1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Guterres ashuhudia malori yaliyokwama kuingia Ukanda wa Gaza

23 Machi 2024

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelitembelea eneo la mpaka kati ya Misri na Ukanda wa Gaza na kushuhudia msururu mrefu wa takriban malori 7,000 ya misaada yaliyozuiliwa kuingia Gaza.

https://p.dw.com/p/4e3da
Misri| Ziara ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alipolitembelea eneo la mpaka kati ya Misri na Ukanda wa Gaza.Picha: Khaled Desouki/AFP/Getty Images

Akiwa katika eneo hilo, Guterres amesema umefika wakati kwa Israel kutoa "ahadi kamili"kuruhusu huduma za kibanadamu katika eneo la Gaza, huku akitoa mwito wa kusitishwa kwa mapigano mara moja pamoja na kuachiliwa kwa mateka wa Israel wanaoshikiliwa na Hamas huko Gaza.

Aidha Katibu Mkuu huyo ameahidi Umoja wa Mataifa utaendelea kufanya kazi na Misri ili "kuboresha" upelekaji wa misaada ya kiutu ndani ya Ukanda wa Gaza.

Ziara ya Guterres inafanyika wakati Israel inakabiliwa na shinikizo la kimataifa la kuitaka iruhusu misaada zaidi ya kibinadamu kuingia Gaza, ambayo imeharibiwa vibaya na vita vya zaidi ya miezi mitano kati ya nchi hiyo na kundi na Hamas.