Gedi ataka majeshi ya Umoja wa Mataifa kulinda amani Somalia | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 29.06.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Timu Yetu

Gedi ataka majeshi ya Umoja wa Mataifa kulinda amani Somalia

Waziri mkuu wa Somalia Ali Mohammed Gedi leo amelitaka baraza la usalama la Umoja wa Mataifa lipeleke majeshi ya kulinda amani nchini mwake.

Waziri mkuu wa Somalia Ali Mohamed Gedi

Waziri mkuu wa Somalia Ali Mohamed Gedi

Licha ya ombi lililotolewa na waziri mkuu wa Somalia, Ali Mohamed Gedi, wanachama wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa mjini New York wamemjibu wakisema wanataka kwanza kuona maendeleo ya kisiasa kuelekea kupatikana kwa amani nchini Somalia.

Balozi wa Uingereza katika baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, Emyr Jones Parry, amewaambia waandishi wa habari mjini New York kwamba jumuiya ya kimataifa inaunga mkono serikali ya waziri mkuu Ali Mohammed Gedi lakini inataka kuona maendeleo ya kisiasa kabla kufikiria kutuma kikosi cha kulinda amani Somalia.

´Si haki kusema fanyeni amani na nitakuja kuilinda´, amesema leo waziri mkuu Gedi wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini humo baada ya kulihutubia baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, waziri Gedi amesema si haki kupuza au kutozingatia haki za Wasomali.

Wanamgambo wa kiislamu wamekuwa wakipigana na majeshi ya serikali ya mpito ya Somalia na majeshi ya Ethiopia tangu mwezi Januari mwaka huu wakati walipofukuzwa kutoka mjini Mogadishu. Kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika bado kinasubiriwa kukamilika mjini humo. Waziri mkuu, Ali Mohammed Gedi, ameliambia baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuwa Somalia iko katika njia panda na huu ndio wakati mwafaka wa kuisadia nchi hiyo kulinda amani na usalama.

Bwana Gedi amesema Somalia inataka kuona kikosi cha Umoja wa Afrika, AMISON, kikibadilishwa na kuwa tume ya kulinda amani ya Umoja wa Mataifa, ombi linalolishinikiza baraza la usalama huku likiandaa kikosi cha pamoja kwa ajili ya eneo la Darfur nchini Sudan, kitakachojumulisha wanajeshi wa Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa.

Wanadiplomasia wanasema wanachama wote wa baraza la usalama isipokuwa Kongo walisita kuhusu kikosi cha amani kwa ajili ya Somalia, ingawa wanaiunga mkono serikali ya mpito ya Somalia.

Umoja wa Mataifa unaandaa mpango ambao huenda ukaruhusu kikosi cha wanajeshi 20,000 wapelekwe Somalia kulinda amani. Ripoti iliyowasilishwa na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, ilionya kwamba tume ya amani ya Umoja wa Mataifa nchini Somalia huenda ikakabiliwa na vitisho kutoka kwa makundi ya waasi na viongozi wa kimbari.

Pamoja na kuwa kazi hiyo ni ngumu, Ban Ki Moon, amekiri huenda pia ikawa hatari na yenye gharama kubwa. Tathmini ya kwanza inapendekeza kikosi kikubwa cha jeshi kilicho imara na kitakachokuwa kikienda kila pembe ya Somalia.

Juhudi za kimataifa za kuleta amani nchini Somalia zina historia mbaya ya kuuwawa kwa wanajeshi wa Marekani mnamo mwaka wa 1993 katika vita vilivyopewa jina la Black Hawk. Mauaji hayo yaliashiria kumalizika kwa tume ya amani ya Umoja wa Mataifa na Marekani iliyoondoka Somalia mwaka wa 1995.

 • Tarehe 29.06.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CB3A
 • Tarehe 29.06.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CB3A
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com