Israel yavamia meli zilizoekea Ukanda wa Gaza | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 31.05.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Timu Yetu

Israel yavamia meli zilizoekea Ukanda wa Gaza

Watu 15 wameripotiwa kuuawa na wengine 30 kujeruhiwa, baada ya wanamaji wa Israel kuvamia msafara wa meli sita za Kituruki zilizokuwa zimebeba misaada inayopelekewa Wapalestina katika Ukanda wa Gaza

default

Abiria aliyejeruhiwa kwenye meli ya Uturuki iliyokuwa ikielekea Ukanda wa Gaza baada ya kuvamiwa na wanajeshi wa Israel

Uturuki imekashifu vikali tukio hili ikisema Israel ilikiuka sheria za kimataifa kwa kuushambulia msafara huo. Ingawa Israel imesema imesikitishwa na mauaji hayo, Wizara ya mambo ya nje ya Uturuki imemuita kufika mbele yake balozi wa Israel nchini humo. Rais wa Mamlaka ya ndani ya Wapalestina Mahmoud Abbas ametangaza siku tatu za maombolezi ya kitaifa.

Hata kabla ya msafara huo wa meli karibu sita kuondoka kutoka Kusini mwa Cyprus hapo jana, tayari Israel ilikuwa imetoa kitisho kuwa itafanya kila njia kuuzuia msafara huo kuingia katika Ukanda wa Gaza, eneo ambalo Israel imekuwa ikilizingira kwa miaka mitatu.

Na naam ahadi hii waliitimiza- alfajiri wanamaji wa Israel walikuwa tayari katika bandari ya Gaza pale msafara huo ulipowasili- Makomando wa Israel waliizuia na kuingia katika meli iliyokuwa inaongoza msafara huo. Watu 15 waliuwawa na wengine 30 kujeruhiwa- baada ya wanamaji hao wa Israel kuwavamia wanaharakati waliokuwa ndani ya meli hiyo iliyopakia misaada.

Khalel Hamada ni msemaji wa vuguvugu linalopigania Israel kuondoka huko Gaza- Free Gaza- ambao ndio waliopanga safari hiyo ya misaada kuelekea Gaza alisema wamesikitishwa na shambulio hilo akilitaja kama la kikatili.

Lakini jeshi la Israel limejitetea kuwa walitumia nguvu baada ya kuvamiwa na watu waliokuwa ndani ya meli hiyo ya misaada.

Mjini Ankara nchini Uturuki- ilikuwa ni hamaki kutoka ngazi za kidiplomasia, mbali na shtuma kutoka kwa wanaharakati wa kutetea haki za kibinadamu na watu wa kawaida kwa jumla kuhusiana na shambulio hilo la Israel. Israel imejiharibia hadhi yake mbele ya macho ya kimataifa, ndio ilikuwa ujumbe kutoka Wizara ya mambo ya nje ya Uturuki. Na hasa shambulizi hili na mauaji hayo ya watu wasiokuwa na hatia pia yanaonekana yatatatiza zaidi uhusiano kati ya Israel na Uturuki ambaye ni mshirika mkuu wa Israel mashariki ya kati.

Wizara hiyo pia imemuita kufika mbele yake balozi wa Israel mjini Ankara kuelezea sababu ya kuvamiwa kwa meli hizo za misaada. Hata hivyo balozi huyo ameshindwa kuondoka kutoka makaazi yake- baada ya umati mkubwa wa wanaharakati kuandaa maandamano mbele ya makaazi yake mjini Ankara.

Mkuu wa sera za nje za Umoja wa Ulaya, Catherine Ashton amesema amesikitishwa na umwagikaji huo wa damu na kutoa wito wa kufanyika kwa uchunguzi kuhusiana na mauaji hayo.

Katibu Mkuu wa Muungano wa nchi za Kiarabu- Amr Mousa amelitaja shambulio hilo la Israel kama uhalifu dhidi ya binadamu.

Israel imekuwa ikilizingira eneo la Gaza- tangu mwaka wa 2007 baada ya Kundi la Hamas kuchukua uongozi wa eneo hilo. Mwishoni mwa mwaka wa 2008 Israel ililishambulia eneo la Gaza kwa madai ya kusitisha mashambulizi ya roketi yaliyokuwa yakirushwa katika miji ya Israel. Kiasi cha Wapalestina milioni 1 na laki tano wanaoishi katika ukanda huo wa Gaza wamekuwa wakitegemea misaada kwa mahitaji yao, na wamekuwa wakiishtumu Israel kwa kuzuiwa misaada kuingia katika eneo hilo.

Mwandishi: Munira Muhammad/ ARTRE, APE

Mhariri: Josephat Charo.

 • Tarehe 31.05.2010
 • Mwandishi Josephat Nyiro Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/NdfH
 • Tarehe 31.05.2010
 • Mwandishi Josephat Nyiro Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/NdfH

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com