1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel, Hamas zakomalia misimamo yao vita vya Gaza

26 Machi 2024

Kundi la Hamas limekataa pendekezo la hivi karibuni zaidi lililowasilishwa kwake na wapatanishi wa kimataifa kuhusu usitishaji vita na kuwachiliwa kwa mateka, huku Israel ikikosoa azimio la Baraza la Usalama la UN

https://p.dw.com/p/4e7hw
Ukanda wa Gaza | Ramadhani | Iftar katika eneo la Deir al-Balah
Watu wa Gaza wamefungaRamadhani chini ya kiwingu cha mashambulizi ya kila siku ya Israel.Picha: Ashraf Amra/Anadolu/picture alliance

Wakati vita vya Gaza vikiingia mwezi wa sita, kila upande umesisitiza hadharani kwamba dhana yake ya ushindi iko karibu, na Jumatatu jioni walikataa juhudi za karibuni za lkimataifa za kukomesha umuagaji damu.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema Israel inaweza kufanikisha malengo yake ya kuisambaratisha Hamas na kuwakomboa mateka ikiwa itatanua operesheni yake ya ardhini katika mji wa kusini wa Rafah, ambako zaidi ya nusu wa wakaazi wa Gaza wametafuta hifadhi, wengi wao wakiwa wamejirundika katika mahema ya muda.

Hamas imesema itaendelea kuwashikilia mateka hao hadi Israel ikubali usitishaji vita wa kudumu, kuondoa vikosi vyake kutoka Gaza na kuwaachia mamia ya wafungwa wa Kipalestina, wakiwemo wanamgambo wa ngazi ya juu.

Marekani | Baraza la Usalama la UN mjini New York | Azimio la kusitisha vita Gaza
Hatua ya Marekani kujiuwia kutumia kura yake katika Baraza la Usalama imeikasirisha Israel.Picha: Fatih Aktas/Anadolu/picture alliance

Ilisema Jumatatu jioni kwamba inakataa pendekezo la karibuni lisilozingatia masharti hayo, ambayo ikiwa yatatimizwa, yataliruhusu kundi hilo kudai ushindi wa gharama kubwa zaidi.

Soma pia: Baraza la Usalama lapitisha azimio la usitishaji mapigano Gaza

Hakuna matumaini ya kukoma kwa vita hivyo, ambavyo kwa mujibu wa wizara ya afya ya Gaza vimeua zaidi ya Wapalestina 32,000. Mapigano yameiacha sehemu kubwa ya Ukanda wa Gaza ikiwa magofu, kuwahamisha wakaazi walio wengi zaidi na kuwaweka theluthi moja katika hatari ya kufa kwa njaa.

Shambulizi ya Israel la Jumatatu jioni dhidi ya jengo la makaazi mjini Rafah ambako familia tatu za watu waliopoteza makaazi zilikuwa zinajihifadhi, liliuwa watu wasiopungua 16, wakiwemo watoto tisa na wanawake wanne, kulingana na rekodi za hospitali na ndugu wa marehemu. Mwandishi wa shirika la habari la Associated Press aliripoti kuona maiti hizo zikiwasilishwa hospitali.

"Tuliskia mlio wa roketi na hatukuweza kuona chochote. Walizungumzia kuilenga nyumba hii. Tulikuta kifusi juu yetu, namshukuru Mungu watoto wangu walipata tu majeraha madogo nilipowakagua," alisema Abu Jihad, mmoja wa wakaazi wa jengo lililoshambuliwa.

"Niliwatafuta majirani zetu na kukuta vipande vya miili yao. Nilibeba mashahidi sita mimi mwenyewe, wote walikuwa watoto, wenye umri wa miaka sita, minne, mitatu, mbali na kichanga cha karibu mwezi mmoja na nusu," aliongeza.

Mapacha vichanga wauwawa Gaza

Israel yaghadhabishwa kuachwa solemba na mshirika

Siku ya Jumatatu, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilifanikiwa hatimaye kupitisha azimio linalotaka kusitishwa kwa vita hivyo baada ya Marekani kujizuwia kutumia kura yake ya turufu, hatua iliyoikasirisha Israel, na kupelekea waziri mkuu wake Benjamin Netanyahu kufuta ujumbe uliokuwa umepangiwa kwenda Marekani jana kujadili hatua mbadala kwa operesheni ya ardhini Rafah, na namna ya kuwasilisha misaada ya kiutu Gaza.

Soma pia: Israel yazingira hospitali mbili zaidi zilizoko mji wa Khan Younis

Azimio hilo linataka kuwachiliwa kwa mateka wote wanaoshikiliwa Gaza lakini halifungamanishi sharti hilo na usitishaji vita.

Waziri wa Mambo ya nje wa Israel, Israel Katz, aliiambia redio ya jeshi Jumanne kwamba azimio hilo linaipa kiburi Hamas kwa kuashiria kwamba shinikizo la kimataifa litahitimisha vita hivyo bila kuilazimisha kutoa muafaka wowote.

"Ujumbe uliowasilishwa kwa Hamas jana ni kwamba hauna haja ya kuharakisha," Katz alisema.

Haniyeh ziarani Tehrani kwa mazungumzo na maafisa wa Iran

Kiongozi mkuu wa kisiasa wa Hamas, Ismail Haniyeh, alifanya ziara mjini Tehran siku ya Jumanne, ambapo alikutana na waziri wa mambo ya nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian na maafisa wengine waandamizi, kwa mujibu wa shirika rasmi la habari la Iran, IRNA.

Kiongozi wa kisiasa wa Hamas Ismail Haniyeh
Kiongozi wa kisiasa wa Hamas Ismail HaniyehPicha: Iranian Foreign Ministry/ZUMA Wire/IMAGO

Hii ni ziara ya pili ya kiongozi huyo wa Hamas mjini Tehran, tangu kundi hilo linaloungwa mkono na Iran kufanya shambulio lisilo kifani dhidi ya Israel Oktoba 7, lililosababisha vifo vya watu karibu 1,160, wengi wao wakiwa raia kwa mujibu wa takwimu rasmiza serikali ya Israel.

Soma pia: Kiongozi wa Hamas asema mkataba wa amani lazima umalize vita

Ziara ya mwisho ya Haniyeh ilikuwa mapema mwezi Novemba, alipokutana na Kiongozi wa Juu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei pamoja na maafisa wengine. Iran ilisifu shambulio la Oktoba 7 kama "mafanikio", lakini ilikanusha ushiriki wowote wa moja kwa moja.

Chanzo: Mashirika