Hillary Clinton waziri wa nje | Magazetini | DW | 02.12.2008
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Hillary Clinton waziri wa nje

Kuteuliwa Hillary Clinton waziri wa nje na Angela Merkel mwenyekiti wa chama cha CDU:

default

Angela Merkel baada ya kuchaguliwa.

Uchambuzi katika safu za wahariri wa magazeti ya leo ya Ujerumani umetuwama zaidi leo juu ya mada mbili:Mkutano mkuu wa chama-tawala cha CDU na kuchagliwa tena mwenyekiti Bibi Angela Merkel kwa wingi mkubwa.Mada ya pili ni rais-mteule wa Marekani Barack Obama kumteua rasmi mpinzani wake chamani Seneta Hilary Clinton kuwa waziri wake wa mambo ya nje .

Gazeti la Badische Zeitung kuhusu kuchaguliwa tena kuwa mwenyekiti Bibi Angela Merkel:Gazeti laandika:

"Bibi Angela Merkel amechaguliwa tena kuwa mwenyekiti wa CDU tena kwa wingi mkubwa.Lakini mtu asidanganyike na hasa Kanzela mwenye. Kuchaguliwa kwa 94.83% ni wingi mkubwa lakini, sio kuonesha imani mno kwake.Kinyume chake.Chama kimeingiwa na wasi wasi wakati huu na kinaingia katika mwaka ujao wa uchaguzi kwa hofu kubwa.Kwahivyo, hakuna chamani alietaka kumtimua mwenyekiti ambae heba ni njema na kutomchagua kungeiharibu heba hiyo."

Gazeti la HEILBRONNER STIMME linaandika kwamba, Bibi Angela Merkel anaelea kileleni mwa madaraka akionesha kuchaguliwa kwake tena kuwa Kanzela wa Ujerumani hakuna shaka yoyote. Gazeti laongeza:

"Kikiwa njiani kuelekea uchaguzi huo,chama cha CDU kimempa Bibi Merkel idhini yake tena kwa kishindo.Ni matokeo tu ya kura yanayodhihirisha mwanya kati ya wajumbe mkutanoni na Bibi Merkel .Msukosuko wa fedha na uchumi uliozuka ni mzigo usiotazamiwa na unakiumbisha chama huku na huko. Wakati wa hotuba nzima ya bibi Merkel, risala yake haiikuonesha kuitikiwa. Aliehutubia alionekana kuwa Kanzela mwenye wasi wasi na wala kabisa hakutamba...."

Likitugeuzia mada na kutuchukua katika uamuzi wa rais-mteule Barack Obama kumteua Bibi Hillary Clinton,mpinzani wake mkali wakati wa uchaguzi kuwa waziri wake wa nje,gazeti la Neue Ruhr/Neue Rhein-Zeitung laandika:

"Kwa kumteua Bibi Hillary Clinton waziri wake wa nje, Barack Obama ,amebainisha sifa zake za kiongozi wa dola.Alikuwa na sababu nyingi kumweka kando kabisa na Ikulu (Whiote House) mpinzani wake mkubwa ,lakini akiwa rais, ameamua kujenga daraja kuunganisha na kufukia mashimo yote yaliochimbwa wakati wa kampeni ya miaka 2 ya uchaguzi.

Kumteua Bibi Clinton hatahivyo, kuna hatari zake ,kwani kwa mara ya kwanza wizara ya nje ya Marekani inaingia mikononi mwa mtu ambae tayari ana heba na nguvu.Kwani, nyuma ya Hillary Clinton, kuna wapigakura milioni 18 waliomchagua wakati wa kampeni na sehemu kubwa pia ya wanachama wa Democratic Party wako nyuma yake.Itavutia sana kuangalia vipi (First Lady) ,mke wa zamani wa rais Bill Clinton,anavyorejea serikalini.Hata ikiwa wizara ya nje kwake yeye ni kifuta-machozi, atalipanda jukwaa la ulimwengu akiwa nyota inayonawiri.

Gazeti la NEUE TAG likiendeleza mada hii laandika kwamba, kidogo mtu anastaajabu kwa uamuzi wa Obama kwa Hillary:Laongeza:

"Barack Obama aliahidi mageuzi na sasa anarudisha serikalini sura zile zile za zamani .Hilary Clinton,Robert Gates na James Jones waliochaguliwa kuongoza siasa ya nje,ulinzi na usalama pamoja na mkongwe wa miaka 81 Paul Volcker anaeingia katika timu ya mabingwa wa fedha na uchumi-Obama hapo anatuambia nini - je,hayo ni mabadiliko ? Anataka mageuzi,lakini hataki kuvunja uhusiano."

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com