Katibu Mkuu mpya wa NATO aelezea malengo yake | Matukio ya Kisiasa | DW | 03.08.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Katibu Mkuu mpya wa NATO aelezea malengo yake

Rasmussen amesema NATO itaishawishi Urusi kuwa jumuiya hiyo siyo adui wa nchi hiyo.

default

Katibu Mkuu mpya wa NATO, Anders Fogh Rasmussen.

Katibu Mkuu mpya wa Jumuia ya NATO, Anders Fogh Rasmussen amesema kuwa jumuia hiyo haina budi kuishawishi Urusi kuwa muungano wa jeshi la NATO, siyo adui wa nchi hiyo. Kauli hiyo ameitoa hii leo wakati akizungumza kwa mara ya kwanza na waandishi habari, tangu achukue rasmi madaraka ya ukatibu mkuu wa NATO.

Akizungumza mjini Brussels, Rasmussen, amesema kuwa anataka kuona maendeleo ya ushirikiano imara na wa kweli wakati wa uongozi wake wa miaka minne. Amesema anaamini kuwa uhusiano katika maeneo ambako wanashirikiana masuala ya kiusalama, utaimarika.

Rasmussen amesema kuwa changamoto zinazomkabili wakati wa uongozi wake ni pamoja na ugaidi, hali ya usalama ya Afghanistan, vitendo vya uharamia pamoja na kuhusu mkataba wa kuzuia uenezaji wa silaha za nyuklia. Ameongeza kuwa kipaumbele chake cha kwanza itakuwa ni kuhusu vita nchini Afghanistan. Zaidi Rasmussen anaeleza:

''Ninaamini kuwa wakati wa uongozi wangu kama Katibu Mkuu wa NATO, Waafghanistan lazima waongoze jukumu la usalama katika maeneo mengi ya nchi yao. NATO lazima na itakuwa hapo kwa kuwaunga mkono watu wa Afghanistan kwa chochote kile. Ngoja nirudie hapo: kwa chochote kile.''

Aidha, Rasmussen amesema kuwa anaichukulia changamoto nyingine ya kuwashawishi watu wa Urusi na uongozi wa kisiasa wa Urusi kuwa NATO siyo adui wa Urusi na kwamba NATO haiongozwi kwa ajili ya kuipinga Urusi.

Uhusiano baina ya Urusi na NATO uliharibika kutokana na vita baina ya Urusi na Georgia mwa mwezi Agosti, mwaka uliopita, ingawa pande hizo mbili mwezi Juni, mwaka huu zilikubaliana kurejesha uhusiano wa kisiasa na kijeshi.

Katibu Mkuu huyo mpya wa NATO amebainisha kuwa lengo lake jingine ni kuimarisha uhusiano na nchi za Mediterranean na Mashariki ya kati, hasa nchi za Kiislamu. Anasema:

''Ushirikiano mwingine utakaokuwa na kipaumbele kwangu pia ni uhusiano baina ya NATO na majadiliano ya Mediterranean na ushirikiano wa nchi za Istanbul. Ngoja nizihakikishie serikali na watu wa nchi 11 za Jumuiya ya Mdahalo wa nchi za Mediterranean na kongamano la ushirikiano la Istanbul kuwa ninataka kabisa kujenga uhusiano imara katika misingi ya heshima, maelewano na kukabiliana na changamoto kama vile ugaidi, mkataba wa kuzuia uenezaji wa silaha za nyuklia na hatari za mataifa yaliyoshindwa.''

Rasmussen ambaye alikuwa Waziri Mkuu wa Denmark mwaka 2005 wakati wa mfululizo wa uchoraji wa vikaragosi katika gazeti la Copenhagen zilizomlenga Mtume Mohammed na kuibua hisia tofauti katika jamii ya Kiislamu, tayari amezialika nchi za Algeria, Bahrain, Misri, Israel, Jordan, Kuwait, Mauritania, Morocco, Qatar, Tunisia na nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu kufanya mazungumzo yatakayolenga uhusiano wa baadaye baina ya NATO na nchi hizo katika masuala ya usalama hasa makundi mawili yanayojulikana kama Jumuiya ya Mdahalo wa nchi za Mediterranean na Kongamano la Ushirikiano la Istanbul.

Rasmussen amethibitisha pia kuwa amemteua Waziri wa zamani wa Mambo ya Kigeni wa Marekani, Madelein Albright kuongoza kundi la wataalamu wa kisiasa na kidiplomasia kuzungumzia mikakati mipya ya usalama ya NATO ili kuongoza mipangilio katika karne ijayo. Katika yote hayo, Katibu Mkuu mpya wa NATO, amesema ziara zake za kwanza za kidiplomasia zitakuwa nchini Uturuki na Ugiriki, ambayo mzozo wake kuhusu Cyprus umesababisha kuwepo kwa uhusiano mbaya baina ya NATO na Umoja wa Ulaya.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (DPAE/AFPE)

Mhariri: M. Abdul-Rahman

 • Tarehe 03.08.2009
 • Mwandishi Kabogo Grace Patricia
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/J2q8
 • Tarehe 03.08.2009
 • Mwandishi Kabogo Grace Patricia
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/J2q8

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com