1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Je siasa za mrengo wa kulia Ulaya zinabadilika?

20 Machi 2026

Vyama vya siasa za wastani za mrengo wa kulia vinazidi kuonekana vikishirikiana na vile vya siasa kali za mrengo wa kulia katika bunge la Ulaya. Hili linaonesha siasa za Ulaya huenda zinaelekea kwenye mageuzi muhimu.

https://p.dw.com/p/5AlGx
Ufaransa Strasbourg 2026 | Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Annalena Baerbock akizungumza katika Bunge la Umoja wa Ulaya
Vyama vya siasa za wastani za mrengo wa kulia Ulaya vinazidi kuonekana vikishirikiana na vile vya siasa kali za mrengo wa kulia katika bunge la Ulaya.Picha: Frederick Florin/AFP/Getty Images

Katika siasa za nchini Ujerumani kuna sheria iliyo wazi kabisa ambayo inakataza kuweko ushirikiano na chama cha siasa kali za mrengo wa kulia. Kile kinachoitwa kwa lugha ya kijerumani ''Brandmauer'' yaani ukuta wa kuzuia mashirikiano ya aina yoyote serikalini na chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha AfD.

Kimsingi ushirikiano na chama hicho unatazamwa kama ni mstari mwekundu au hatari kwa demokrasia alau katika ngazi ya kitaifa katika siasa za Ujerumani.

Lakini ndani ya Umoja wa Ulaya tangu Brussels mpaka Strasbourg, suali kubwa limezuka ikiwa kweli bado wanasiasa wa vyama vya siasa za wastani za mirengo ya kulia waamini  katika kuvitenga vyama vya siasa kali au vinazidi kuvitegemea vyama hivyo kupata wingi wa kupitisha sheria pale ambapo inahitajika?

Je chama cha EPP kinaweza kubadilisha mwelekeo?

Sauti zinazidi kuongezeka kuhusu suali hilo baada ya ripoti kuonesha kwamba wabunge kutoka chama cha wananchi wa Ulaya, EPP(European Peoples Party) ambacho ndio kundi kubwa katika vyama vya siasa za wastani za mrengo wa kulia kwenye bunge la Ulaya, walishirikiana na makundi ya vyama vya siasa kali za mrengo wa kulia kabla ya kupigwa kura kuhusu sera za uhamiaji barani Ulaya, sambamba na mependekezo ya kile kinachoitwa ''vituo vya kuwarudisha wahamiaji'' nje ya kanda ya Umoja wa Ulaya.

Uhispania Madrid 2025 | Mkutano wa pamoja wa viongozi wa vyama vya Kizalendo barani Ulaya pamoja na Viktor Orban na Marine Le Pen
Vyama vya siasa za wastani za mrengo wa kulia vinazidi kuonekana vikishirikiana na vile vya siasa kali za mrengo wa kulia katika bunge la Ulaya.Picha: AlterPhotos/ABACA/IMAGO

Umuhimu wa ripoti hiyo sio tu imeonesha kwamba vyama vya siasa kali vya mrengo wa kulia vilipiga kura sawasawa na vile vyasiasa za wastani za mrengo wa kulia lakini ni ule ukweli kwamba huenda hata walifanya mawasiliano na kukubaliana kabla ya kura hiyo.

Na kutokana na hilo inaonesha kwamba hali halisi ya mitizamo ya kisiasa inakwenda mbali zaidi ya kisa hicho kimoja kuhusu kura kuhusu sera za uhamiaji.

Inaleta maswali mengi kuhusu ikiwa kundi la EPP linaanza kujenga utaratibu mpya wa uongozi ambao ni wa kushirikiana na wanasiasa wa siasa za wastani wanaounga mkono Ulaya na wakati mwingine kubadilika na kujiegemeza kwa wanasiasa wa mirengo mikali ya kulia pale yanapojitokeza maslahi yao 

Kwa nini chama cha AfD ni maarufu mashariki mwa Ujerumani ?

Wataalamu wakiri mabadiliko ya muundo

Nicolai von Ondarza mtaalamu kuhusu taasisi za Ulaya, kutoka taasisi ya kijerumani inayohusika na masuala ya kimataifa na usalama SWP anahoji kwamba hiki sio kisa kimoja tu, bali ni ishara  inayoonesha mabadiliko ya kimuundo kuhusu namna bunge la Ulaya linavyofanya kazi.

Mtalaamu huyo ameiambia Dw kwamba bunge la Umoja wa Ulaya liko kwenye mwelekeo wa kufikia hali kama ile inayoshuhudiwa kwa baadhi ya serikali za mataifa yanayoongozwa na kile kinachoitwa serikali ya wachache.

Kwa maneno mengine anasema, chama cha EPP kinazidi kuonekana kuchagua kati ya mambo mawili ya kumpatia wingi wa viti bungeni. Moja, ama kufuata mfumo wa kawaida wa kushirikiana na vyama vinavyopendelea Umoja wa Ulaya ambavyo ni vyama vya Kisoshalisti na Waliberali au kupata wingi huo kwa kushirikiana na vyama vya mrengo wa kulia.

Picha ya pamoja | Alice Weidel na Victor Orban
Picha ya pamoja ya Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Orban na Alice Weidel wa chama cha mrengo mkali wa kulia nchini Ujerumani, AfDPicha: Thomas Lohnes/Getty Images | Thomas Coex/AFP/Getty Images

Vyama vinavyopendelea Ulaya bado vina nguvu

Na hiyo haimaniishi kwamba bunge kwa ujumla wake limejiegemeza upande huo. Ondarza ametilia mkazo kwamba zaidi ya asilimia 80 ya maamuzi katika bunge hilo bado yanafanywa na vyama vikubwa vilivyozoeleka vinavyopendelea Umoja wa Ulaya ambavyo vina wingi.

Lakini anakumbusha, kwamba mabadiliko muhimu yanayoshuhudiwa ni kule kuonekana kwamba vyama vya siasa kali za mrengo wa kulia sio tena mwiko kushirikiana navyo.

Na mtaalamu mwingine Sophia Russack kutoka taasisi ya utafiti ya CEPS mjini Brussels anasema, ripoti hizi za karibuni kimsingi zinathibitisha tu kile ambacho wengi walikuwa wakikishuku. Kwamba kushirikiana na vyama vya siasa kali za mrengo wa kulia ni kitu kinachoanza kuwa cha kawaida.

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW