1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Habari za Ujerumani: CDU yaongoza katika kura za Hesse

Iddi Ssessanga afpe, rtre,ape,epd,KNA
Imechapishwa 16 Machi 2026ilisahihishwa mwisho 16 Machi 2026

Chama cha Kansela Friedrich Merz, CDU, kinatarajiwa kuendelea kuwa chama chenye nguvu zaidi katika ngazi ya serikali za mitaa katika jimbo la kati la Hesse.

https://p.dw.com/p/5ATOH
Uchaguzi wa serikali za mitaa Hesse 2026 | Mfano wa karatasi ya kupigia kura katika kituo cha kupigia kura mjini Frankfurt
Karatasi za kupigia kura katika uchaguzi wa jimbo la Hesse ziliwapa wapiga kura chaguo mbalimbaliPicha: Andreas Arnold/dpa/picture alliance
Ruka sehemu inayofuata Unachohitaji kujua

Unachohitaji kujua

  • Vyama viwili vinavyotawala nchini Ujerumani, chama cha mrengo wa kati kulia cha CDU na chama cha mrengo wa kati kushoto cha SPD, vinaonekana kuendelea kuwa nguvu kuu za kisiasa baada ya uchaguzi wa serikali za mitaa katika jimbo la Hesse
  • Matokeo ya awali yanaonyesha kuwa chama cha mrengo mkali wa kulia cha AfD kimepata ongezeko la kura lililokuwa chini ya matarajio na kushika nafasi ya tatu

Huu ni muhtasari wa habari kuu na simulizi za kuvutia zinazohusu au kutoka Ujerumani siku ya Jumatatu, Machi 16, 2026:

Ruka sehemu inayofuata Migomo yatarajiwa kuathiri usafiri wa umma, uwanja wa ndege wa Berlin na Eurowings
16 Machi 2026

Migomo yatarajiwa kuathiri usafiri wa umma, uwanja wa ndege wa Berlin na Eurowings

Ujerumani | Mgomo wa wafanyakazi wa usalama katika uwanja wa ndege wa Cologne–Bonn
Migomo ya onyo ya mara kwa mara ni jambo la kawaida nchini Ujerumani wakati wa mazungumzo kati ya wafanyakazi na waajiriPicha: Ying Tang/NurPhoto/picture alliance

Chama cha wafanyakazi cha Verdi kimetangaza migomo ya onyo katika sekta ya usafiri wa umma katika majimbo kadhaa ya Ujerumani. Kwa mujibu wa chama hicho, mabasi na tramu hazitafanya kazi siku nzima ya Alhamisi katika majimbo ya Bavaria, North Rhine-Westphalia na Hamburg.

Asubuhi ya Jumatatu iliripotiwa kuwa migomo pia inaweza kufanyika katika majimbo ya Saarland na Brandenburg, ingawa matawi ya chama hicho katika maeneo hayo yamesema bado haijathibitishwa.

Katika jimbo la North Rhine-Westphalia, migomo ya onyo katika usafiri wa umma itafanyika pia katika maeneo mengi kuanzia Jumanne, mbali na siku ya Alhamisi.

Uamuzi kuhusu iwapo kampuni za usafiri katika jimbo la Hesse zitajiunga na mgomo huo unatarajiwa kutolewa mapema Jumatatu baada ya mazungumzo. Nchini Bremen, Verdi imesema uamuzi unatarajiwa Jumatano.

Wasafiri wanapaswa pia kutarajia usumbufu mkubwa katika uwanja wa ndege wa Berlin BER siku ya Jumatano. Jumatatu, chama cha Verdi kiliwataka wafanyakazi wa uwanja huo kushiriki mgomo wa onyo wa siku nzima baada ya kupokea ofa kutoka kwa waajiri ambayo chama hicho kiliitaja kuwa “haikubaliki.”

Wakati huo huo, migomo ya marubani pia inatarajiwa katika kampuni tanzu ya Lufthansa, Eurowings. Kwa mujibu wa chama cha marubani cha Vereinigung Cockpit, asilimia 94 ya wanachama waliopiga kura waliunga mkono kuchukua hatua za mgomo, ingawa tarehe maalum bado haijatangazwa.

https://p.dw.com/p/5AUzk
Ruka sehemu inayofuata Vita vya Iran si suala la NATO — serikali ya Ujerumani
16 Machi 2026

Vita vya Iran si suala la NATO — serikali ya Ujerumani

Vita vinavyoendelea Iran havihusiani na muungano wa kijeshi wa Magharibi wa NATO, na Ujerumani haitashiriki katika juhudi za kijeshi za kulinda usafirishaji wa kibiashara kupitia Mlango wa Bahari wa Hormuz, msemaji wa serikali ya Ujerumani amesema Jumatatu.

“Vita hivi havina uhusiano wowote na NATO. Hivi siyo vita vya NATO,” alisema Stefan Kornelius, akibainisha kuwa jukumu la muungano huo ni kulinda maeneo ya nchi wanachama wake na kwamba hakuna mamlaka ya kupeleka vikosi katika hali ya sasa.

Aliongeza kuwa, “Kadiri vita hivi vitakavyoendelea, hakutakuwa na ushiriki wowote — hata katika juhudi za kijeshi za kuhakikisha Mlango wa Bahari wa Hormuz unabaki wazi.”

NATO ni nini?

Kauli zake zinafanana na zile za Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Johann Wadephul alizotoa mjini Brussels siku hiyo hiyo.

“Sioni kwamba NATO imechukua uamuzi wowote katika mwelekeo huo au inaweza kuchukua jukumu la kulinda Mlango wa Bahari wa Hormuz. Kama ingekuwa hivyo, vyombo vya NATO vingeshughulikia suala hilo ipasavyo,” alisema Wadephul kabla ya mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Umoja wa Ulaya.

Rais wa Marekani Donald Trump amekuwa akishinikiza washirika wa Ulaya kusaidia kulinda njia hiyo muhimu ya usafirishaji wa mafuta, akionya kuwa vinginevyo NATO inaweza kukabiliwa na mustakabali “mbaya sana.”

Usafirishaji wa meli katika njia hiyo ya maji umesimama karibu kabisa kutokana na hofu ya mashambulizi ya Iran, kufuatia mashambulizi ya pamoja ya Marekani na Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

https://p.dw.com/p/5AUsu
Ruka sehemu inayofuata Makubaliano mapana Ujerumani dhidi ya kuingilia kati katika Mlango - Bahari wa Hormuz
16 Machi 2026

Makubaliano mapana Ujerumani dhidi ya kuingilia kati katika Mlango - Bahari wa Hormuz

Mazoezi ya NATO Steadfast Dart 2026 | Bayraktar TB3 na TCG Anadolu katika operesheni yao ya kwanza nje ya nchi
Licha ya kuwa na jeshi imara la majini, serikali ya Ujerumani imesema jeshi hilo halijaandaliwa kushiriki operesheni ya HormuzPicha: Dursun Aydemir/Anadolu Agency/IMAGO

Kauli za maafisa mbalimbali wa sera za kigeni nchini Ujerumani katika siku za hivi karibuni zinaonyesha kuwepo kwa upinzani mpana wa kisiasa dhidi ya wazo la kupeleka meli za kivita za Ulaya katika Mlango wa Bahari wa Hormuz kulinda usafirishaji wa kibiashara, kama alivyoomba rais wa Marekani Donald Trump.

Msemaji wa sera ya nje wa muungano wa vyama vya kihafidhina vya CDU/CSU unaoongozwa na Kansela Friedrich Merz amesema katika mahojiano na kituo cha redio cha Deutschlandfunk kwamba vikosi vya majini pekee havingeweza kuimarisha usalama wa mlango huo dhidi ya mashambulizi ya Iran.

Amesema Iran inaweza kwa urahisi kufanya mashambulizi ya makombora au droni kutoka katika ukanda wa pwani wenye wakazi wengi wa njia hiyo ya maji kati ya Iran na Oman.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Johann Wadephul pia alikataa kuhusika kwa kijeshi kwa Ujerumani katika eneo hilo siku ya Jumapili.

Mtaalamu wa sera za mambo ya nje wa chama cha mrengo wa kati kushoto cha Social Democratic SPD, Adis Ahmetovic, amesema licha ya uwezo wa jeshi la wanamaji la Ujerumani, kwa sasa halijaandaliwa kushiriki katika operesheni ya aina hiyo.

Kiongozi mwenza wa chama cha mrengo mkali wa kulia cha Alternative for Germany (AfD), Alice Weidel, pia aliiambia tovuti ya habari ya The Pioneer kuwa kupeleka “jeshi dogo la wanamaji la Ujerumani … kutakuwa ni jambo la kinadharia tu na lenye hatari kubwa.”

Usafirishaji wa meli kupitia Mlango wa Bahari wa Hormuz — njia muhimu inayotumika kusafirisha takribani theluthi moja ya mafuta ya dunia — umesitishwa karibu kabisa na Iran kufuatia mashambulizi ya Marekani na Israel.

https://p.dw.com/p/5AUio
Ruka sehemu inayofuata “Jitu la falsafa” — Katibu Mkuu wa UN Guterres kuhusu Jürgen Habermas
16 Machi 2026

“Jitu la falsafa” — Katibu Mkuu wa UN Guterres kuhusu Jürgen Habermas

Ugiriki, Athens 2013 | Jürgen Habermas katika Kongamano la Dunia la Falsafa
Habermas, anayeonekana hapa mjini Athens mwaka 2013, alikuwa mmoja wa wanafikra wenye ushawishi mkubwa zaidi wa nyakati zetuPicha: Louisa Gouliamaki/AFP/Getty Images

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, ameonesha masikitiko yake makubwa kufuatia kifo cha mwanafalsafa na mwanasosholojia wa Ujerumani Jürgen Habermas, aliyefariki dunia siku ya Jumamosi akiwa na umri wa miaka 96.

“Hakuna mwanafalsafa aliyekuwa na ushawishi mkubwa katika mtazamo wangu wa kisiasa katika maisha yangu yote kama Jürgen Habermas,” amesema Guterres katika taarifa iliyotolewa na ofisi yake ya habari siku ya Jumapili.

Guterres amemwelezea Habermas kama “jitu la falsafa na msomi halisi wa masuala ya umma.”

Amesema mchango wake katika fikra za kisiasa na kisheria, sosholojia, taaluma ya mawasiliano, nadharia ya hoja, lugha na usemi umechangia kwa kiasi kikubwa kuelewa asili na thamani ya jamii za kidemokrasia.

Kwa mujibu wa Guterres, ufafanuzi wa Habermas kuhusu demokrasia — miongoni mwa mambo mengine — kuwa ni “mtiririko endelevu wa mawasiliano kati ya watoa maamuzi wa kisiasa na jamii za kiraia,” una umuhimu mkubwa hasa katika nyakati za sasa.

“Leo kuliko wakati mwingine wowote, tunahitaji mwingiliano huu wa mara kwa mara — njia ya mawasiliano ya pande mbili kati ya siasa na wananchi — ili kuelewa vyema changamoto tunazokabiliana nazo na kupata suluhisho madhubuti,” amesema Guterres.

https://p.dw.com/p/5AU6i
Ruka sehemu inayofuata Benki ya Italia UniCredit yawasilisha ombi la kuinunua Commerzbank ya Ujerumani
16 Machi 2026

Benki ya Italia UniCredit yawasilisha ombi la kuinunua Commerzbank ya Ujerumani

Benki ya Italia UniCredit imesema imewasilisha rasmi ofa ya kuinunua benki ya Ujerumani Commerzbank yenye thamani ya euro bilioni 35, sawa na takribani dola bilioni 40.

UniCredit imesema ofa hiyo inalenga kuvuka kiwango cha umiliki cha asilimia 30 kinachotajwa katika sheria za ununuzi wa kampuni nchini Ujerumani, ingawa haitegemei kupata udhibiti kamili wa benki hiyo.

Kwa sasa UniCredit tayari ni mbia mkubwa zaidi katika Commerzbank.

Hatua hiyo inatarajiwa kukabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa uongozi wa Commerzbank, wawakilishi wa wafanyakazi pamoja na serikali ya Ujerumani.
 

https://p.dw.com/p/5AU2a
Ruka sehemu inayofuata Muungano tawala Ujerumani wakabiliwa na mtihani wa chaguzi kadhaa 2026
16 Machi 2026

Muungano tawala Ujerumani wakabiliwa na mtihani wa chaguzi kadhaa 2026

Uchaguzi wa kwanza kati ya chaguzi tano za majimbo mwaka huu tayari umefanyika katika jimbo la Baden-Württemberg, ambapo chama cha CDU cha Kansela Friedrich Merz kilishindwa kwa tofauti ndogo na chama cha Kijani.

Hata hivyo bado kuna chaguzi nne zijazo, huku chama cha mrengo mkali wa kulia cha Alternative for Germany (AfD) kikiangaliwa kwa karibu zaidi kutokana na kuongezeka kwa umaarufu wake kote nchini, hasa katika majimbo ya mashariki yaliyokuwa sehemu ya Ujerumani ya Mashariki ya kikomunisti.

Ifuatayo ni muhtasari wa chaguzi zinazotarajiwa kufanyika katika kile kinachoelezwa kama “mwaka mkuu wa uchaguzi” nchini Ujerumani, ingawa tarehe zote bado ni za muda:

Rhineland-Palatinate (Machi 22):
Jimbo la magharibi la Rhineland-Palatinate kwa sasa linaongozwa na muungano wa vyama vinavyojulikana kama “taa za barabarani” — chama cha mrengo wa kati kushoto cha Social Democratic Party (SPD, rangi nyekundu), chama cha Free Democrats (FDP, rangi ya njano) kinachounga mkono biashara, pamoja na chama cha Kijani.

Waziri mkuu wa jimbo hilo tangu mwaka 2024 ni Alexander Schweitzer, aliyekuwa waziri wa kazi wa jimbo hilo, ambaye alichukua nafasi ya mwenzake wa chama Malu Dreyer baada ya kujiuzulu kwa sababu za kiafya.

Katika uchaguzi wa mwaka 2021, SPD ilipata asilimia 35.7 ya kura, CDU asilimia 27.7, Greens asilimia 9.3, AfD asilimia 8.3 na FDP asilimia 5.5.

Hata hivyo kura za maoni za hivi karibuni zinaonyesha mabadiliko, huku CDU ikiongoza kwa tofauti ndogo dhidi ya SPD, wakati uungwaji mkono kwa AfD ukiongezeka zaidi ya mara mbili. FDP kwa upande wake imeshuka chini ya kizingiti cha asilimia 5 kinachohitajika ili kuingia bungeni.

Tazama yaliojiri miaka 30 baada ya Ujerumani mbili kuungana

Saxony-Anhalt (Septemba 6):
Jimbo la mashariki la linaongozwa na muungano wa CDU, SPD na FDP chini ya waziri mkuu wa CDU Sven Schulze, aliyerithi wadhifa huo Januari mwaka huu kutoka kwa mwenzake Reiner Haseloff.

Mwaka 2021, CDU kilikuwa chama chenye nguvu zaidi kwa kupata asilimia 37.1 ya kura, kikifuatiwa na AfD kwa asilimia 20.8. SPD ilipata asilimia 8.4, nyuma ya chama cha mrengo wa kushoto cha Left Party kilichopata asilimia 11. FDP ilipata asilimia 6.4 na Greens asilimia 5.9.

Kura ya maoni ya Januari kutoka taasisi ya Insa inaonyesha hali tofauti, ambapo AfD inaongoza kwa asilimia 39, ikifuatiwa na CDU kwa asilimia 26. Left Party ina asilimia 11, SPD asilimia 8, chama kipya cha mrengo wa kushoto BSW asilimia 6, huku Greens na FDP vyote vikiwa chini ya kizingiti cha asilimia 5.

Berlin (Septemba 20):
tangu mwaka 2023 linaongozwa na muungano unaoitwa jadi “muungano mkubwa” wa CDU na SPD chini ya meya mtendaji Kai Wegener, ambaye ana hadhi sawa na mawaziri wakuu wa majimbo mengine.

Katika uchaguzi uliorudiwa mwaka 2023 baada ya ule wa 2021 kubatilishwa, CDU ilipata asilimia 28 ya kura, SPD na Greens asilimia 18.4 kila kimoja, Left Party asilimia 12.2 na AfD asilimia 9.1. FDP kwa mara nyingine ilishindwa kufikia kizingiti cha asilimia 5.

Kura ya maoni ya Februari ya taasisi ya Insa inaonyesha AfD imeongeza umaarufu wake na ingeweza kupata takribani asilimia 17 ya kura kama uchaguzi ungefanyika sasa, na kuwa chama cha pili kwa nguvu baada ya CDU chenye asilimia 22. SPD iko karibu na asilimia 16, ikifuatiwa na Greens na Left Party kwa takribani asilimia 15 kila kimoja.

Joe Chialo Seneta wa chama cha CDU apongeza matokeo ya uchaguzi

Mecklenburg-Vorpommern (Septemba 20):
Jimbo la mashariki la Mecklenburg-Vorpommern, ambalo wakati mwingine huitwa Mecklenburg-Western Pomerania kwa Kiingereza, kwa sasa linaongozwa na muungano wa mrengo wa kushoto wa SPD na chama cha kijamaa cha Left Party chini ya waziri mkuu wa SPD Manuela Schwesig.

Katika uchaguzi wa mwaka 2021, SPD ilipata asilimia 39.6 ya kura, AfD asilimia 16.9, CDU asilimia 13.3, Left Party asilimia 9.9, Greens asilimia 6.3 na FDP asilimia 5.8.

Hata hivyo utafiti wa hivi karibuni wa taasisi ya Forsa unaonyesha AfD imepata ongezeko kubwa la uungwaji mkono hadi asilimia 37. SPD iko karibu asilimia 23, CDU na Left Party asilimia 13 kila kimoja, BSW asilimia 11 na Greens asilimia 5. Kwa mara nyingine, FDP iko chini ya kizingiti cha asilimia 5.

https://p.dw.com/p/5ATlQ
Ruka sehemu inayofuata Deutsche Bahn yalipa fidia ndogo kwa ucheleweshaji wa treni mwaka 2025
16 Machi 2026

Deutsche Bahn yalipa fidia ndogo kwa ucheleweshaji wa treni mwaka 2025

Ujerumani, Cologne | Mgomo wa onyo wa GDL | Ucheleweshaji na kufutwa kwa safari za treni
Huduma za treni za safari za masafa marefu huathiriwa zaidi na ucheleweshaji, hali inayosababisha malipo makubwa ya fidiaPicha: Jana Rodenbusch/REUTERS

Shirika la reli la taifa la Ujerumani Deutsche Bahn (DB) lililipa zaidi ya euro milioni 156, sawa na takribani dola milioni 178.5, kama fidia kwa abiria — au waliokusudia kusafiri — kutokana na ucheleweshaji na kufutwa kwa safari za treni mwaka 2025. Kiasi hicho ni kidogo ikilinganishwa na takribani euro milioni 197 zilizolipwa mwaka uliotangulia.

Mwakilishi wa DB amesema kupungua kwa malipo hayo huenda kumetokana kwa sehemu na kupungua kwa matukio ya kipekee kama vile migomo iliyoshuhudiwa mwaka 2024.
Hata hivyo, Michael Peterson, anayesimamia huduma za treni za masafa marefu, amesema fidia hizo bado ni mzigo mkubwa kifedha kwa kampuni hiyo.

Kwa mujibu wa DB, kulikuwa na madai ya fidia takribani milioni 6.2 mwaka 2025 — mara tatu zaidi ya mwaka 2019, ambapo euro milioni 52.6 zililipwa kama fidia.

Kuhusu huduma za treni za masafa marefu, kiwango cha kufika kwa wakati kilikuwa asilimia 59.4 mwezi Februari, ikimaanisha kuwa karibu asilimia 40 ya safari zilichelewa kwa angalau dakika sita katika vituo vilivyokuwa njiani.

Aidha, ni asilimia 65.3 tu ya abiria wa safari za masafa marefu waliofika katika vituo vya mwisho kwa kuchelewa chini ya dakika 15.

DB hulipa marejesho ya asilimia 25 ya nauli ya tiketi ya safari ya upande mmoja endapo ucheleweshaji utazidi dakika 60, na asilimia 50 ikiwa treni itachelewa zaidi ya dakika 120.

Mtandao wa reli nchini Ujerumani kwa sasa unafanyiwa ukarabati mkubwa baada ya miaka mingi ya kupuuzwa kwa miundombinu hiyo. Hata hivyo, inaripotiwa kuwa serikali ya muungano inayoongozwa na wahafidhina chini ya Kansela Friedrich Merz imepunguza baadhi ya ahadi zake kuhusu maboresho hayo.
 

https://p.dw.com/p/5ATjA
Ruka sehemu inayofuata Kesi ya mchongaji Mjerumani mkosoaji wa Putin yasikiliza hoja za mwisho
16 Machi 2026

Kesi ya mchongaji Mjerumani mkosoaji wa Putin yasikiliza hoja za mwisho

Ujerumani, Düsseldorf 2025 | Jacques Tilly katika maonyesho maalum ya “Freigeist” katika Makumbusho ya Jiji.
Jacques Tilly akiwa amesimama kando ya moja ya miundo yakePicha: Oliver Berg/dpa/picture alliance

Mahakama moja mjini Moscow leo inatarajiwa kusikiliza hoja za mwisho katika kesi inayomkabili mchongaji wa Ujerumani Jacques Tilly, anayeshtakiwa kwa kumkejeli rais wa Urusi Vladimir Putin kupitia sanamu za kejeli zilizotumika katika maandamano ya Carnival.

Kesi hiyo inasikilizwa bila mtuhumiwa kuwepo mahakamani, na hukumu pamoja na adhabu vinaweza pia kutolewa.

Tilly ameshtakiwa chini ya sheria za Urusi kuhusu kashfa pamoja na sheria zinazokataza kile kinachoitwa “propaganda ya mahusiano ya kimapenzi yasiyo ya jadi.”
Mashtaka mengine yanahusiana na madai ya kukosa kuheshimu hisia za kidini na kuchapisha taarifa zinazodaiwa na mamlaka kuwa za uongo kuhusu hatua za jeshi la Urusi nchini Ukraine.

Msanii huyo ameunda sanamu kadhaa zinazomlenga Putin, ambazo ziliwasilishwa katika gwaride za Carnival jijini Düsseldorf, ambako anaishi. Moja ya sanamu hizo ya mwaka 2024 ilimuonyesha Putin pamoja na Patriarki wa Kanisa la Kiorthodoksi la Urusi Kirill katika tukio la utani, huku nyingine ikimuonyesha Putin akiwa katika bafu la damu ya Waukraine, ikirejelea uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine.

Iwapo atapatikana na hatia, Tilly hatasafirishwa kwenda Urusi kutoka Ujerumani na hivyo hatakabiliwa na kifungo huko. Hata hivyo, huenda uhuru wake wa kusafiri ukapunguzwa na kulazimika kuepuka nchi zilizo na makubaliano ya kusalimishana watuhumiwa na Moscow.
 

https://p.dw.com/p/5ATSo
Onesha matokeo zaidi