1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yakaidi kitisho cha Trump cha Mlango wa Hormuz

7 Aprili 2026

Iran imewahimiza vijana kuunda uzio wa binadamu kwa kuyazunguka maeneo yake ya nishati na Rais wa nchi hiyo amesema watu milioni 14 wameitikia miito ya kujitolea kupigana.

https://p.dw.com/p/5Bm8w
Rais wa Marekani Donald Trump akiwahutubia waandishi habari katika Ikulu ya White House
Iran inakabiliwa na muda wa mwisho wa kuufungua Mlango-Bahari wa Hormuz lasivyo miundombinu yake ishambuliwePicha: Evan Vucci/REUTERS

Trump ametishia kushambulia kwa mabomu mitambo yote ya umeme na madaraja ya Iran ikiwa kufikia Jumanne saa sita usiku nchi hiyo haitaruhusu safari za meli kuanza tena kikamilifu kupitia mlango Bahari wa Hormuz. "Tuna mpango kwa sababu ya nguvu ya jeshi letu, ambapo kila daraja nchini Iran litaharibiwa ifikapo saa sita usiku wa kesho, ambapo kila kiwanda cha umeme nchini Iran hakitafanya kazi. Kitateketea, kitalipuka na hakitatumika tena. Namaanisha, kuangamizwa kabisa ifikapo saa sita usiku. Na itatokea kwa muda wa masaa 4 kama tukitaka. Hatutaki hilo litokee. Tunaweza hata kujihusisha na kuwasaidia kujenga upya taifa lao." Amesema Trump.

Mashambulizi mapya ya anga ya Marekani na Israel yameyalenga maeneo kote nchini Iran, na kuua karibu watu kumi na nne. Jeshi la Israel limesema lilishambulia kiwanda kimoja cha Iran huko Shiraz, ikiwa ni siku ya pili mfululizo kukipiga kituo kama hicho baada ya kushambulia kiwanda kimoja cha gesi asilia. Jeshi hilo limewaonya Wairan kwa lugha ya Kifarsi kuepuka kupanda treni siku nzima, ikiwezekana kwa kufichua maeneo ya reli yanayotarajiwa kulengwa.

Shambulio jingine liliupiga Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Khorramabad magharibi mwa Iran, na shambulio jingine katika jimbo la Alborz, kaskazini magharibi mwa Tehran, liliwaua watu 18, kulingana na vyombo vya habari vya serikali.

Kituo cha jeshi la angani la Iran cha Bushehr
Kituo cha jeshi la angani la Iran cha Bushehr kilishambuliwa na makombora ya Israel na MarekaniPicha: Vantor/AP Photo/picture alliance

Iran haijaonyesha dalili zozote za kusalimu amri huku Rais Masoud Pezeshkian akichapisha kwenye X kwamba Wairan milioni 14 wameitikia kampeni za vyombo vya habari vya serikali na ujumbe mfupi wa simu wakiwahimiza watu kujitolea kupigana iwapo Marekani na Israel watavamia ardhini – idadi hii ikiwa mara mbili ya takwimu zilizopita. Alireza Rahimi ni Mkuu wa masuala ya Vijana katika Baraza Tawala la Iran. "Ninawahimiza vijana wetu wote, wanamichezo, wasanii, wanafunzi, wanafunzi wa vyuo vikuu, na maprofesa. Jumanne saa 8 mchana kuzunguka mitambo ya umeme ambayo ni mtaji wetu wa kitaifa, bila kujali msimamo wowote wa kisiasa, na ni mali ya mustakabali wa Iran na vijana wa Iran. Kusanyikeni ili kuuambia ulimwengu kwamba kushambulia miundombinu ya umma ni uhalifu wa kivita."

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ameonya Marekani kwamba mashambulizi dhidi ya miundombinu ya raia yamepigwa marufuku chini ya sheria za kimataifa, kulingana na msemaji wake. Trump, akizungumza na waandishi wa habari, alisema "hana wasiwasi wowote" kuhusu kufanya uhalifu wa kivita kwa mashambulizi kama hayo.

Ufaransa ilijiunga na sauti zinazoongezeka za kimataifa zainazotaka pande zote za vita kujizuia, huku Waziri wa Mambo ya Nje Jean-Noël Barrot akisema mashambulizi yanayolenga miundombinu ya raia na nishati "yanazuiwa na sheria za vita, sheria za kimataifa."

Daraja la King Fahd, linalounganisha Saudi Arabia na Kisiwa cha Bahrain
Daraja la King Fahd, linalounganisha Saudi Arabia na Kisiwa cha Bahrain lilifungwa kwa saa kadhaa kutokana na mashambulizi ya IranPicha: Naushad Kallivalappil/IMAGO

Mapema Jumanne, Tehran ilirusha makombora saba ya balestiki kuelekea Saudi Arabia, ambayo mamlaka ilisema yalidunguliwa na vifusi vikaanguka karibu na vituo vya nishati. Msemaji wa Wizara ya Ulinzi Meja Jenerali Turki al-Malki alisema uharibifu huo unatathminiwa.

Mashambulizi hayo yaliifanya Saudi Arabia kulifunga Daraja la Mfalme Fahd, linalounganisha Saudi Arabia na Kisiwa cha Bahrain kwa saa kadhaa. Daraja hilo la umbali wa kilomita 25 ndilo Barabara pekee ya kuunganisha Bahrain, ambako kuna kituo cha Kikosi cha 5 cha Jeshi la Wanamaji la Marekani, na Rasi ya Uarabuni.

Kwingineko, wanaharakati wameripoti wimbi jipya la mashambulizi mjini Tehran, ambalo baadaye Israel ilidai kuhusika. Watu tisa waliuawa katika jiji la Shahriar na wengine sita huko Pardis katika mashambulizi mengine ya anga, vyombo vya habari vya Iran viliripoti. Iran pia ilirusha makombora kuelekea Israel, huku kukiwa na ripoti za makombora yaliyoioingia Tel Aviv na Eilat.

Wakati muda wa mwisho uliowekwa na Trump ukikaribia, juhudi bado zinaendelea kufikia suluhisho la mazungumzo. Ingawa Iran imekataa pendekezo la hivi karibuni kutoka Marekani, maafisa wanaohusika katika diplomasia wanasema kwamba mazungumzo bado yanaendelea.

AFP, AP, Reuters, DPA