1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kombe la Afrika laanza Accra l

Ramadhan Ali18 Januari 2008

firimbi inalia jumapili hii kuanzisha kombe la 26 la Afrika la mataifa.Je, nani ataivua taji Misri ?Wenyeji Ghana au tembo wa I.Coast

https://p.dw.com/p/CuOZ

Kesho asie na mwana aeleke jiwe na asie na mguu atie gongo-mkutano uwanjani Accra,kwani kombe la 26 la Afrika la mataifa linaanza kwa wenyeji „Black Stars“-Ghana wakifungua dimba na jirani zao Guinea.

Mitaa na njia za jiji la Accra imepambwa kwa bendera za timu zote 16 zinazoshiriki na wauza maduka tayari wameanza biashara zao kuanzia uuzaji jazi za mastadi kama Michael Essien-jogoo la nyumbani hata Didier Drogba-nahodha wa Ivory Coast na za mshambulizi wa Kameroun,Samuel Eto’o. Nao akina „mama ntilie“ tayari wanauza ugari wao mitaani.

Mabingwa Misri, mpambano wao wa kwanza utakua na simba wa nyika Kamerou porini.Kuna simba wa Teranga-simba wa Senegal waliotia fora katika kombe la dunia 2002 wakicheza tena na Al Hadj Doiuf.Wao wanadai pia huu ni mwaka wao kuvaa taji la Afrika.

Finali ya kombe la Afrika kuanzia kesho jumapili hadi Februari 10, yaonesha itachezwa katika viwanja 3 tofauti:kimoja cha timu 2,kingine cha wachawi wao vichakani na kingine katika qasri za marais na wafalme wa timu zote 16.Kwani ,rais Abddoulaye Wade wa Senegal ameshapiga firimbi ya kwanza:Ameiamrisha ndege yake ya rais kuwapakia mashabiki wa Senegal hadi Ghana na kurudi na kombe februari 10.

Nikiwafunulia kawa, hili ni kombe la 26 nchini Ghana tangu lile la awali kabisa 1957 mjini Khartoum,liliozishirikisha timu 3 tu-mabingwa wa sasa Misri, Ethiopia na wenyeji Sudan.Sudan inarudi mara hii katika finali hizi baada ya kitambo cha miaka 32.

Mechi ya ufunguzi kesho jioni na ile ya finali zitachezwa katika uwanja wa Ohene Djan Stadium,mjini Accra.

Hii ni mara ya 4 kwa Ghana kuwa mwenyeji wa kombe la Afrika la Mataifa na linafanyika mwaka tangu Ghana kuadhimisha kwa shangwe na shamra shamra miaka 50 tangu uhuru 1957 –mwaka lilipoanzishwa kombe la Afrika.

Ghana ililiandaa kombe hili kwanza 1963,halafu tena 1978 na tena 2000.Mara ya mwisho waliandaa kwa ubia na majirani na mahasimu wao Nigeria.

Kombe la Afrika kwa desturi linachezwa kila baada ya miaka 2 na kombe lijalo baada ya hili Ghana,litakua Angola,2010 mwaka wa kombe la dunia –la kwanza barani Afrika katika nchi jirani ya Afrika Kusini.

Baada ya Angola 2010,itakua zamu ya guinea ya Ekweta 2012 na baadae Libya 2014.

Mabingwa watetezi-mafiraouni wa Misri wametwaa kombe hili mara 5 –nayo ni rekodi,lakini wenyeji Ghana na simba wa nyika-Kameroun wamepania kusawazisha rtekodi yao mara hii nchini Ghana.

Rekodi nyengine ambayo Ghana na Kameroun ziko mbali kuifikia ni ile kuwa Misri imeshiriki mara 21 katika finali za Kombe hili la Afrika. Isitoshe, ndio ilioweka pia rekodi ya kucheza mechi nyingi kabisa katika finali za Kombe la Afrika (X 77).

Rekodi nyengine ya mafiraouni ndio timu ilioshinda mechi nyingi kabisa juma ni 40 na ndio iliotia magoli mengi kabisa :121.Kutwaa kombe lililopita lakini bao 1 zaidi kuliko Tembo wa Ivory Coast,lilitosha kulibakisha kombe Cairo,nyumbani mwa CAF-shirikisho la dimba la Afrika.

Timu 13 kati ya zile zilizowahi kutawazwa mabingwa wa Afrika zinashiriki mara hii.Hakuna hata timu moja kati ya zote 16 zinazocheza mara hii nchini Ghana,haikuwahi kucheza finali za kombe hili.Kwahivyo, wote ni wenyeji.Kwa timu 2 lakini-Namibia na Benin hii itakua mara yao yapili.

Sudan inarudi mashindanoni kwa mara ya kwanza tangu 1974.Wakiwa waasisi wa kombe hili,Sudan walilitwaa 1970.

Kuanzia kesho Ghana inawatembeza mastzadi wakubwa wa dimba wa Afrika waliohanikiza dunia nzima:akina Michael Essien na Didier Drogba wa Chelsea na Samuel Eto’o wa Kameroun.

Na Kombe litaelekea wapi Februari 10 ? W wanasema, „Usikate kanzu kabla mtoto kuzaliwa.“

Kombe la 26 linaloanza kesho Accra kwa changamoto kati ya Ghana na Guinea mwishoe, litanyakuliwa na timu gani ? hapo maoni ya mashabiki yanatofautiana.

„tembo wa Ivory Coast“ watatoroka na kombe la 2008 la afrika alisema mzungu pekee alietawazwa bingwa wa kombe hilo kama nahodha wa Bafana bafana ilipotamba nyumbani 1996 mbele ya Madiba - Neil Tovey.

Nahodha huyo wa zamani aliekabidhiwa kombe na mzee Mandela,1996 baada ya Afrika kuisini kuilaza Tunisia katika finali mjini Johannesberg, anabashiri kwamba Ghana,Morocco,Ivory Coast,Nigeria na Kameroun,Misri,Senegal na Bafana Bafana-Afrika Kusini,zitakata tiketi ya duru ya pili-ya robo-finali.

Tovey anaamini kwamba Didier Drogba atawatia shime Tembo wa Corte d’Iviore kutamba mbele ya morocco na hata Kameroun katika duru 2 ya kutoana na baadae Tembo watawameza Super Eagles-Tai wa Nigeria katika finali Februari 10.

Tovey alisema, „ naiangalia Ivory Coast kuwa ndio timu bora kabisa ya taifa barani afrika wakati huu na kumpoterza kocha mjeru mani uli Stielike kunaweza kukachangia mambo kuwaendea vyema .“

Beki huyo wa zamani wa Ujerumani –kocha wa Ivory Coast alilazimika kurudi nyumbani wiki 2 kabla kuanza kombe hili baada ya mwanwe wa kiume kuzimia .Hivyo, nafasi yake imechukuliwa na mfaransa Gerard Gili aliekwishaikatia Ivory Coast tiketi ya Beijing ya dimba la olimpik.

Kwahivyo, anasema nahodha huyo wa zamani wa Bafana Bafana, Tembo watajiwinda kutamba zaidi kuonesha heshima zao kwa kocha waop mjerumani uli Stielieke.

Tovey, ameitaja Angola kuwa ni timu inayoweza kuzusha msangao katika kombe hili.mimi ningeongeza nakusema hata Mali.

Na vipi timu yake ya Afrika Kusini, mwenyeji wa kombe lijalo la dunia 2010 ?

Bafana Bafana inaongozwa na kocha Mbrazil Carlos Parreira,ambae alianza kazi yake ukocha akiwa bado chipukizi huko huko Ghana. Wakati ule alipotumwa ghana na shirikisho la dimba la Brazil kinyume na hii leo, Parreira alilipwa posho ya dala 100 tu anasema.hatahivyo, alifurahia kuwa kocha wa Black Stars na hata Asante Kotoko. Anafurahia kwahivyo, kurudi ghana akiwa kocha wa Afrika Kusini kwa kitita mkikubwa zaidi.Parreira ameshaweka wazi baada ya kombe la dunia na afrika kusini,atastaafu-hicho ni kituo chake cha mwisho kabla kurudi Brazil,alioitawaza mabingwa wa dunia 1994 nchini Marekani.

Wachambuzi wanadai kwamba Parreira anakwenda ghana kuwanoa akina Piener na zuma pamoja na chipukizi wengine kwa kombe lijalo la dunia 2010. Si zaidi.

Hofu za Tovey, ni kwamba finali ya kombe hili Februari 10,isije nayo ikaamuliwa k

Na nini matumaini ya wenyeji-Ghana ?

Nahodha wao wa zamani Abedi Pele anaipigia upatu nchi yake Ghana kulitwaa kombe.Pele anaamini kwamba Black Stars itavumilia kumpoteza nahodha wao Stephen appiah alieumia na kuweza kusawazisha rekodi ya Misri ya kutwaa kombe kwa mara ya 5.Abedi pele anadai, „Ghana inacheza nyumbani na mcheza kwao hutunzwa.Anadai kumkosa Appiah kutafidiwa na akina Michael essien,Laryea Kingston na sulley Muntari-wachezaji bora kabisa wsa kiungo wakati huu. Abedi Pele anaungama hata hivyo, kwamba mahasimu wakubwa wa Ghana watatoka kundi B-nao ni tembo wa Ivory Coast na hata Nigeria .Pele binafsi alitawazwa mabingwa wa afrika,1982 pale alipoichezea ghana huko Libya akiwa na umri wa miaka 17 tu-sawa na vile Pele wa Brazil alipoichezea kwa mara ya kwanza Brazil huko Sweden, 1958 akiwa na umri wa miaka 17.

Akiulizwa ni stadi gani ataibuka „jogoo la kombe hili“ ?

Nahodha huyo wa Afrika kusini katika kombe la Afrika 1996, alisema:Salomon kalou wa Ivory Coast,kwavile atanufaika kwa kucheza ubavuni mwa stadi wao Didier drogba-mchezaji bora wa mwaka wa Afrika. Akaonya kwamba Benin,Nigeria na mali-mahasimu wa Corte d’Iviore katika kundi hili watamkodolea macho mno Didier Drogba mshambulizi hatari mno anaeogopwa wakati huu kutoka Afrika.

Iliobaki sasa tusiandike mate na wino upo.Ghana na Guinea zafungua dimba kesho na itatuchukua siku 20 hadi februari 10 kujua nani mabingwa wapya na nani mabingwa wa zamani wa Afrika.

Ulimwengu mzima wake kwa waume wsakubwa kwa wadogo wanakodoa macho na kutega masdikio Ghana-Brazil ya Afrika.

Usiache kuwa nasi siku zote hadi Februari 10 tukilisindikiza kwa pamoja nyumbani kombe la 26 la Afrika.