1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Joto kali lasababisha maafa ya moto kwenye nchi kadhaa Ulaya

Zainab Aziz
25 Julai 2023

Ndege ya wazima moto imeanguka kusini mwa Ugiriki wakati ambapo mamlaka za nchi hiyo zinapambana na majanga ya moto kote nchini humo Uturuki, Algeria na Tunisia nazo zinakabiliwa na matukio ya moto mkali

https://p.dw.com/p/4UNP7
Griechenland I Waldbrände auf Rhodos
Picha: Aristidis Vafeiadakis//ZUMAPRESS.com/picture alliance

Ajali hiyo imetokea katika kisiwa cha Evia, na ilitangazwa katika televisheni ya taifa iliyoonesha ndege hiyo ikiruka kwa umbali wa chini kabisa na ikatumbukia kwenye korongo na muda mfupi baadaye moto mkubwa ulionekana ukiwaka. Jeshi la wanahewa la Ugiriki limesema kulikuwa na wanajeshi wawili ndani ya ndege hiyo aina ya amphibious Canadair CL-215 wakati ilipoanguka.

Ndege ya wazima Moto iliyoanguka kusini mwa Ugiriki.
Ndege ya wazima Moto iliyoanguka kusini mwa Ugiriki.Picha: Spyros Bakalis/AFP

Wimbi la tatu la joto kali nchini Ugiriki limesababisha viwango vya joto kupanda na kupindukia nyuzi joto 40 katika baadhi ya maeneo nchini humo. Shughuli za uokoaji zinaendelea huku mioto hiyo kwa siku kadhaa ikishindikana kuidhibiti. Waziri Mkuu wa Ugiriki, Kyriakos Mitsotakis amesema nchi yake imo vitani na kwamba serikali yake itaendelea kuwa katika hali ya tahadhari.

Makao makuu ya zima moto mjini Athens imesema hatari ya moto ni kubwa karibu katika kila mkoa nchini Ugiriki. Wakati huo huo wazima moto kutoka nchi 11 za Ulaya wamejumuika na wenzao wa Ugiriki katika juhudi za kuzima moto kwenye maeneo tofauti ya nchi hiyo.

Waziri Mkuu wa Ugiriki Kyriakos Mitsotakis
Waziri Mkuu wa Ugiriki Kyriakos Mitsotakis Picha: Louiza Vradi/REUTERS

Je! ni wapi pengine panateketea moto duniani kutokana na joto kali lililoikumba dunia linalosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi? Huko nchini Uturuki maafisa wazima moto wanapambana na moto unaosambaa karibu na eneo la mapumziko kwenye mji wa Kemer uliyo kusini mwa jimbo la Antalya huku eneo hilo likikabiliwa na joto kali mno. Upepo mkali ulisababisha moto huo kusambaa kwa kasi hadi msituni kwa mujibu wa taarifa ya gavana wa Antalya Ersin Yazici.

Waziri wa Utalii wa Uturuki Mehmet Nuri Ersoy, amewaambia waandishi wa habari kwamba ndege kumi, helikopta 22 na magari ya kuzima moto zaidi ya 200 yamepelekwa katika juhudi za kuuzima moto huo unaowaka kwenye baadhi ya sehemu za mji wa Kemer na takriban hekta 120 za msitu zimeteketea.

Uturuki pia yapambana na majanga ya moto kutokana na joto kali.
Uturuki pia yapambana na majanga ya moto kutokana na joto kali.Picha: MEHMET CIL/DHA

Moto mkubwa pia unawaka kwenye pwani ya Algeria, moto huo umeenea hadi nchi Jirani ya Tunisia ambako viwango vya nyuzi joto 49 vimeorodheshwa katika baadhi ya miji mnamo wiki hii. Algeria inapambana na moto mkali unaowaka msituni kwenye pwani ya Mediterania.

Mamlaka imesema watu 34 wamekufa kutokana na maafa hayo ya moto na kwamba hadi sasa wazima moto wamefaulu kudhibiti thuluthi moja ya eneo linaloungua. Watu 1,500 wamehamishwa kutoka kwenye makazi yao. mamlaka imesema moto huo ulichochewa na upepo mkali uliotokea nchi jirani ya Tunisia, hali iliyolazimisha mipaka kufungwa kati ya nchi mbili hizo.

Maafa ya moto katika eneo la El Kala mkoani Taref nchini Algeria.
Maafa ya moto katika eneo la El Kala mkoani Taref nchini Algeria.Picha: Ramzi Boudina/REUTERS

Wimbi la joto limesababisha maafa katika sayari nzima ndani ya mwezi huu wa Julai, na joto lililovunja rekodi limeorodheshwa katika nchi za China, Marekani, kusini mwa Ulaya na Afrika Kaskazini. Joto kali pia limesababisha uharibifu mkubwa.

Nchini Ujerumani kampuni za safari zimewarejesha nyumbani maelfu ya watu waliokuwa wanafanya likizo katika maeneo mbalimbali yanayokumbwa na balaa la moto kwa sasa.

Vyanzo:AFP/DPA/AP/RTRE