Israel yajibu shambulio la bomu la Hamas. | Matukio ya Kisiasa | DW | 28.01.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Israel yajibu shambulio la bomu la Hamas.

Hali ya wasi wasi imetanda katika Ukanda wa Gaza baada ya ndege za jeshi kushambulia eneo la mpakani baina ya Gaza na Misri .

default

Wanajeshi wa Israel -Bomu la kutegwa barabarani mjini Gaza lamuua mwanajeshi mmoja.


Shambulio hilo limevuruga utulivu ambao umekuwa ukishuhudiwa katika eneo hilo kwa muda wa siku kumi zilizopita.


Hatrua hiyo imetokea siku moja tu baada ya kuwasili mjumbe wa rais Barack Obama wa Marekani, George Mitchell, katika eneo la mashariki ya kati, kutoa msukumo zaidi kwa mpango wa amani katika eneo hilo.


Wakaazi wa mji wa Gaza sasa wamo mbioni tena kukimbilia usalama, kufuatia shambulio la mapema hii leo ambalo limezua kumbukumbu ya dhiki ya mateso waliopitia kwa muda wa wiki tatu za mashambulio, pale wanajeshi wa Israel walipoingia Gaza disemba 27.


Israel inasema kuwa ililazimika kutekeleza shambulio hilo, kujibu shambulio la bomu lililotegwa kando ya barabara lililomuua mwanajeshi mmoja wa Israel hapo jana.


Ndege za Israel zilishambulia mahandaki na njia za chini ya ardhini katika mji wa mpakani wa Rafah na kumuua Mpalestinha mmoja anayedaiwa kupanga shambulio hilo.

Msemaji wa jeshi la Israel alithibitisha kwamba ndege za Israel zilishambulia maeneo yanayotumiwa na Hamas kuingiza silaha Gaza.

Pande zote mbili sasa zinalaumiana kwa kukiuka tangazo la kusimamisha mapigano, huku Israel ikisema kuwa bado inatafakari kitendo hicho na kwamba haitasita kujibu shambulio lolote kutoka kwa Hamas katika kutekeleza haki aya kuwalinda raia wake..


Waziri mkuu wa Israel, Ehud Olmert, anatarajiwa kukutana na baraza la usalama nchini humo,kujadilia jinsi nchi hiyo itakavyokabiliana na kitisho hicho cha hivi punde.

Hata hivyo, waziri huyo mkuu alisema kuwa anatarajia mazungumzo atakayofanya na mjumbe wa Marekani, George Mitchell, hivi leo yatakuwa na manufaa makubwa.

Olmert alisema ´´ Nafahamu kwamba wakati Bwa Obama amemtuma mjumbe wake nchini Israel, sio kwa lengo la kuja kuvutana nasi bali kushirikiana kwa njia za kirafiki kutafuta uwezekano wa kuleta maelewano na Wapalestina kutekeleza maelewamo´´.


Shambulio la hivi punde ni changamoto kubwa kwa mjumbe huyo anayesifika kwa kuleta amani kwa mzozo wa Ireland Kaskazini. Aliwasili jana mjini Cairo akiwa na ujumbe maalum kutoka kwa Rais Barack Obama kwamba wakati sasa umewadia kwa pande hizo mbili kurejea katika meza ya mazungumzo ili amani ya kudumu ipatikane katika eneo hilo la mashariki ya kati.

George Mitchell alisema ``nafikiri mojawapo ya kosa kubwa lililofanyika katika siku za nyuma ni kuwekwa muelekeo wote katika suala la Iraq, na kupuuza mzozo wa Waisrael na Wapalestina na nadhani hilo litabadilika katika utawala mpya´´.


Rais wa Palestina, Mahmud Abbas, akizungumza mjini Ramallah katika eneo la ukingo wa Magharibi, alionya kuwa huenda akabadili msimamo wake kufuatia shambulio hilo la Israel. Alikitaja kitendo hicho kuwa kwenda kinyume kabisa na harakati za kutafuta amani katika eneo la Gaza.


Israel ilitekeleza mashambulio makali dhidi ya Hamas katika eneo la Gaza lililosababisha Wapalestina 1,3000 kuuawa na wengine 5000 kujeruhiwa.Misri inaongoza mpango wa amani baina ya pande hizo mbili, mpango unaoitaka Israel kufungua maneo yote ya mpakani na kuondoka kabisa katika eneo la Ukanda wa Gaza.


Kwa upande wake, Israel inataka Hamas kukomesha mashambulio ya mizinga ya maroketi dhidi yake na maeneo hayo ya mpakani yasimamiwe ili kuwazuia wanaharakati wa Hamas kuingiza silaha kimagendo.

Ponda/Afp, Reuters

 • Tarehe 28.01.2009
 • Mwandishi Eric Kalume Ponda
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/GhnL
 • Tarehe 28.01.2009
 • Mwandishi Eric Kalume Ponda
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/GhnL
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com