DW | 10.12.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Michezo

Kombe la Cecafa: Zanzibar 2-Sudan 2

Katika kombe la challenge cup la kanda ya Afrika mashariki na kati,Zanzibar imewasangaza mabingwa watetezi Sudan kwa 2:2.

default

Bayer Leverkusen

Zanzibar Heroes yazusha msangao katika kombe la Cecafa-kombe la Afrika mashariki na kati kwa kutoka suluhu mabao 2:2 na mabingwa Sudan wakati Taifa Stars (Tanzania) wenyeji wafungua dimba kwa kunguruma mabao 2:1 mbele ya Kenya “Harambee Stars”.

Bayern munich,wameteleza nyumbani katika Bundesliga baada ya kupoteza pointi kwa Duisburg na katika Premier League-Ligi ya uingereza, Arsenal yapata pigo lake la kwanza msimu huu kutoka kwa Middlesbrough.

Tukianza na ligi mashuhuri barani Ulaya,Bayer Leverkusen ilitamba jana kwa mara ya 5 mfululizo walipoizaba Hansa Rostock mabao 3-0 katika BayArena.

Matokeo hayo yameipeperusha Leverkusen katika nafasi ya 4 ya ngazi ya Bundesliga.Viongozi wa Ligi-Bayern Munich,walitoka tupu na kuacha uwanjani pointi 3 waliozihitaji kupanua zaidi mwanya wao kileleni.Munich ikicheza nyumbani Allianz Arena mjini Munich ilimudu suluhu tu 0:0 na chipukizi Duisburg iliopanda msimu huu daraja ya kwanza.

Kocha wa Bayern Munich Ottmar Hitzfeld,akisikitishwa na jinsi timu yake ilivyopoteza nafasi za kutia mabao na kuondoka na ushindi alisema: “Bila shaka yavunja moyo ikiwa unacheza nyumbani na timu kama Duisburg na huondoki na pointi 3. Hii inatokana na kwamba hatukutumia nafasi tuliopata na hasa mnamo dakika 10 za kwanza”.

Ikiwa kumesalia mpambano 1 tu kabla ya bundesliga kwenda likizo ya x-masi na mwaka mpya, Munich hatahivyo, inaongoza kileleni ikiwa na jumla ya pointi 35,huku Werder Bremen ikiwa nyuma kwa pointi 2 na pointi 33.Brem,en nayo iliteleza jumamosi ilipochapwa mabao 4-3 na Hannover 96.Hamburg inayonyatia nafasi ya 3 ilimudu sare pia 0:0 kati yake na Energie Cottbus.

Ama katika premier League ,viongozi wa Ligi Arsenal jana walionjeshwa shubiri walipozabwa mabao 2-1 na Mioddlesbrough .Kwa pigo hilo la jana, mwanya wa Arsenal kileleni mwa premier League,umepungua hadi pointi 1.

Katika mapambano mengine,Bolton wamezusha maafa zaidi kwa Wigankwa kuwatimua nje kwa mabao 3-1 huku Tottenham,ikinyakua ushindi wake 3 msimu huu ilipoibwaga chini Manchester City kwa mabao 2-1.

Zambia imemuita tena kujiunga na kikosi cha Taifa-Chipolopolo-stadi wake wa Bundesliga na nahodha wake wa zamani Moses Sichone.Sichone anaichezea sasa Kickers Offenbach –klabu ya daraja ya pili ya Bundesliga.Sichone ameitwa kujiunga na kikosi cha wachezaji 28 cha Zambia kwa kombe lijalo la afrika la mataifa nchini Ghana mwezi ujao.

Zambia katika kombe hilo la Afrika la mataifa imeangukia kundi moja na mabingwa Misri,mabingwa mara 4-simba wa nyika Kamerun na mabingwa wa Cecafa Sudan, ambao mwishoni mwa wiki walitolewa jasho na Zanzibar heroes katika kinyan’ganyiro cha kombe la Challenge cup-kombe la Afrika mashariki na kati.Kwani, chipukizi hao wa Zanzibar walimudu kwa msangao wa wengi suluhu ya mabao 2:2 na mabingwa hao watetezi-Sudan –timu pekee katika kanda hiyo inayocheza mwezi ujao katika Kombe la Afrika la mataifa nchini Ghana.

Taifa Stars-Tanzania bara ilifungua dimba mjini Dar-es-salaam kwa kuilaza Kenya mabao 2:1.ilikua Kenya lakini iliotangulia kutia bao la penalty kabla Tanzania kusawazisha.

Uganda ilijaza kikapu cha Djibouti kwa mabao 7:0-ushindi mkuu hadi sasa katika kombe hili la Challenge cup.

Kuaibika kwa aliekua malkia wa mbio fupi wa Marekani-Marion Jones kunakamilishwa wiki hii pale kamati tendaji ya halmashauri kuu ya olimpik ulimwenguni (IOC) itakapokutana mjini Lausanne, uswisi na kuzifuta katika vitabu vyake vya rekodi medali zote 5 alizoshinda katika michezo ya Olimpik ya Sydney, 2000.

Jones, aliungama karibuni kutumia madawa ya kutunisha misuli kuongeza kasi.Na kama Ben Johnson wa Kanada,kabla yake, malkia huyu amebidi nae kuadhibiwa kwa madhambi yake.

 • Tarehe 10.12.2007
 • Mwandishi Ramadhan Ali
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CZmE
 • Tarehe 10.12.2007
 • Mwandishi Ramadhan Ali
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CZmE