Mashambulizi ya Israel na Marekani yawaua 25 Iran
6 Aprili 2026
Marekani na Israel zimeendelea kuishambulia Iran leo Jumatatu na kusababisha mauaji ya watu 25, huku Jamhuri hiyo ya kiislamu, ikijibu kwa kuvurumisha makombora dhidi ya vituo vya Israel na Marekani katika mataifa jirani ya Ghuba.
Mabomu yamevurumishwa mjini Tehran huku ndege za kijeshi zikisikika kwa saa kadhaa hewani wakati baadhi ya majengo yakishambuliwa. Moshi mkubwa ulionekana karibu na mji wa Azadi baada ya bomu moja kurushwa katika chuo kimoja cha masuala ya teknolojia cha Sharif.
Waziri wa ulinzi wa Iran amesema miongoni mwa waliouwawa katika mashambulizi ya leo ni mkuu wa ujasusi wa Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Iran, IRGC, Meja Jenerali Majid Khademi. Israel kupitia waziri wake wa ulinzi Israel Katz imetangaza pia mauaji ya Khademi na ikasema itaendelea na mashambulizi yake ikiwalenga viongozi wa utawala iliyouita wa kigaidi.
"Kama tulivyosema awali: Ikiwa mashambulizi ya makombora dhidi ya raia wa Israel yataendelea, Iran italipia gharama kubwa. Tutashambulia na kusambaratisha miundombinu yake ya nishati na uwezo wa kushambulia wa utawala huo wa kigaidi. Kwa pamoja tutaendelea kuwalenga viongozi hao magaidi na kushambulia maeneo ya kiusalama na ya kimkakati kote Iran.”
Haya yanajiri wakati Iran ikiushambulia mji wa Haifa nchini Israel.Watu wawili waliouawa waliopatikana chini ya vifusi vya jengo lililoporomoka. Hadi sasa bado waokoaji wanaendelea na shughuli ya kutafuta miili pamoja na manusura.