1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yakasirishwa na Marekani kujizuwia na kura ya Gaza

Bruce Amani
26 Machi 2024

Wanajeshi wa Israel wameendelea kupambana na wanamgambo wa Hamas huko Gaza licha ya kupitishwa kwa azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linalotaka usitishaji mara moja wa mapigano.

https://p.dw.com/p/4e771
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio la kusitishwa mapigano Gaza huku Marekani pekee ikijizuwiaPicha: Fatih Aktas/Anadolu/picture alliance

Baada ya zaidi ya miezi mitano ya vita, Baraza la Usalama kwa mara ya kwanza limepitisha azimio hilo huku Marekani ambayo ni mshirika mkuu wa Israel ikijizuwia kupiga kura hatua ambayo imeichukiza Israel.

Mara tu baada ya kura hiyo kupitishwa, Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alifuta ujumbe uliokuwa umepangiwa kwenda Marekani kujadili operesheni ya kijeshi mjini Rafah. Israel imesema hatua ya Marekani kujizuwia inaathiri juhudi zake za kivita na jitihada za kuwachiwa mateka.

Soma pia: Israel yazingira hospitali mbili zaidi zilizoko mji wa Khan Younis

Marekani ambayo ina kiti cha kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, na ina nguvu ya kura ya turufu, ilijizuwia kutumia kura yake hapo jana, na kusafisha njia ya kupita kwa azimio hilo, ambalo liliungwa mkono na wanachama wengine 14 wa Baraza hilo.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametaka azimio hilo kutekelezwa, na kusema kushindwa kulitekelezwa kutakuwa jambo lisilosameheka. Mjumbe wa Palestina Riyad Mansour, alipambana kuzuwia machozi wakati akisema kwamba azimio hilo linapaswa kuwa mwanzo wa mabadiliko makubwa katika kukomesha vita vya Gaza.