KARACHI:Benazir Bhutto ashtumu vikali shambulio la bomu lililolenga msafara wake | Habari za Ulimwengu | DW | 19.10.2007
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Habari za Ulimwengu

KARACHI:Benazir Bhutto ashtumu vikali shambulio la bomu lililolenga msafara wake

Waziri Mkuu wa zamani wa Pakistan Bi Benazir Bhutto anashtumu vikali shambulio la bomu la hapo jana punde baada ya kuwasili mjini Karachi.Shambulio lililenga msafara wake na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 130.Kulingana na kiongozi huyo wafuasi wake wamejitoa muhanga kulinda demokrasia

''Tunataka kujiepusha na umwagikaji damu…na vifo ila nataka kusema kuwa ikiwa italazimika kutoa muhanga maisha yetu ili kuokoa demokrasia tunayoamini itaokoa taifa la Pakistan basi tuko tayari kufanya hilo.Ila hatuko tayari kuruhusu nchi yetu kushambuliwa na wapiganaji wanaotaka kuyumbisha nchi yetu.''

Viongozi kote ulimwenguni wanakashifu shambulio hilo la kujitoa muhanga lililomlenga Bi Bhutto na kueleza kuwa linaashiria umuhimu wa ushirikiano wa pamoja wa dharura ili kupambana na ugaidi. Marekani iliyo mwandani wa Pakistan katika vita dhidi ya ugaidi inasema kuwa shambulio hilo sharti lisiruhusiwe kuathiri uchaguzi ujao unaopangwa kufanyika mwanzoni mwa mwaka ujao.Mataifa jirani ya India na Uchina aidha Umoja wa Matifa na Ulaya pia wanashtumu vikali shambulio hilo.Bi Bhutto alirejea nchini mwake Pakistan na kuahidi kuongoza chama chake cha PPP kushiriki katika uchaguzi ujao baada ya Rais Pervez Musharraf kuruhusu mahakama kumfutia mashtaka ya rushwa yaliyomkabili.

India na Pakistan zinatarajiwa kufanya mazungumzo jumatatu ijayo kujadilia juhudi za kupambana na ugaidi yakiwemo maelezo ya kijasusi kuhusu wanamgambo.Rais Hamid Karzai wa taifa jirani la Afghanistan anasema kuwa shambulio hilo dhidi ya ndugu zao wa Pakistan linaonyesha umuhimu wa ushirikiano katika mapambano dhidi ya ugaidi.

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com