Israel yaidhinisha ujenzi wa makaazi mapya | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 18.11.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Timu Yetu

Israel yaidhinisha ujenzi wa makaazi mapya

Israel imeidhinisha ujenzi wa mamia ya makaazi mapya ya walowezi wa Kiyahudi, katika eneo ililolinyakua la Waarabu la Jerusalem ya mashariki.

Eneo la ujenzi wa makaazi ya walowezi wa Kiyahudi, Jerusalem ya Mashariki.

Eneo la ujenzi wa makaazi ya walowezi wa Kiyahudi, Jerusalem ya Mashariki.

Hatua hiyo imezusha shutuma za mataifa ya magharibi kwa kuzidi kuhatarisha juhudi za kutafuta amani Mashariki ya Kati ambazo tayari ziko mashakani.

Wizara ya mambo ya ndani ya Israel imesema kwamba imeidhinisha ujenzi wa makaazi mapya 900 huko Gilo mojawapo ya madarzeni ya makaazi ya walowezi Jerusalem ya mashariki katika hatua ambayo imezima wito wa Wapalestina unaoungwa mkono na serikali ya Marekani wa kutaka kusitishwa kabisa kwa ujenzi mpya wa makaazi hayo kabla ya kuanza kwa mazungumzo mapya ya amani.

Marekani kwa haraka ilielezea kutofurahishwa kwake na uamuzi huo.

Robert Gibbs msemaji wa Ikulu ya Marekani amesema 'Tumefadhaishwa na uamuzi wa kamati ya mipango ya Jerusalem kuendelea na mchakato wa kuidhinisha utanuzi wa Gilo huko Jerusalem. Wakati tunashughulikia kuanzisha tena mazungumzo hatua hizo zinafanya iwe vigumu zaidi kwa juhudi zetu kufanikiwa.'

Repoti za vyombo vya habari za Israel zimesema kwamba Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu amekataa ombi kutoka rafiki yao wa Marekani kusitisha ujenzi huko Gilo. Haifahamiki wazi iwapo ombi hilo hususan lilihusika na mradi huo uliodhinishwa hapo jana.

Kauli ya Katibu Mkuu wa UM

Akiyaita makaazi hayo kuwa sio halali Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ameiomba Israel kuheshimu ahadi zake za kusitisha shughuli zote za ujenzi wa makaazi kwa kuzingatia mchakato wa Ramani ya Amani kati ya Israel na Wapalestina chini ya kile kinachoitwa kuwa ufumbuzi wa mzozo wa Mashariki ya kati kwa kuwepo mataifa mawili la Palestina na Israel.

Msemaji wake amesema Ban anaamini kwamba hatua hizo zinadhoofisha juhudi za kufikiwa amani na kuweka mashaka juu ya uwezekano wa kupatikana ufumbuzi kwa kuwepo kwa mataifa hayo mawili.

Kuidhinishwa kwa makaazi hayo mapya yumkini kukaharibu zaidi juhudi za Marekani ambazo tayari zimekwama kuwarudisha tena Waisrael ma Wapalestina katika meza ya mazungumzo huku kukikuwepo sitafahamu kubwa juu ya suala tata la maakazi ya walowezi wa Kiyahudi.

Madai ya Wapalestina

Wapalesstina wanadai Israel isitishe ujenzi wote wa makaazi ya walowezi katika eneo inalolikalia kwa mabavu la Ukingo wa Magharibi ikiwa na pamoja na Jeruslam ya mashariki ilioitwaa kabla ya kuanza upya kwa mazungumzo lakini hadi sasa Israel imekubali kupunguza kidogo tu ujenzi huo.

Wapalestina wanasema tangazo hilo la Israel ni pigo jipya kwa juhudi za amani.

Mpatanishi mkuu wa Wapalestina Saeb Erakat amesema Mamlaka ya Wapalestina inalaani vikali uamuzi huo na kwamba ujenzi wa makaazi hayo lazima uzuiliwe na kuwa hiyo ni njia pekee ya kurudi tena katika mchakato wa kweli wa kutafuta amani.

Rais Mahmoud Abbas wa Wapalestina amesema mkwamo huo umemfanya awe hana chaguo isipokuwa kutafuta utambuzi wa kimataifa wa taifa la Palestina juu ya kwamba Ulaya na Marekani zimekataa kushajiisha hatua hiyo.

Baada ya mazungumzo yake mjini Cairo na Rais Housni Mubarak wa Misri amekaririwa akiuliza 'ufumbuzi kwoa ni nini? Kuendelea kukwama kama hivyo bila ya kuwepo katika amani?' Amesema hiyo ndio sababu iliomfanya achukuwe uamuzi huo.

Maafisa wa Wapalestina mapema wiki hii walisema wanakusudia kuliomba Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kulitambua taifa hilo hatua ambayo wachambuzi wengi wanasema imekusudia kuishinikiza Israel na juhudi za kutafuta amani za Marekani zinazozorota.


Mwandishi:Mohamed Dahman /AFP

Mhariri: Abdul-Rahman


 • Tarehe 18.11.2009
 • Mwandishi Mohamed Dahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/KaA6
 • Tarehe 18.11.2009
 • Mwandishi Mohamed Dahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/KaA6
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com