Israel yarusha roketi kadhaa ukanda wa Gaza. | Redio | DW | 02.04.2010
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Redio

Israel yarusha roketi kadhaa ukanda wa Gaza.

Jeshi la Israel lasema lililenga karakana za silaha, Gaza

Vifusi katika eneo lililopigwa na roketi ya Israel mwezi Machi.

Vifusi katika eneo lililopigwa na roketi ya Israel mwezi Machi.

Naibu waziri mkuu wa Israel, Silvan Shalom, alisema katika redio ya serekali kwamba ikiwa mashambulio ya roketi hayatasitishwa na kundi la Hamas ndani ya mpaka wa Israel, basi watalivamia eneo la Gaza na watalazimika kuimarisha mikakati na operesheni ya kijeshi.

Shalom alisema anatumai uvamizi unaweza kuepukika, lakini ikiwa hawatakuwa na suluhisho lingine watautekeleza hivi karibuni.

Mkuu wa idara ya masuala ya dharura ya Palestina, Moawiya Hassanein, alisema watoto watatu wenye umri wa miaka miwili, minne na kumi na moja walipigwa na vifusi vya glasi katika mojawapo ya mashambulio sita yaliyotekelezwa na Israel usiku wa kuamkia leo. Hakukuwa na visa vingine vya majeruhi.

Kiongozi wa kundi la Hamas linalodhibiti ukanda wa Gaza, Ismael Haniya, ameilaumu Israel kwa kuzidisha hali ya wasiwasi.

Katika taarifa yake, Haniya alisema anaiomba jumuiya ya kimataifa kuingilia kati ili kukomesha uvamizi wa Israel.

Palästinenser Gaza Israel Raketenangriff auf Israel Hamas

Roketi za wanamgambo wa Kipalestina zilizolenga Israel.

Jeshi la Israel lilisema kwamba mashambulio yao yalijiri baada ya roketi iliyorushwa na wanamgambo wa Kipalestina kuanguka kusini mwa Israel katika mji wa Ashkelon jana jioni ingawa hakukuwa na visa vyovyote vya majeruhi.

Takriban roketi ishirini zimerushwa ndani ya mpaka wa Israel katika kipindi cha mwezi uliopita ikiwemo moja iliyomuua mkulima wa kutoka Thailand na iliyokuwa shambulio baya zaidi tangu kusitishwa kwa uvamizi wa siku ishirini na mbili wa Israel katika ukanda wa Gaza mwezi Disemba mwaka wa 2008.

Tangu vita hivyo vilivyosababisha vifo vya Wapalestina 1,400 na Waisraeli 13, Israel imekuwa ikijibu kwa mashambulio ya roketi ikiwemo uvamizi wa angani katika shimo za chini kwa chini zinazotumiwa na Wapalestina kusafirisha mizigo katika biashara ya magendo.

Waffenruhe Israel Gaza Panzer im südlichen Israel

Jeshi la Israel lailaumu kundi la Hamas kwa mashambulio ya roketi ndipo likalipiza kisasi.

Mashambulio ya jana usiku ya Israel yalilenga eneo la Khan Yunis kusini katika Gaza. Mashambulio mawili yalilenga kituo cha kikosi cha wanamgambo wanaounga mkono Hamas cha Ezzedine al-Qassam.

Kulingana na Hamas na walioshuhudia, shambulio lingine lililenga karakana katika kambi ya wakimbizi ya Nuisserat eneo la kati ya Gaza.

Jeshi la Israel lilisema kwamba lilipiga karakana za kutengeza silaha kaskazini mwa ukanda wa Gaza na lingine katika eneo la kati linalotumiwa kuhifadhi silaha.

Mashambulio hayo ya roketi yanajiri huku kukiwa hali ya wasiwasi kitanda kutokana na hofu ya Waarabu kwamba Israel inapania kusongesha mpaka wake hasa mashariki mwa mji wa Jerusalem mashariki na kumekuwa na uvamizi mpakani mwa Israel na Gaza.

Siku ya jumanne wiki hii mvulana wa Kipalestina aliuawa na wengine kujeruhiwa baada ya wanajeshi wa Israel kufyatua risasi dhidi ya waandamanaji mpakani.

Wanajeshi wawili wa Israeli waliuawa pamoja na Wapalestina waliokuwa wamejihami katika mapigano mapya mwishoni mwa juma lililopita katika ukanda wa Gaza.

Mwandishi, Peter Moss/AFP

Mhariri, Othman Miraji