1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroMali

Mali yawashutumu maafisa wa jeshi kwa kushirikiana na waasi

Saleh Mwanamilongo
2 Mei 2026

Mamlaka za Mali zinafanya uchunguzi dhidi ya wanajeshi wanaotuhumiwa kuhusika katika mashambulizi ya pamoja ya wiki iliyopita dhidi ya kambi za jeshi kote nchini.

https://p.dw.com/p/5D9rE
Mali, Gao 2013 | Msafara wa kijeshi wa Ufaransa ukiwa njiani kuelekea Gao
Orodha ya washirika wanaoweza kuhusika inajumuisha wanajeshi watatu waliokuwa kazini, mwanajeshi mstaafu, na mwanajeshi aliyekuwa ame“fukuzwa” ambaye aliuawa katika mapigano karibu na kambi kuu ya jeshi la nchi hiyo huko Kati, kilomita 15 nje ya mji mkuu BamakoPicha: Pascal Guyot/AFP

Mamlaka nchini Mali zimesema baadhi ya maafisa wa jeshi walishirikiana na wanamgambo wa kijihadi na waasi wanaotaka kujitenga katika mashambulizi makubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa kwa zaidi ya muongo mmoja. Mashambulizi hayo yamelenga mji mkuu Bamako pamoja na maeneo mengine kwa wakati mmoja.

Kundi la waasi la Azawad Liberation Front (FLA) limesema limeteka kambi muhimu ya kijeshi katika mji wa Tessalit kaskazini mwa nchi, baada ya jeshi la Mali na washirika wake wa Urusi kujiondoa. Hili ni pigo jingine kwa utawala wa kijeshi unaoongoza Mali tangu mapinduzi ya mwaka 2020.

Uchunguzi wa mwendesha mashataka mkuu mjini Bamako umebaini ushahidi wa kuhusika kwa baadhi ya wanajeshi katika kupanga na kutekeleza mashambulizi hayo, huku pia wanasiasa wakitajwa kuhusika.

Wakati huo huo, wanamgambo wamezuia barabara zinazoingia Bamako, hali inayozidisha hali ngumu ya usafiri na usalama nchini humo.