Kiongozi wa kijeshi Mauritania ajiuzulu | Matukio ya Kisiasa | DW | 16.04.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Kiongozi wa kijeshi Mauritania ajiuzulu

Nia ni kutaka kugombea urais

Mohamed Ould Abdel Aziz akihutubia baada ya mapinduzi Agosti mwaka jana

Mohamed Ould Abdel Aziz akihutubia baada ya mapinduzi Agosti mwaka jana

Kiongozi wa jopo linalotawala Mauritania tangu mapinduzi ya kijeshi ya Agosti mwaka jana, Jenerali Mohammed Ould Abdel Aziz amesema anajiuzulu ili kupigania kiti cha rais uchaguzi utakapoitishwa June sita mwaka huu.

Alikua yeye mwenyewe Ould Abdel Aziz aliyeongoza mapinduzi hayo miezi minane iliyopita na kuutimua madarakani utawala wa Sidi Ould Cheikh Abdallahi,rais wa kwanza aliyechaguliwa kwa njia za kidemokrasi,mwaka 2007 nchini Mauritania.

Nimeamua kujiuzulu wadhifa wangu wa mwenyekiti wa baraza kuu la taifa na kiongozi wa taifa kuambatana na sheria na kufuata kanuni ziliozoko" amesema hayo Ould Abdel Aziz katika hotuba yake iliyotangazwa na radio na televisheni ,usiku wa jana kuamkia leo.

Mwanajeshi huyo aliyesomea,mwenye umri wa miaka 52,aliyetumikia jeshi kwa muda wa miaka 32 ya maisha yake,amebainisha anataka kutetea wadhifa wa rais uchaguzi utakapoitishwa kabla ya wakati June sita mwaka huu.

Ili kuweza kupigania wadhifa huo,analazimika kujiuzulu kama mwanajeshi na kuachana pia na madaraka aliyo nayo siku 45 kabla ya uchaguzi huo kuitishwa.

Jenerali Mohammed Ould Abdel Aziz amesema "ana hamu ya kweli ya kujenga Mauritania mpya itakayofuata misingi ya sheria,usawa na uhuru".Amezungumzia pia maendeleo yaliyoweza kufikiwa nchini tangu alipotwaa madaraka Agosti mwaka jana.

Amewakosoa kwa mara nyengine tena wapinzani wake wa kisiasa,anaowataja kua "kundi la wahalifu" na kuwatuhumu kutaka kusababisha njaa kwa "kuiwekea vikwazo nchi yake."

Chama cha "Muungano wa taifa wa kuhifadhi Democrasia-FNDD kimeutaja uamuzi wa jenerali huyo aliyeamua kuvaa suti badala ya sare za kijeshi kua ni "kiini macho tuu kilicholengwa kuwahadaa walimwengu na kuhalalisha mapinduzi yake ya kijeshi."

FNDD na vyama vyingi vyengine vya upinzani vinapanga kuususia uchaguzi huo wa rais.

Wapinzani wa jenerali Mohammed Ould Abdel Aziz wanamlaumu kwa kutumia mali ya taifa tangu miezi kadhaa iliyopita kuendesha kampeni yake ya uchaguzi kote nchini na kuzifunga njia zote za kupigania wadhifa huo wa rais.

Kabla ya hotuba yake ya jana usiku,Ould Abdel Aziz alikutana na mwenyekiti wa baraza la Senet,Ba Mamadou,aliyeteuliwa kua "rais wa mpito" na baraza la katiba.

Mwandishi Hamidou Oummilkheir

Mhariri Abubakar Liongo
 • Tarehe 16.04.2009
 • Mwandishi Oumilkher Hamidou
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/HYBg
 • Tarehe 16.04.2009
 • Mwandishi Oumilkher Hamidou
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/HYBg
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com