Hali ngumu inayowakabili wakimbizi wa kiafghan nyumbani | Masuala ya Jamii | DW | 27.02.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Masuala ya Jamii

Hali ngumu inayowakabili wakimbizi wa kiafghan nyumbani

Maelfu ya wakimbizi wa Kiafghanistan waliolazimishwa kuondoka Iran wanakabiliwa na hali ngumu nyumbani, katika makambi wanakoishi. Wengi wamejikuta bila ya ajira, makaazi wala mpango wowote wa serikali wa kuwasaidia.

Baadhi ya wakimbizi wa Afghanistan.

Baadhi ya wakimbizi wa Afghanistan.

Wengi miongoni mwa wakimbizi waliorejea nyumbani Afghanistan kutoka Iran waliikimbia nchi yao baada ya uvamizi wa iliokua Soviet Union au Urusi ya zamani, hali iliofuatiwa na vita vya kiraia. Hivi sasa wanaishi katika mahema yaliotengenezwa kutokana na amatambara ya nguo yakisaidiwa na mbao kuhimili upepo.

Karibu familia 400 zinaishi katikati ya eneo la mradi wa ujenzi wa makaazi la Chamany Babrak katika mji mkuu Kabul, ambako mahema kadhaa yako katikati ya tope, kukiwa hakuna maji wala umeme bali watu waliochafuka na watoto wasio na mavazi.

Sehemu hiyo inawakimbizi kutoka nchi jirani na kutoka miji mengine ya Afghanistan. Baadhi wanadai wamerudishwa kutoka Pakistan ambako waliishi na kufanya kazi miaka ya vita. Lakini mbali na wakimbizi wa kiafghan katika kambi hiyo, kuna wakimbizi kutoka Pakistan pia walioikimbia hali ya kisiasa nchini mwao.

hata hivyo idadi kubwa ni ya waafghan waliorudishwa kutoka Iran, ambako maafisa waliwafukuza maelfu ya waafghan miezi ya karibuni.

Katika nchi kama Afghanistan inayotapia ujenzi mpya baada ya miongo kadhaa ya vita, ajira ni haba. Wakati baadhi ya wakaazi wanamudu mara moja moja kupata kazi za ujira wa malipo ya siku,wengi wanalazimika kuomba.

Shirika la kuwahuduma wakimbizi la umoja wa mataifa na serikali ya Afghanistan zimeanzisha miradi ya kuwasaidia watu ambao wanarejea nyumbani kwa hiyari lakini sio waliofukuzwa kutoka nchi jirani.

Mmoja miongoni mwa waliolazimishwa kuihama Iran anasema, wanajeshi waliwaambia " kama hamrudi kwenu Afghanistan tutawaua." Baadae anasema Fazel Ghrias aliyeishi iran miaka 20, waliokataa kurudi nyumba zao zilichomwa moto."

Shirika la wakimbizi la umoja wa mataifa UNHCR linakadiria kuna karibu waafghan milioni moja waliorudi kutoka Iran 2001 na kwamba mwaka jana Iran ikawarejesha wengine 360,000 .

Shirika hilo na serikali ya Iran zote zinadai waliorejeshwa walikua wakimbizi ambao hawakuorodheshwa na hivyo walizingatiwa kuwa wako nchini kinyume cha sheria wakitafuta kazi .

Kutokana na hayo waliorejeshwa nyumbani wanazidi kukabiliwa na hali ngumu za kimaisha. mmoja wao katika kambi ya Chamany Babrak alisikika akisema " tunahitaji chakula na mbao za kujenga alau makaazi ya kuishi . hatuna mafuta, unga wala mkate, baadhi ni wagonjwa na hatuna matibabu. kwa kweli hatuna msaada wa aina yoyote na wala hatujui la kufanya ."


 • Tarehe 27.02.2008
 • Mwandishi Abdulrahman, Mohamed
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/DEJT
 • Tarehe 27.02.2008
 • Mwandishi Abdulrahman, Mohamed
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/DEJT
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com